Chapter 15 - SURA YA KUMI NA TANO
HAMNA KITU
Jengo lenye sura ya kuvutia wa mawe, la MAKSERI, lilisimama kwa urefu wa ghorofa mbili. Umati uliovalia nadhifu ulikusanyika langoni, ukingojea kuingia. Walijitia kutong'amua ule ubishi uliokithiri nyuma yao katika lile eneo wazi. Jonathan alipokuwa akijiunga na hilo kundi, alisoma kwa shauku herufi nzito za shaba nyeusi zilizokuwa juu ya sehemu ya mlangoni. "MAKTABA YA WATU YA BIBIYE BESS TWEED"
Wageni waliokuwa mbali upande wa nyuma wa ule umati walijinyosha ili kuona kilichokuwa kikiendelea mbele. Walimaka kwa sauti kwa kile walichokiona. "Ajabu:", baadhi yao walinong'ona. "Inavutia sana", wengine wakasema. Licha ya kujaribu sana, Jonathan hakuweza kuona walichokuwa wakikimakinikia.
Kwa ustadi na wembamba, Jonathan alijichoma kwenye ule umati na kuelekea kunako meza ya muktubi ndani ya lango. "Ni nini huu umati unachokiona kuwa cha kustaajabisha na kuvutia?" alimuuliza mwanamume aliyekuwa amekaa nyuma ya ile meza.
"Shhh!" akaonya vikali muktubi. "Tafadhali shusha sauti yako." Huyo mwanamume akagonga kidogo pembe za kitopa cha kadi na kuzitia chini vizuri mbele yake. Akasimama mbele na kumtizama Jonathan kupitia miwani yake yenye fremu nusu nusu. "Hawa ni wanachama wa Tume ya sanaa ya Baraza. Wamefungua tu sasa hivi onyesho la kazi mpya kabisa tuliyopata katika ukusanyaji wetu wa sanaa."
"Vizuri sana", alinong'ona Jonathan. Huku akinyosha shingo kutizama haraka, alisema. "Ninapenda sanaa nzuri, lakini ipo wapi? Ninadhani ni ndogo sana." "Hapo inategemea", akasema kwa dharau yule muktubi. "Baadhi waweza kudai ni pana. Huo ndio umbuji wa sehemu hii. Anwani yake ni "Tupu katika mruko."
"Lakini sioni chochote", akasema Jonathan, akikunja uso huku na kuchunguza eneo kubwa jeupe juu ya ile sehemu ya lango.
"Hivyo ndivyo kabisa. Inavutia, sio?" Muktubi alilitazama lile eneo huku uso wake ukionyesha hisia tupu za kinjozi. "Hakuna kitu kinachofumbata ukweli kamili wa juhudi za mwanadamu za kuwania ile hali inayotukuzwa ya kufahamu ambayo mtu huweza kuihisi tu anapolinganua vuguvugu kuu la rangi nyepesi na ufahamu kamili wa uasili wetu wa ndani. Hakuna kitu kinachomruhusu kila mtu kupata tajriba ya mawazo bora zaidi ya kijumuishi."
Kwa kuchanganyikiwa, Jonathan alitikisa kichwa chake na kuuliza kwa mkanganyo, "Kwa hivyo ama kwa kweli si chochote? Kile kisicho chochote chawezaje kuwa sanaa?"
"Hicho ndicho hasa kinacholifanya kuwa wasilisho la ki - usawa zaidi la sanaa. Tume ya Sanaa ya Baraza huandaa mchezo wa bahati nasibu unaotekelezwa vizuri sana ili kufanya uteuzi", akasema Muktubi.
"Mchezo wa bahati nasibu kuteua sanaa?" akasaili Jonathan kwa mshangao. "Mbona mchezo wa bahati nasibu?"
"Katika siku ambazo hapakuwepo maendeleo halmashauri ya sanaa iliyoteuliwa ilifanya uteuzi", akajibu huyo mwanamume. "Kwanza, wakosoaji waliishutumu huyo Halmashauri kwa kuteua zile kazi walizozipendelea kibinafsi na kwa hisia zao wenyewe. Waliondolea mbali sanaa ambayo hawakuipenda kwa vile mwananchi wa kawaida alilipia hiari za Halmashauri kupitia ushuru, watu walipinga huo utabaka bora."
"Na kuhusu kuijaribu Halmashauri mpya?" akapendekeza Jonathan.
"Oh, naam, tulilijaribu hilo mara nyingi lakini wale waliokuwa kwenye Halmashauri hawangeweza kukubaliana na wale waliokuwa nje ya Halmashauri. Kwa hivyo waliishia kufutilia mbali suala lote la Halmashauri - na mahala pake pakachukuliwa na Tume na mchezo mpya wa bahati nasibu. Kila mtu alikubali kuwa mchezo wa bahati nasibu ndio mbinu pekee iliyo ya kihisia bila uhisia. Mtu ye yote angeweza kuingia shindanoni - na karibu kila mtu alifanya hivyo! Baraza la Watawala lililifanya tuzo hilo kuwa karimu iwezekanavyo na kila kidahizo kilifuzu. Tupu katika kuruka imeshinda mchoro asubuhi hii tu."
Jonathan aliingilia, "Lakini mbona watu wasiachiwe sanaa yao wenyewe kila mmoja badala ya kuwatoza ushuru ili kununua uteuzi wa mchezo wa bahati nasibu? Kisha kila mtu angejichukulia anachokipenda."
"Nini!" Muktubi alimaka. "Baadhi ya watu wachoyo hawatanunua cho chote na wengine huenda wakawa na uteuzi mbaya. La, kabisa, Watawala sharti waonyeshe mchango wao kwa sanaa!" Huku akimakinikia "Tupu katika kuruka", muktubi alipishanisha mikono yake na uso wake ukaonyesha hisia zisizoeleweka.
"Uteuzi mzuri, unakubali? Utupu una ubora wa kulipa utulivu lango la maktaba na wakati huo huo kuhifadhi mazingira. Aidha", aliendelea kwa furaha, "hakuna ye yote awezaye kupinga ubora wa kisanaa au mtindo wa kiumbuaji wa hii kazi sadakta. Ni nani ambaye angeweza kuudhika?"
© Copyright 2005,
Inter Region Economic Network, Nairobi, Kenya, All Rights Reserved.