Inter Region Economic Network, Nairobi, Kenya  

Home
About IREN
Media & Press
Projects
News & Newsletters
Articles
Events
Resources
Speeches and Publications
Student Outreach
Contact IREN

Chapter 12 - SURA YA KUMI NA MBILI



FUJO KWENYE MAKAZI

Barabara zilizidi kuwa tulivu kadiri Jonathan alivyoenda taratibu chini kupitia msururu mwingine wa nyumba zisizo na rangi nzuri. Alitambua kuwa kulikuwa na kundi la watu waliojivalia vivi hivi wakiwa wamejikusanya mbele ya majengo matatu marefu yaliyoitwa JENGO A, JENGO B, na JENGO C. JENGO A halikuwa na watu na katika hali ya kutisha ---- uashi wasambaratika, madirisha yamevunjika, na bambaza za vioo zilizobaki zilikuwa na uchafu wa masizi. Katika ujirani kwenye JENGO B, watu walisongamana kwenye vipandio vya mbele. Jonathan alizisikia sauti za juu zikitoka mule ndani zikiandamana na sauti za shughuli zilizopelekwa mbio mbio kwenye orofa zote tatu. Nguo zilizofuliwa zilitundikwa ovyo ovyo kwenye vijiti vilivyotokeza kutoka kote kuliko kuwa na dirisha na roshani. Ilifurika kwa wapangaji.

Upande wa pili wa barabara kulikuwa na JENGO C likiwa limetunzwa pasipo doa na kama vile JENGO A, halikuwa na watu. Madirisha yake yaliyosuguliwa na kusafishwa sana yaling'ara juani; kuta zake zilizopakwa chokaa zilikuwa laini na safi.

Huku akiwa ameyakodolea macho majengo haya matatu, Jonathan alisikia mguso hafifu kwenye bega lake. Kugeuka, alimwona msichana mdogo mwenye nywele ndefu za rangi ya hudhurungi ya mchanga. Nguo zake za kijivu hafifu hazikumkaa kisawasawa na hakuonekana mrembo alipoangaliwa kwa mara ya kwanza, lakini kwa Jonathan alionekana chapuchapu na mkarimu.

"Je, unafahamu chumba cho chote cha kukodesha?" aliuliza kwa sauti laini na ya kupendeza. "Nasikitika", alisema Jonathan. "Mimi sitoki janibu hizi. Lakini mbona usiyaangalie yale majengo mawili yasiyo na watu?"

"Hamna haja", alijibu kwa unyenyekevu.

"Lakini", alisema Jonathan, "yananionekania yaliyo tupu."

"Ndivyo yalivyo. Familia yangu ilikiishi pale JENGO A kabla ya kubanwa kwa kodi ya nyumba."

"Mbano wa kodi ya nyumba ni nini?" aliuliza Jonathan.

"Ni sheria inayowazuia wenye nyumba kupandisha kodi za nyumba."

"Mbona?" alisaili Jonathan.

"Ah, ni hadithi ya kipumbavu", alisema. "Wakati ambapo Mashine ya Ndotoni ilikuja katika ujirani wetu, babangu na wapangishaji wengine walilalamika dhidi ya wenye nyumba kupandisha kodi. Ndio, gharama zilikuwa juu na watu wengi zaidi walikuwa wakikodisha nyumba, lakini babangu akasema kuwa hiyo haikuwa sababu ya sisi kulipa zaidi. Kwa hivyo wapangaji ----- au wale waliokuwa wapangaji, niwaite hivyo ------ walilitaka Baraza la Watawala kupinga kuongezwa kwa kodi za nyumba. Hivyo ndivyo Baraza lilivyofanya na kisha kuajiri kwa wingi watawala, wakaguzi, mahakimu, na walinzi ili kuhakikisha kutekelezwa kwa hizo sheria mpya."

"Je, wapangaji walifurahia hili?"

"Mara ya kwanza, ndio. Babangu alijihisi alikuwa na uyakini kuhusu gharama ya kile kisusi kilichotufunika. Lakini wenye nyumba waliacha kujenga nyumba mpya na kuacha kuzikarabati zile za zamani."

"Kulifanyika nini?"

"Gharama ziliendelea kupanda ------ wafanya ukarabati, walinda usalama, wasimamizi, matumizi, ushuru, na kadhalika ----- lakini wenye nyumba wasingethubutu kuongeza kodi kulipia huduma hizi zote. Kwa hivyo waliwaza, 'kuna haja gani kujenga na kukarabati ambapo pesa zinapotea?'"

"Je, ushuru pia ulipanda?" Jonathan aliuliza.

"Naam, ili kuweza kulipia huduma za kubanwa kwa kodi za nyumba. Makadirio na wafanyakazi ni vitu vilivyotuna", alisema yule msichana. "Baraza lilipitisha ubanaji wa kodi ya nyumba, na wala si kubana ushuru. Naam, matengenezo pamoja na utunzaji uliposimamishwa, kila mtu alianza kuwachukia wenye nyumba."

"Je, hawakuchukiwa hapo mbeleni?"

"La, kabla ya kubanwa kwa malipo ya nyumba, tulikuwa na nyumba nyingi sana ambazo tungeweza kuchagua. Iliwapasa wenye nyumba wawe ni watu wazuri ili kuwavutia wapangaji. Wengi katika wenye nyumba walikuwa ni watu wazuri na walifanya mambo yawe ya kuvutia. Pale palipotokea mwenye nyumba mbaya, watu waliweza kufahamishwa haraka na watu walikosa kushirikiana naye kwa ubaya wake. Wenye nyumba wazuri walikuwa na wapangaji waliodumu hali wale wabaya walikuwa na nyumba nyinyi zisizokuwa na watu."

"Ni nini kilichobadilika?"

"Baada ya kubanwa kwa kodi ya nyumba kila mtu alibadilika na kuwa mwenye nia mbaya", alisema kwa mwangalio ulioashiria ukataji tamaa. "Ni watu waovu waliofanikiwa zaidi." Aliketi chini kwenye jiwe kando ya njia ili kumkuna yule paka kwa jina Mices nyuma ya masikio yake. Mices alipingirika na kuanza kukoroma.

Akitambua kuwa Jonathan amemkodolea macho, aliendelea kusimulia kishupavu, "Gharama zilipanda, lakini si kodi za nyumba. Hata wale wenye nyumba wazuri zaidi walibana gharama za utunzi wa nyumba. Nyumba ziliishia kuwa zisizoishika au hatari kwa usalama wa wapangaji, na ndipo wapangaji walipokasirishwa na kulalamikia wakaguzi. Wakaguzi wakawapiga faini wenye nyumba. Baadhi ya wenye nyumba waliwahonga wakaguzi ili waende kwingine. Hatimaye, mwenye JENGO A, mume mtahifu, hangeweza kustahimili hasara au kuhonga tena na kwa hivyo alichoka na kujiondokea."

"Aliacha nyumba yake mwenyewe?" Jonathan alitokwa na swali hili kimbubujiko.

"Ndio. Hutokea sana", alisema kwa kuhema. "Fikiria kukiacha kitu kilichokugharimu sana kukijenga! Naam, nyumba zilizidi kuwa chache kadiri uchao lakini idadi ya wapangaji ilizidi kukua. Watu walilazimika kusongamana katika zile zilizokuwa zimesalia. Hata wenye nyumba wabovu, kama mwenye JENGO B, hawakuwa na nyumba tupu tena. Vumi zinasema kuwa huyu bwana huchukua hongo kutoka kwa watu wanaotaka nyumba ili kuvukisha majina yao kwenye orodha ndefu ya wanaosubiri. Wale walio na pesa za kutosha hufaulu. Huyu mwenye nyumba sugu hufanya mambo kama mnyang'anyi."

"Na je, JENGO B nalo?" alisema Jonathan, akifikiri kuwa atakuja kumfaa yule. "Unaweza kuingia jengo hilo?"

"Orodha ya wale wanaosubiri ni ya kustaajabisha. Wakati Dame Whitmore alipofariki dunia kulikuwa na ugomvi na ghasia ----- kila mtu alishindana na kupigia mwenzake makelele akitaka nafasi hiyo. Mwana wa kiume wa Bibiye Tweed ndiye aliyekipata chumba hicho hatimaye ----- ingawa hakuna akumbukaye kumwona katika wale waliojitokeza siku ile. Kunao wakati ambapo familia yangu ilijaribu kuishi kikoa katika nyumba fulani kwenye JENGO B, lakini kanuni za ujenzi haziruhusu kuishi hivyo."

"Je, kanuni za ujenzi ni nini?" aliuliza Jonathan.

Msichana yule alikunjamana uso. "Ilianza kama masharti kadhaa ya usalama. Lakini kwa sasa Watawala huitumia ili kuweka na kutathmini viwango vya maisha. Unajua, vitu kama vile idadi inayostahili ya sinki, majiko, na vyoo; idadi stahilifu ya watu na aina za watu; nafasi stahilifu." Kwa tashtiti hivi aliongeza, "Kwa hiyo tulibakia kuwa ni watu wa barabarani ambapo hapana kanuni ----- hakuna sinki, majiko, au vyoo, hakuna ufaragha, na nafasi ni kubwa sana."

Jonathan alihuzunishwa alipoyafikiria maafa ya mama huyu. Kisha akakumbuka jengo la tatu ----- jipya sana hali bila wapangaji. Bila shaka jengo hili lingekuwa tatuzi kwa matatizo yake. "Mbona usipangishe nyumba pale penye JENGO C, upande ule wa pili wa barabara?"

Alicheka kicheko chenye uchungu. "Hiyo itakuwa ni kuvunja kaida za sheria zinazowatenga watu katika sehemu mbalimbali."

"Sheria za kuwatenga watu katika sehemu mbalimbali?" Jonathan alikariri. Huku akijiegemeza kwenye jiwe alilolikalia pale penye barabara - kando ya miguu, Jonathan alikitikisa kichwa chake kwa kutoyaamini yale.

"Hizo ni sheria kuhusu sehemu. Uwekaji sehemu hufanya kazi vifuatavyo", alisema haya huku akikichukua kijiti ili achore ramani ndogo mchangani. "Baraza hutenga sehemu mbalimbali za mji. Watu wanaruhusiwa kulala upande mmoja wa kitengo usiku, lakini lazima wafanya kazi ule upande wa pili wakati wa mchana. JENGO B lapatikana upande wa kulala nalo JENGO C lipo upande wa kufanya kazi. Ni kaida kwa majengo ya kazi kuwa ng'ambo ile ya mji kinyume na yale ya kulala na hali hii humlazimisha kila mtu kwenda mwendo mrefu kila subuhi na jioni. Wanasema kuwa miendo mirefu ni mizuri kwa ajili ya mazoezi na mauzo ya magari."

Jonathan alikodoa macho kwa mshangao. Alishangaa kuona nyumba ya kupanga iliyofurika kwa watu ikiwa imekitwa katikati ya nyumba mbili tupu na barabara iliyojaa wasikwao. Kwa huruma aliuliza, "Sasa utafanya nini?"

"Tunaikabili siku moja moja jinsi inavyotujia. Babangu anataka niandamane naye hadi kwenye tamasha za 'Thumbs Up Party' ambazo Bibiye Tweed amewaandalia watu wasio na makao hapo kesho. Ameahidi kutupa matumaini maishani kwa kutuandalia michezo na mankuli ya mchana yaliyo bure."

"Ukarimu ulioje huo", alisema Jonathan taratibu, akikumbuka mazungumzo yake na Bibiye Tweed. "Labda atakuacheni mwishi nyumbani kwake mpaka mpate mahali penu."

Babangu alipata ujasiri wa kumwuliza hilo wakati mmoja, hasa ikizingatiwa kuwa Tweed ndiye anayeongoza Baraza katika kutekeleza kubanwa kwa kodi za nyumba. Bibiye Tweed alimwambia, 'Lakini hilo litakuwa ni tendo la kuonyesha huruma!' Alimwelezea babangu kuwa ni tendo la taadhima zaidi kuomba walipa - ushuru watupe nyumba. Alimwambia awe mvumilivu na kuwa angefanya mipango na Baraza."

Yule mama mwenye umri mdogo alimwangalia Jonathan kwa tabasamu na kisha kumwuliza, "Naomba kukufahamisha kuwa jina langu ni Alisa. Je, waweza kujiunga nasi kwa mankuli ya mchana yaliyo ya bure kwa Tweed kesho alasiri?"
Jonathan alifadhaika aijue la kusema. Labda ataichukua fursa hii kujifunza kukifurahia kisiwa hiki. "Naam, nitafurahi kuandamana nanyi. Na, mimi ni Jonathan."
Alisa alichachawa, huku akiwa yuatabasamu. "Hivyo basi, Jonathan, tukutane hapa kesho wakati kama wa leo. Njoo na paka wako."





© Copyright 2005,
Inter Region Economic Network, Nairobi, Kenya, All Rights Reserved.