Inter Region Economic Network, Nairobi, Kenya  

Home
About IREN
Media & Press
Projects
News & Newsletters
Articles
Events
Resources
Speeches and Publications
Student Outreach
Contact IREN

Chapter 10 - SURA YA KUMI


MASHINE YA NDOTONI

Jonathan angefikaje nyumbani? Alikuwa ni kijana mwenye afya njema na mwaminifu, aliyekuwa tayari kufanya kazi yo yote ile. Labda angebahatika kupata kazi na mabaharia wa meli. Ama kwa kweli kisiwa kilistahili kuwa na bandari pamoja na meli. Wakati akilitafakari suala hili, alimwona mume mmoja mkondefu aking'ang'ana kupakia mashine kubwa kwenye kochi kubwa lililokokotwa na farasi. Alijivalia suti nyekundu iliyong'ara sana na kofia iliyotengezwa kwa mtindo wa kisawasawa na ambayo ilikuwa na unyoya mkubwa ulitundikwa kwenye utepe. Kwa kumwona Jonathan, yule bwana aliita kwa sauti ya juu, "Wee, kijana, nitakulipa shilingi tano ukinisaidia kupakia mzigo huu"

"Shilingi?" alikariri Jonathan kwa hamu kubwa.

"Pesa, pesa taslimu. Wazitaka au la?"

"Nazitaka", alisema Jonathan, huku akiwa hajui jinsi ya kulikabili lile jukumu. Haikuwa kazi ya melini, lakini alihitaji kujikimu. Isitoshe, yule bwana alionekana mwenye busara na ambaye angempa ushauri. Baada ya kusukuma na kuburusha kwingi, walifanikiwa kunyanyua ile mashine isiyoshikika na kuiweka kwenye kochi. Huku akipanguzapanguza paji la uso wake, Jonathan alipiga hatua kadhaa nyuma akiwa yuahema na kuuangalia mzigo aliokuwa ameshughulikia. Mashine hiyo ilikuwa kubwa, ikiwa na violezo maridadi vilivyopakwa kote kote. Juu yake kulikuwa na pembe kubwa iliyofanana na ile ambayo Jonathan aliwahi kuona kwenye fonografu iliyotengezwa kwa mkono kule nyumbani kwao.

"Hizi ni rangi malidadi", alisema Jonathan, akiwa yuahisi kizunguzungu na huku akikodolea macho zile ruwaza zenye mafumbo zilizotikisika.

"Je ile pembe kubwa juu ya mashine ni ya nini?"

"Njoo huku mbele ili ujionee." Jonathan alilipanda lile kochi ambapo alisoma ishara iliyochorwa kwa herufi nzuri za dhahabu: "MASHINE YA NDOTONI YA GOLLY GOMPER."

"Mashine ya ndotoni", alikariri Jonathan, "Je, una maana kwamba mashine hii hufaulisha ndoto?"

"Naam" alisema yule bwana aliyekuwa na uso uliochongoka. Aliizungusha skrubu ya mwisho na kukitoa kibao kilichofunika mashine hiyo kwa upande wa nyuma. Ndani yake kulikuwa na kazi za fonografu sahii. Badala ya pao lililozungushwa kwa mkono, kulikuwa na springi iliyokuwa na funguo. Swichi iliweza kufanya kinanda kiimbe.

"Hamna cho chote isipokuwa kisanduku kikuukuu cha mziki!" alishangaa Jonathan. "Ulitarajia nini", alisema yule bwana, "msaidizi usiomtarajia?"

"Sijui. Nilidhani kuwa ingekuwa ya kustaajabisha kiasi. Kama ujuavyo, ni mambo spesheli yafanyayo ndoto za watu kufaulishwa."

Kicheko cha kijanja kilionekana usoni pa uso mwembamba wa mume huyu na ambaye alimwangalia Jonathan kirefu na kwa mkazo. "Maneno, rafiki yangu utakaye kujua. Maneno pekee huweza kufaulisha baadhi ya ndoto. Tatizo ni kuwa hujui kwa yakini kama ni nani atakayepata ufanifu wa ndoto unapotamani kitu fulani."

Kwa kuona jinsi Jonathan alivyoonyesha kuchanganyikiwa, yule mume alipiga mkono mfukoni ambamo alitoa kedi nyeupe ya biashara iliyokuwa imefikichika. Alijitambulisha kwa sauti ya king'ong'o isiyo na mwelekeo mwema. "Jina ni Tanstaafl. T.P Tanstaafl." Ni wakati huo ambapo alitambua kuwa alikuwa kampa Jonathan kedi ambayo siyo, ile iliyosoma "G.Gomber." Aliimpokonya. "Naomba samahani, mwanangu, hii ni kedi ya jana."

Huku akigurugusha kibeti chake, aliipata kadi nyingine iliyokuwa na ukubwa pamoja na rangi tofauti kidogo na ile ya kwanza na iliyokuwa na jina la siku ile. Kisha akatoa kibandiko kilichokuwa na uzuri wa herufi za dhahabu ambacho alibandika juu ya jina asilia kwenye kadi yake. Wakati huu ilisoma, "MASHINE YA NDOTONI YA DAKTA TANSTAAFL."


Yule bwana alieleza taratibu, "Watu wanazo ndoto zao, au siyo? Ni kwamba hawajui jinsi ya kuzifanya ndoto zao zifaulu, au siyo?" Dakta Tanstaafl aliinamisha kichwa chake kila aliposema "Au siyo?" Jonathan pia alianza kuinamisha kichwa chake pasi na kusema neno ili kumwitikia.

"Kwa hivyo wewe hulipa pesa, ukazungusha funguo, na kisha hili sanduku zee huitikia kwa maagizo laini tena na tena, au siyo?" Tanstaafl aliinamisha kichwa tena, naye Jonathan akafuatia kwa mkutuo. "Ujumbe ni ule ule ambapo wanaoota ni wengi ambao wangependa kuusikia, au siyo?"

"Ujumbe ni upi, bwana Tanstaafl?" aliuliza Jonathan, huku yuafahamikiwa na tendo lake la kukutua kichwa chake juu chini.

Yule bwana alimkosoa Jonathan, "Tafadhali! Dakta Tanstaafl. Jinsi nilivyokuwa nikisema, Mashine ya Ndotoni huwaambia watu wafikirie kile ambacho wangependa kupata, na ....." Yule bwana alipaangalia pale walipokuwa ili kuona kama kulikuwa na yeyote akisikiliza. "Halafu inawaelezea waota-ndoto kifaacho kufanywa ---- kwa jinsi ambayo ni ya kushawishi sana, au siyo?"

"Una maana kuwa inawatia katika hali ya kutenda mambo yanayoamriwa katika usingizi?" aliuliza Jonathan, akiwa ameyakodoa macho.

"Oh hapana!" alikana yule mume. "Inawaeleza kuwa ni watu wema na kuwa kile wanachokitamani ni kitu chema, au siyo? Ni nzuri sana kiasi kwamba wanaiomba kwa nguvu, au siyo?"

"Ni hivyo tu?" Jonathan alisema kwa hofu.

"Ni hivyo tu."

Baada ya kusita kwa muda, Jonathan aliuliza, "Ni kipi ambacho hawa waota-ndoto hutaka?

Bwana yule alitoa kopo la mafuta na kisha akapaka gia zilizokuwa ndani. "Naam, inategemea hasa na mahali ambapo naitia mashine hii. Mara nyingi huwa naiegesha mbele ya kiwanda kama hiki --- Bastiat Builders."

Alielekeza dole-gumba lake upande wa jumba lililochutama na lililokuwa la gorofa mbili upande wa pili wa barabara. "Na wakati mwingine huwa nikiegesha karibu na Ikulu ya Watawala. Karibu na hapa, watu hutaka pesa zaidi. Pesa zaidi ni kitu kizuri, wafahamu, maana bei za bidhaa hupanda kila uchao nao watu wahitaji bidhaa zaidi, au siyo?"

"Nimesikia ni hivyo", Jonathan alisema, huku akiwa yuafingirisha macho yake kwa huruma. "Je, wao huzipata?"

Yule mume alipiga hatua nyuma na kuipanguza mikono yake kwa kitambara kilichoraruka. "Baadhi huzipata ---- hivyo hivyo tu!" alisema kwa kualisha vidole vyake. "Waota-ndoto walikuja Ikulu na kutaka sheria ambazo zitawapa mishahara na maslahi mara tatu zaidi."

"Maslahi yapi?" aliuliza Jonathan.

"Kama vile usalama. Usalama zaidi ni kitu kizuri, au siyo? Kwa hivyo waota-ndoto walitaka sheria ambazo zingelazimisha viwanda kuwanunulia bima. Bima kwa ugonjwa. Bima kwa ukosefu wa ajira. Bima kwa kifo, au siyo?"

"Hali hiyo yaonekana ya ajabu!" alisema Jonathan kwa mshangao. "Haikosi waotaji-ndoto hao walifurahi sana." Aligeuka kukiona kiwanda ambapo aligundua kuwa hakukuwa na mengi yaliyokuwa yakiendelea pale. Rangi zilizochuchuka ziliyafanya majengo yale yaonekane makuukuu na hakukuwa na taa zilizowaka kutokea madirisha yake machafu na yaliyovunjika. Vipande vipande vya glasi vilivyovunjika vilitapakaa kandokando ya barabara.

Yule mume alimaliza kupaka mafuta mtambo wake, akaregesha kibao cha nyuma na kisha akafunga skrubu. Kwa matumizi ya kitambaa kilichoraruka alilipanguza sanduku pale alipopapaka mafuta, akaruka kutoka kwenye gari lile la magurudumu mawili na kisha akaenda kuangalia kigwe cha kuongozea gari lake. Jonathan aliruka kutoka garini na kumkabili yule bwana kwa kukariri, "Nilisema haikosi walifurahia sana ----- yaani kupata pesa zote hizo na bima. Na, pia walishukuru. Je walikupa nishani au kukuandalia karamu katika kusherehekea?"

"Hakukuwa na cho chote kama hicho", alisema Dakta Tanstaafl kwa haraka. "Nusura niuawe. Waliponea chupuchupu kuharibu Mashine yangu hafifu ya Ndotoni jana usiku kwa matumizi ya miamba, matofali, na cho chote kile walichoweza kurusha. Sasa, kiwanda chao kilifungwa jana ambapo wafanyakazi walinilaumu mimi."

"Mbona kiwanda kifungwe?"

"Yamkinika kiwanda hicho hakingeweza kuzalisha bidhaa ambazo zingeweza kugharamia nyongeza za wafanyakazi pamoja na maslahi yao mengine. Sasa hivi inabidi wenye kiwanda hiki watafute zana zingine ili wajaribu kuzalisha bidhaa nyingine."
"Lakini, sasa", alisema Jonathan, "hiyo ina maana kuwa ndoto hazikuwa. Endapo kiwanda kitafungwa, basi hapana anayepata cho chote! Kwa hivyo, wewe ni mlaghai tu. Ulisema kuwa Mashine ya Ndotoni ......."

"Achia hapo, mwanamume! Ndoto zilifaulu. Nilichokisema kilikuwa",

alisisitiza taratibu, "kuwa hujui hasa ni nani atakayefaulishiwa ndoto unapotamani kitu. Inafanyika hivi kwamba kila mara kiwanda cha zamani kinapofungwa hapa kwenye kisiwa cha Korampo, ndoto ile ile hufaulishwa upande wa pili wa maji haya kwenye kisiwa cha Nie. Juzi kumefunguliwa kiwanda kipya, muda wa safari ya majini ya juma moja tu kutoka hapa. Kule kunazo kazi nyingi pamoja na usalama. Ila kwangu, mimi hupata pesa kupitia machine hii bila kujali kinachotokea."

Jonathan alitafakari sana kuhusu mambo yale ya Nie, akitambua kuwa kumbe kulikuwa na kisiwa kingine tajiri kuliko hicho. "Je hiki kisiwa cha Nie kiko wapi?" aliuliza.

"Mashariki ya mbali baada ya upeo wa macho. Watu wa Nie wana kiwanda kama hiki. Gharama za viwanda zilipopanda hapa, viwanda vya kule vilipata agizo za bidhaa nyingi sana. Wao wanaelewa kwamba kuwa na wateja wengi ndiyo njia nzuri zaidi ya kupata cho chote kile kwa wingi wake ---- malipo na usalama. Wafanyakazi Korampo hawawezi kutaka zaidi kutoka kwa wateja wao. Hapana vitu kama vile mankuli ya mchana ya bure, wafahamu. Kila kitu sharti kiuzwe."

Dakta Tanstaafl alicheka huku akiifunga mashine yake kwa kamba. Alimlipa Jonathan kwa huduma zake na kisha akarukia kiti cha dereva na kuvuta kigwe. Jonathan aliziangalia pesa alizokuwa amepewa na kisha akawa na wasiwasi kuwa hazingefaa kitu. Ilikuwa ni ile ile pesa rasmi aliyoionyeshwa na yule mke na mume mbele ya Afisi Rasmi ya Utengenezaji Pesa. "We, Dakta Tanstaafl, ngojea!"

"Eti?"
"Naomba unilipe kwa kutumia aina nyingine ya pesa. Yaani, ile ambayo haitapoteza thamani yake."

"Ni pesa rasmi, rafiki. Ichukue. Je, wafikiri ningetumia pesa kama hizi lau kama kungekuwa na zingine? Nenda kaitumie haraka!" Yule bwana alimpigia makelele farasi wake na akaondoka.








© Copyright 2005,
Inter Region Economic Network, Nairobi, Kenya, All Rights Reserved.