Inter Region Economic Network, Nairobi, Kenya  

Home
About IREN
Media & Press
Projects
News & Newsletters
Articles
Events
Resources
Speeches and Publications
Student Outreach
Contact IREN

Chapter 11 - SURA YA KUMI NA MOJA


UUZAJI WA MAMLAKA

Pandikizi la jana-jike lenye furaha lilimsongelea Jonathan wakati akiwa amesimama asijue aende wapi sasa. Bila kusita, mwanamke huyo alimkamata mkono wake wa kulia na kuanza kuutikisa kwa nguvu. "U hali gani? Si leo ni siku njema?" alisema kwa mbubujiko wa kasi kubwa, huku akiwa bado yuautikisa mkono wa Jonathan kwa jikono lake nono. "Mimi ni Bibiye Bess Tweed, mwakilishi wako mpendwa kwenye Baraza la Watawala, na nitashukuru sana ikiwa utanipa mchango wako pamoja na kura yako itakayoniwezesha kuchaguliwa tena na hapo utakuwa umepiga ndipo, hiyo ndiyo hali inayosumbua jamii yetu nzuri."

"Kweli?" alisema Jonathan. Kasi na nguvu ya usemi wake vilimshutua Jonathan kiasi. Hakuwahi kukutana na mtu ambaye angeweza kusema maneno mengi kiasi hicho pasi na kusita.

"Ah, ndivyo", aliendelea Bibiye Tweed, bila kusikiliza jawabu la Jonathan, "na niko tayari kukulipa, ni nini kingine utakachotaka, au vipi?"
"Unilipe kwa kukuchangia na kukupigia kura?" Jonathan aliuliza huku uso wake ukionyesha kuchanganyikiwa.

"Bila shaka siwezi kukupa pesa ------ hiyo si haki, ni hongo ------- usitaje hiyo tena, usitaje hiyo tena!" alisema Bibiye Tweed, akiwa yuampigia kope kijanja na kumsukuma ubavuni akitumia kisugudi chake. Aliendelea, "Lakini naweza kukupa kitu kilicho kizuri kama pesa na ambacho thamani yake ni mara nyingi zaidi ya mchango wako kwangu. Ni rahisi kama vile kutema mate. Nitilie pesa chache mkononi sasa na utarajie mengi makubwa baadaye. Hilo ndilo nitakalofanya na sijui kama wewe waonaje?"

"Itakuwa ni sawa", alijibu Jonathan, ambaye alitambua wazi kuwa yule mama alikuwa hamsikilizi hata.

"Kazi yako ni ipi? Naweza kufanya mpango ukasaidiwa ---- mikopo au leseni au kutolewa pesa ya kusaidia au kupata misangao ya kodi. Naweza kuwavuruga wapinzani wako kwa sheria na kanuni na ukaguzi na ada. Kwa hivyo unaona, hapana namna nyingine ya kuegeza hapa duniani kuliko kwa wanasiasa walio imara. Labda utataka barabara mpya au bustani ijengwe katika ujirani wako au labda jengo kubwa au ............"

"Ngojea!" alisema Jonathan kwa sauti ya juu, akijaribu kuzuia mfuriko wa maneno. "Ni vipi ambavyo unaweza kunipa zaidi ya nitakavyokupa? Je, wewe ni tajiri sana na karimu?"

"Mimi tajiri? Kwa jina la mtume, la!" alijibu vikali Bibiye Tweed. "Mimi si tajiri. Naam, siyo kuwa naweza kukubali. Karimu? Unaweza kusema hivyo, lakini sipangi kulipa na pesa zangu mwenyewe. Naam, waona, mimi ndiye ninayesimamia hazina rasmi. Na, kukuhakikishia, naweza kuwa karimu sana na pesa hizo, kwa watu wafaao ........." Alicheka kipumbavu, akampigia kope mara mbili na kumpiga kikumbo ubavuni tena. "Usiseme zaidi, usiseme zaidi!"

Jonathan hakufahamu kama mama huyu alimaanisha nini. "Lakini unaponunua mchango wangu pamoja na kura, si hiyo ni aina ya naam, ni kama hongo?"

Bibiye Tweed alimpa mwangalio wa busara. "Nitakuwa wa kusema waziwazi mbele yako, rafiki mpendwa." Aliupandisha mkono wake begani pa Jonathan na kisha kumvuta kushoto kwake kwa kumkaza kwa njia iliyomkosesha utulivu aliokuwa nao. "Ni hongo. Lakini ni halali pale ambapo mwanasiasa anatumia pesa kutoka kwa watu wengine na wala si mfukoni mwake. Hivyo hivyo, ni haramu kwa wewe kunipa pesa ili nikufanyie mapendeleo fulani, isipokuwa ukaziita 'mchango wa kampeni.' Hivyo kila kitu ni shwari. Unaweza kununua nakala mia za kitabu juu ya maisha yangu na usisome hata nakala moja. Je, huoni raha kunipa pesa moja kwa moja? Mwombe rafiki au jamaa au mshirika kukupa mikopo ya milele, hiari za hisa, au maslahi utakayonipa mimi au jamaa yangu ------ sasa au baadaye." Alisangaa akitarajia jawabu. "Sasa, waelewa?"

Jonathan alitikisa kichwa chake, "Mpaka sasa sioni tofauti. Nina maana kwamba kuwahonga watu ili kupata kura na mapendeleo ni hongo bado, bila kujali kama wao ni akina nani au pesa husika ni ya nani. Jina halileti tofauti endapo tendo ni lile lile."

Bibiye Tweed alitabasamu taratibu, "Rafiki yangu, rafiki mpenzi, wahitaji kukubali zaidi mambo yalivyo. Jina ni kila kitu." Kwa mkono wazi, alikishika taratibu kidevu chake na kukipindua kichwa chake Jonathan upande. "Jina lako nani? Je, ulijua kuwa unayo sura nzuri? Unaweza kwenda mbali sana kama utaomba kushikilia afisi ya umma. Ikiwa utakuwa mtu wa kukubali mambo, nakuhakikishia nitakupa kazi nzuri katika afisi yangu baada ya mimi kuchaguliwa tena. Ama kuna cho chote unachokihitaji?"

Jonathan alitikisa kichwa chake ili aachiliwe na alifaulu kujiokoa kutoka kwa mikono ya mama yule. "Unafaidi vipi kwa kuwapa wengine pesa za walipa-kodi? Je, waweza kubinafsisha pesa unazozipewa kama mchango?"

"O, baadhi ya pesa hizi zaweza kutumika kwa matumizi yangu na nimeahidiwa mali endapo nitastaafu kutoka siasani, lakini mara nyingi pesa hizi zaninunulia utambuzi au usadikifu au umaarufu au upendo au ustahifu au nafasi katika historia. Yote hii na hata zaidi ni kwangu na kizazi changu!" Bibiye Tweed alicheka polepole. "Kura ni mamlaka na hakuna ninachokifurahia zaidi kuliko kuwa na ushawishi juu ya maisha, uhuru, na mali ya kila mtu kwenye kisiwa hiki. Fikiria ni watu wangapi wajapo kwangu-mimi-ili niwafanyie mapendeleo makubwa na ya milele! Kila kodi na taratibu hunipa mimi fursa ya kutoa makatazo spesheli. Kila tatizo, kubwa au dogo, hunipa mimi ushawishi zaidi. Natoa mankuli ya mchana pamoja na usafiri wa bure kwa ye yote nichaguaye. Toka nikiwa kijana mdogo niliota niwe mtu muhimu kiasi hiki. Wewe, pia, waweza kushirikishwa katika utukufu huu!"
Jonathan alijaribu kuutoa mkono wake. Lakini Bibiye Tweed alimshikilia ndi ndi ndi. "Naam", alisema Jonathan, "wewe na rafiki zako mna shughuli nzuri, lakini watu wengine hawakasirishwi mnapotumia pesa zao kununulia kura, mapendeleo, na mamlaka?"

"Bila shaka", alisema kwa madaha huku akiwa yuainua taya zake zilizojigawa vipande viwili sawa vya videvu. "Na huwa nasikiza wanayoyataka. Kwa hivyo nimekuwa ni mpiganiaji wa mageuzi." Huku akiuachilia mkono wa Jonathan hatimaye, Bibiye Tweed aliirusha hewani ngumi yake kubwa iliyopambwa kwa vito. "Kwa muda wa miaka mingi nimeandika sheria mpya zilizonuiwa kutenganisha siasa na pesa. Nimesema tena na tena kuwa pesa za kampeni husababisha hatari kubwa. Na nimefaulu kupata kura kiasi kwa kuahidi mageuzi." Alipumzika ili kucheka kisha akaendelea, "Kwa bahati nzuri kwangu, nafahamu jinsi ya kuzikabili sheria zangu pale ninapokuwa na vitu vya thamani nitavyowapa watu kwa mapendeleo." Alimpigia kope na kumpiga kikumbo tena, "Unajua ninacho maanisha, unajua ninacho maanisha?"

Bibiye Tweed alimwangalia Jonathan kihakiki, akizingatia jinsi alivyoonekana mwenye mararuraru. "Hapana anayekulipa peni ili umpendelee kwa sababu wewe, sasa hivi, huna mapendeleo unayoweza kuuza. Huoni? Lakini, kwa jinsi ulivyo mtu usiyeonyesha hatia ---- na kwa kuungwa mkono vema nami, waweza kufanya mengi. Naam, jozi mpya ya nguo, viatu vilivyoinuka, mtindo mwema wa kunyolewa, na mchumba wa kike mzuri. Ndio, naweza kwa hakika kupata mara tatu zaidi kura za wapigao kura kwa mara ya kwanza kupitia kwako. Halafu, baada ya miaka kumi au ishirini ya uongozi mwema ----- haidhuru, hapana kikomo kwa mawezekano! "Njoo unione pale Ikulu ya Watawala na nitaona la kufanya." Bibiye Tweed aliliona kundi la wafanyakazi lililokuwa limejikusanya upande wa pili wa barabara, likiangalia kinyonge kile kiwanda kilichofungwa. Mara moja akapoteza ilhamu kwa Jonathan na kuondoka kwa kutembea haraka, akiwa yuatafuta mawindo mapya.

"Kuzitumia pesa za watu wengine kwaonekana kama uchokozi", Jonathan aliyamumunya maneno yake.

Huku akiwa na masikio yaliyokuwa tayari kusikia kutoridhika ko kote, Bibiye Tweed alisangaa na kupinduka kwa kasi, "Je, ulisema uchokozi? Ha! Ni kama kumpokonya mtoto mchanga halua. Endapo watu hawanifanyii kazi ili kuzalisha nikitakacho, mimi huazima kutoka kwao. Unaona, nitakuwa tayari nimejiendea zangu na kukumbukwa sana pale ambapo watoto wao ambao hawakuzaliwa bado wataambiwa walipie. Kijana, unaitwa nami?"

"Ah, Jonathan Gullible, ma'ama." Bibiye Tweed alibadili sura ikaonekana mbaya. "Nitakukumbuka, Jonathan Gullible. Pale ambapo huniungi mkono, inamaanisha unanipinga. Mimi huwazawadisha marafiki na kuadhibu maadui. Huwezi kuwa katikati, au vipi? Hivyo ndivyo ilivyo, ndiyo hali ngumu inayokumba jumuia yetu nzuri. Usiseme zaidi!" Kisha uso wake uliirudia hali yake ya kawaida ya tabasamu kubwa iliyo ng'ara. Halafu akatokomea barabarani upande wa chini.








© Copyright 2005,
Inter Region Economic Network, Nairobi, Kenya, All Rights Reserved.