Chapter 13 - SURA YA KUMI NA TATU
UHALIFU UNAOONGEZEKA
Akiwa amefurahi kupata rafiki mpya, Jonathan aliondoka huku kapumbazika. Mara, alitanabahi kuwa ilimbidi kuzingatia sana ujirani wake la sivyo asingeweza kurudi kesho yake.
Alimkuta polisi, ambaye hakuwa na umri mkubwa sana kuliko wake, akisoma gazeti na akiwa ameketi kwenye ubao wa kukalia. Jonathan alizikazia macho sare nyeusi zilizojikaukia pamoja na bunduki iliyokuwa iking'ara. Lakini ule ujana, uwazi kwenye uso wa yule polisi ulimpa Jonathan kutulizana. Yule polisi alikuwa kajishughulisha sana na gazeti na ndipo Jonathan alipotupia jicho mada-kuu: WATAWALA WAIDHINISHA ADHABU YA KIFO KWA VINYOZI WATORO.
"Adhabu ya kifo kwa vinyozi?" alistaajabu Jonathan. Yule polisi alimtazama Jonathan. "Naomba samahani", alisema Jonathan. "Siyo nia yangu kukubugudhi, lakini mada kuu ya gazeti hili imenivutia. Je, adhabu hii ni maendelezo mabaya au vipi?"
"Ngojea, tuone." Afisa yule alisoma kwa sauti ya juu, 'Baraza la Watawala limeidhinisha sasa adhabu ya kifo kwa ye yote atakayepatikana akinyoa nywele bila kibali.' Naam, si maendelezo mabaya. Ni kipi ambacho sicho kwa hilo?"
"Hiyo si adhabu kali sana kwa kosa dogo kama hilo?" aliuliza Jonathan kwa tahadhari.
"Siyo", alijibu yule polisi. "Adhabu ya kifo ndilo tishio la mwisho kabisa la sheria zote ----- bila kujali udogo wa kosa."
Jonathan alikodoa macho. "Kwa kweli hamwezi kuua mtu eti kwa sababu amenyoa bila leseni!"
"Bila shaka tunaweza", alisema yule polisi huku akipapasapapasa bunduki yake kama njia ya kutilia ging'izo maneno yake. "Hata hivyo ni nadra sana kupata hilo limetendeka."
"Kwa nini?"
"Naam, kila hatia huongezeka kwa uzito. Hii ina maana kuwa adhabu huongezeka kadiri mtu anapopinga. Kwa mfano, ikiwa mtu atataka kunyoa nywele bila leseni, faini itamtozwa. Ikiwa atakataa kulipa faini, au kuendelea kunyoa nywele, hapa kinyozi mtoro yule atakamatwa na kuzuiwa." "Halafu", yule mume akasema kwa toni iliyoonyesha utulivu, "kukataa kushikwa humpelekea mhalifu kupata adhabu nzito." Uso wake ulionyesha magunyugu. "Mtoro aweza hata kupigwa risasi. Ukinzani unapokuwa mkubwa, nguvu nyingi pia zamtumikiwa."
Majadiliano haya ya kikatili yalimsikitisha Jonathan. "Vile tishio la mwisho kwa kila sheria hasa ni kifo? Ama kwa kweli mamlaka yafaa kuwekea adhabu ya kifo matendo maovu zaidi ya kikatili na kihalifu ----- vitendo vya maguvu kama uuaji na ubakaji!"
"Hapana", yule afisa polisi alisema. "Sheria hutawala maisha yote ya kibinadamu na kibiashara. Mamia ya vyama vya kazi hulinda wanachama wake kwa leseni kama hizi. Seremala, madaktari, mafundi wa mabomba ya kuleta maji nyumbani, mahasibu, wafiatua - matofali, na wanasheria -- wo wote wale, wote wachukia wadukizi.
"Je, leseni huwalinda vipi?" aliuliza Jonathan.
"Idadi ya leseni hubanwa na kupewa wachache wanaofaulu mtihani wa wanachama wa chama. Hali hii hudondosha ile hali ya upinzani usio wa haki kutoka kwa wadukizi walio na mawazo mapya ya kipekee, shauku kubwa, ustadi uliokithiri, au bei za kikatili. Ushindani usionyooka kama huu si ushindani na huhatarisha kaida za taaluma zetu zinazoheshimika."
Mpaka wakati huu Jonathan asingeweza kuelewa. "Je, utoaji wa leseni huwalinda wateja?"
"Naam. Hivyo ndivyo inavyosemwa hapa hivi." Yule polisi aliregelea kulisoma gazeti, "Leseni huwapa wanachama katika biashara fulani ukiritimba ili nao waweze kuwalinda wateja kutokujiingiza katika maamuzi yasiyofaa na pia teuzi nyingi za bidhaa." Huku akijipigapiga fua lake kwa maringo, yule polisi aliongeza kusema, "Nami huhakikisha kuwa ukiritimba umedumishwa."
"Ukiritimba ni mzuri?" aliuliza Jonathan.
Yule polisi alikasirika, akatelemsha gazeti kutoka pale usoni pake. "Sijui, kwa hakika. Mimi hufuata amri tu. Kunao wakati ambapo mimi huhakikisha kuwa ukiritimba umedumishwa na pia wakati ambapo huvunja ukiritimba."
"Kwa hivyo ni hali gani nzuri?"
Yule polisi alisita. "Hilo si jukumu langu mimi. Baraza la Watawala huamua na kuniambia mimi kama nielekeze bunduki yangu upande upi."
Kwa kuona uso wa Jonathan ukiwa na hofu, yule polisi alijaribu kumtia moyo. "Usifanye wasiwasi. Ni nadra sana kwetu kumhukumu mtu adhabu ya kifo. Ni watu wachache wanaothubutu kuwa na upingamizi kwa kuwa sisi ni mafundi katika ufundishaji wa utiifu kwa niaba ya Baraza. Adhabu ya kifo hutajwa kwa nadra sana kiasi kwamba mkubwa wangu, Afisa Stuart, anaiita Bunduki lisiloonekana.''
"Je, umewahi kuitumia yako?" Jonathan aliuliza, huku akiwa yuaiona bastola ya kioga.
"Dhidi ya mtoro?" aliuliza yule polisi. Akifanya kana kwamba ni mazoezi, aliibandua vema ile bastola kutoka kwenye mfuko
wake wa ngozi na kisha akashika kwa mshindo mtutu baridi wa chuma. "Mara moja pekee." Alifungua chemba, akauangalia mtutu, akalalisha kufunga, na kisha akaitamani bunduki ile. "Hii ni moja katika teknolojia nzuri zaidi kisiwani hapa. Baraza hufanya juu chini ili kutupa zana safi zaidi kwa jukumu letu muhimu. Naam, mimi na bunduki hii tuliapa kulinda maisha, uhuru, na mali ya kila mtu kisiwani hapa."
"Uliitumia lini?" aliuliza Jonathan.
"Inashangaza kuwa wauliza", alisema, lakini kwa huzuni wa ghafula. "Nimekuwa kazini kwa muda wa mwaka mmoja bila kuitumia mpaka asubuhi hii ya leo. Mama kizee fulani alipatwa na wazimu na akaanza kutisha kwa kijiti kundi la wabomoaji. Alikuwa akitaja kitu kama kuinyakua tena nyumba 'yake'. Ha! Ni ujinga ulioje huo."
Moyo wake Jonathan ulikosea pigo moja. Aliikumbuka nyumba nyeupe nzuri na yule mwanamke mwenye heshima aliyedai kuimiliki. Yule polisi aliendelea, "Nilijaribu kumshawishi aachane nayo. Stakabadhi zilikuwa sawa ---- nyumba ile ilikuwa imepimwa na kusemekana kuwa haifai na kwa hivyo ilifaa kubomolewa ili mahali pake pajengwe Bustani ya Watu ya Bibiye Tweed."
Jonathan asingeweza kusema zaidi. "Ni nini kilichotokea?"
"Nilijaribu kumshawishi kwa kumpa sababu. Nilimweleza kuwa labda angepata adhabu hafifu kidogo kama angenisikiliza. Lakini akanitisha, akaniambia niachane na mali yake! Naam, hii ilikuwa ni kesi dhahiri ya mtu aliyekataa kushikwa. Fikiria ujasiri wa mwanamke huyo!"
"Naam", alihema Jonathan. "Ujasiri upi?"
Mawasiliano yalikoma. Yule polisi alisoma kimoyomoyo huku Jonathan naye akiwa kasimama kimya, akidukuadukua jiwe kwa mguu wake. Akijitia ujasiri, Jonathan aliuliza, "Je, mtu ye yote aweza kununua bunduki kama hii yako?"
Huku akiwa yuapindua ukurasa wa gazeti, yule polisi alijibu, "Haiwezekani hata ukajaribu vipi. Huenda mtu akaumizwa."
© Copyright 2005,
Inter Region Economic Network, Nairobi, Kenya, All Rights Reserved.