Chapter 9 - SURA YA TISA
UTENGENEZAJI WA PESA
Akishirikiana na Mices, Jonathan aliendelea na safari. Majengo yalizidi kuwa makubwa nao mtaa ulifurika na watu. Kutembelea kandokando mwa barabara kulikuwa rahisi, hata kwa wale waliokwenda kwa magoti. Alipopita jumba moja kubwa lililojengwa kwa matofali, alisikia mngurumo wa mashine ukitokea upande wa juu. Ile sauti kali na ya kasi kwake ulimpa kufikiri kuwa ilitoka kiwanda cha upigaji chapa. "Labda ni gazeti la mji huu", Jonathan alisema kwa sauti ya juu kana kwamba alimtarajia yule paka kumjibu. "Sawa! Naweza basi kujisomea yote kuhusu kisiwa hiki."
Haraka haraka Jonathan alipiga kona akiwa yuatafuta lango la kupaingilia na ndipo alipokutana na nusura kugongana na mke na mume waliovalia nadhifu wakiwa watembea kwenye barabara hiyo iliyotengezwa kwa mawe mawe huku wakiwa wameshikana mikono. "Tafadhali", aliomba Jonathan, "je, hapa ndipo panapotoleshewa magazeti ya mji huu?"
Yule bibi alitabasamu naye bwana akamkosoa Jonathan "Umekosea, kijana. Hii ni Afisi Rasmi ya Utengenezaji Pesa, siyo magazeti."
"Oh", alisema Jonathan kwa udhiko. Nilitumai kupata mtambo wa kupiga chapa ambao ungenifaa.
"Usifadhaike", yule bwana alisema. "Hakuna mtambo wa upigaji chapa ulio na manufaa kuliko hii afisi. Je, si ni hivyo mpenzi?" yule bwana alimpapasa yule bibi kwa mikono yake iliyovaliwa mifuko ya mikono. "Naam, hiyo ni kweli" alisema yule mke kwa kicheko. "Afisi hii huleta furaha nyingi kwa sababu ya pesa inazochapisha."
"Hilo laonekana ajabu", alisema Jonathan akiwa kavutiwa. "Pesa ni kitu ambacho kwa hakika kingenifurahisha sasa hivi. Lau kama ningeweza kuchapisha pesa fulani inge ....."
"Oh, hapana!" alisema yule bwana kwa kumpiga Jonathan. Huku akimwashiria kidole usoni alisema, "Sivyo ilivyo."
"Hasa", alisema yule mwanamke kwa kukubaliana na bwana yake. "Wachapishaji wa pesa ambao hawakuteuliwa na Baraza la Watawala wanabandikwa jina la 'waigaji' na wanafungwa. Hatutaki walaghai", Yule bwana aliinamisha kichwa chake kwa nguvu, ishara ya kukubaliana na yule mama. "Walaghai wanapochapisha pesa zao haramu na kuzitumia, kunakuwa na pesa nyingi sana zikitumika. Bei hupanda, mishahara, akiba, na malipo ya uzeeni hukosa thamani. Huu ni wizi wa hali ya juu!"
Jonathan alionyesha uso uliokunjamana. Ni nini ambacho hakuelewa? "Nilifikiri kuwa ulisema eti uchapishaji wa pesa nyingi huwafurahisha watu?"
"Ah, ndiyo, ni kweli", alijibu mama. "Isipokuwa ....."
" ......iwe ni uchapishaji pesa ulio rasmi", yule bwana aliingilia kati kabla bibi hajamaliza. Hawa wawili walijuana vema sana kiasi kwamba waliweza kukamilishiana semi. Yule mume alitoa kibeti kikubwa kilichotengenezwa kwa ngozi kutoka mfuko wa koti lake ambamo alitoa kipande cha karatasi ili kumwonyesha Jonathan. Akionyesha alama rasmi ya Baraza la Watawala, alisema, "Tazama hapa. Hii inasema 'fedha inayoruhusiwa na serikali', na hii inafanya pesa kuwa pesa rasmi."
Uchapishaji wa pesa rasmi unaitwa 'sera ya pesa', yule mama aliendelea, kana kwamba alikuwa akikariri kutoka kwa kitabu fulani pendwa cha shuleni. Sera ya pesa ni sehemu ya mpango mkuu."
Huku akikiweka kibeti chake, yule bwana aliongeza kusema, "Ikiwa ni rasmi, basi wale wanaopeana hii 'pesa inayoruhusiwa na serikali' si wezi."
"La hasha!" alisema mama. "Baraza la Watawala hutumia hii pesa iliyoruhusiwa kwa niaba yetu."
"Naam, na ni watu walio wakarimu sana", alisema kwa kukonyeza jicho. "Wanazitumia pesa hizo rasmi kwa miradi inayowafaidi watawaliwa wanyenyekevu hasa wale wanaowasaidia kuchaguliwa."
"Naomba niulize swali moja zaidi", aliendelea Jonathan. "Ulisema kuwa endapo pesa haramu ziko kila mahali, bei za bidhaa zinapanda, na mishahara, akiba, na malipo ya uzeeni hukosa thamani. Je, si hali hii pia hutokea pale palipo na pesa inayoruhusiwa na serikali?"
Huyo mke na mume waliangaliana kwa furaha. Bwana akasema, "Naam, bei za bidhaa hupanda, lakini sisi hufurahika Watawala wanapokuwa na nyingi za kutumia kwetu. Kunayo mahitaji mengi ya watu walioajiriwa, wasioajiriwa, waliotiliwa makatazo, wasiotiliwa makatazo, vijana, wazee, mafukara, na wasio fukara."
Mama aliongezea, "Watawala hufanya utafiti wa kina kuhusu vyanzo vya matatizo yetu ya bei. Tumetambua bahati mbaya na hali mbaya ya hewa kama ni vyanzo vikuu. Mabadiliko ya maumbile husababisha bei za bidhaa kupanda pamoja na kushukisha viwango vya maisha ----- hususan katika maeneo yetu ya misitu na mashambani."
"Ndivyo ilivyo!" mfuasi wake katika safari alisema kwa nguvu, "Kisiwa chetu kimezingirwa na mapinduko makubwa ya mambo ambayo huvuruga uchumi wetu kwa kufanya bei za bidhaa zipande. Kusema kweli bei za juu za mbao na chakula zitakuja kutusababishia kuanguka siku moja."
"Na kuhusu bei za chini", alisema kwa sauti ya juu. "Wapitanjia, na ushindani wao mbaya, wanajaribu kila mara kutuuzia mishumaa na makoti kwa bei zilizo za chini sana. Baraza letu la Watawala wenye busara huweza kuwaadhibu madubwana hawa pia." Huku akimgeukia mwenzake alijivuta kwenye mkono wa vazi lake.
"Umepiga ndipo", yule mume alimweleza. "Natumai utaturuhusu kuondoka, kijana. Tunayo miadi na mwana-benki wetu wa rasilmali. Lazima tupate kibunda kutokana na ardhi pamoja na madini yenye thamani. Njoo, mpenzi." Yule mwungwana aliinamisha kofia, bibi naye akainama kwa adabu, huku wote wawili wakimpa Jonathan kwaheri kwa uchangamfu.
© Copyright 2005,
Inter Region Economic Network, Nairobi, Kenya, All Rights Reserved.