Inter Region Economic Network, Nairobi, Kenya  

Home
About IREN
Media & Press
Projects
News & Newsletters
Articles
Events
Resources
Speeches and Publications
Student Outreach
Contact IREN

Chapter 16 - SURA YA KUMI NA SITA


TAMASHA YA NIA MAALUM

Jua lilikuwa linatua Jonathan aliporejea kwenye vidato vya maktaba. Mji ulipata uhai baada ya magharibi na hili alilipenda; watu huanza kutembea tembea pale kwenye eneo wazi. Watu wengi zaidi walifululiza kuelekea kwenye hema pambe la tamasha lililokitwa karibu MAKSERI.

Huku akiziajabia taa, mitazamo ya watu, na sauti, Jonathan aliranda hadi kwenye hema la ajabu. Ishara ya kuvutia juu yake iliandikwa "TAMASHA YA NIA MAALUM."

Mwanamke mmoja wa kupendeza aliyevalia vazi la rangi nyingi na lenye kumkaza maungo alizuka kutoka kwenye umati na kuwapaazia sauti wote. "Sikizeni! sikizeni! kwa msisimko wa kipekee, ingia moja kwa moja kwenye Tamasha ya Nia Maalum." Ghafula akamwona Jonathan, ambaye alikuwa kakodoa macho kwa mshangao, na kumnyaka mkono. "Kila mtu ni mshindi kijana."

"Inagharimu kiasi gani?" akauliza Jonathan.

"Leta shilingi kumi na uondoke na zawadi kubwa ajabu!" akajibu. Huyo mwanamke akautolea ule umati ishara pana", sikizeni! sikizeni! Tamasha ya Nia Maalum itawafanya matajiri!"

Kwa vile hakuwa na fedha za kutosha, Jonathan alitegea hadi huyo mwanamke akawa ameshughulika na wengine, kisha akatambaa hadi nyuma ya lile hema. Akainua hema kidogo ili kutizama ndani.

Watu waliketi kwenye vibanda kando kando mwa hema. Kati kati, waelekezi waliovalia sare waliwaelekeza washiriki kwenye viti vilivyokuwa vimepangwa kwa duara kubwa. Washiriki kumi walisimama au walipiga magoti nyuma ya viti vyao kwa matarajio. Kisha, nusu ya ile mishumaa ikazimwa, ngoma ikavuma na mrindimo wa chini wa matarumbeta ukasikika. Taa yenye mwanga mwingi ilimwangaza mwanamume mmoja mbeja aliyevalia suti nyeusi ya kumeta meta na chepeo hariri. Akainamia ile duara ya wale kumi.

"Masalkheri", akasema mwanamume huyo, huku akiachilia tabasamu yenye mng'ao wa meno meupe. "Mimi ndiye mkuu wa Duara.! Usiku huu, nyinyi kumi mliobahatika ndinyi mtakaokuwa washindi katika mchezo wetu wa kipekee. Nyote mtashinda. Nyote mtaondoka mkiwa wachangamfu kuliko mlivyoingia. Tafadhali kaeni." Baada ya kusema hayo na kupunga mkono wake uliokuwa na glovu nyeupe haraka, Mkuu wa Duara alikusanya shilingi moja moja kutoka kwa kila mshiriki. Hakuna aliyesita.

Kisha Mkuu wa Duara akatabasamu tena na kutangaza, "Sasa mtaona jinsi mlivyozawadiwa." Na ghafla akaangusha shilingi tano pajani mwa mmoja wa washiriki. Naye huyo aliyebahatika kuzipata akapiga unyende kwa shangwe.

"Hutakuwa mshindi wa pekee", akasema Mkuu wa Duara. Na hivyo ndivyo ilivyokuwa. Alizunguka mara kumi kwenye lile kundi, akikusanya shilingi moja moja kutoka kwa kila mtu.

Baada ya kila duru, akawa anaangusha shilingi tano kwenye paja la mmoja wa washiriki, na kila wakati aliyezipokea huruka kwa furaha.

Baada ya kelele kupusa na washiriki kuanza kufuatana kutoka nje, Jonathan alikimbia hadi mbele ya hema kuona kama kila mtu aliridhika. Mwanamke aliyekuwa langoni alifunua na kushikilia lisani ya hema. Alimsimamisha mmoja wa washiriki aliyekuwa akijivuta kwa magoti na kumuuliza: "Je, umefurahia?"

"Oh, hakika!" huyo mwanamume akajibu huku akitabasamu kwa furaha. "Furah ilioje!"

"Siwezi kusita kuwaelezea rafiki zangu", akasema mwingine. Huenda nikarejea tena baadaye."

Kisha mshiriki mwingine mwenye mhemuko akaongezea, "Naam, oh naam. Kila mtu ameshinda zawadi ya shilingi tano!"

Jonathan, huku akiwaza, alilitazama lile kundi lilipokuwa likifumukana. Yule mwanamke alimgeukia Mkuu wa Duara, ambaye aliupungia umati mkono wa kwaheri na kusema kwa kunong'oneza, "Naam, sisi tuna furaha ya kipekee. Tumeshinda shilingi hamsini ilhali hawa wajinga wote wamefurahia! Ninadhani mwaka ujao tutaliomba Baraza la Watawala kupitisha sheria itakayomtaka kila mtu kushiriki!"

Hapo hapo mwelekezi alinyatia nyuma ya Jonathan na kumkamata ukosi. "Simama hapo, wewe kitundu. Nilikuona ukiangalia kule nyuma. Ulidhani ungepata kutizama bure bila kulipa, eeh?"

"Kumradhi:", akasema Jonathan huku akijitahidi kujikwamua kutoka kwenye mshiko wa mwelekezi. "Sikujua ulihitajika kulipa ili kutizama tu. Yule mwanamama mrembo aliifanya kuonekana ya kusisimua sana - na wala sikuwa na pesa za kutosha, tafadhali."
Mkuu wa Duara aliwakunjia uso Jonathan na mwelekezi, "Hukuwa na pesa?" Lakini yule mwanamke akatabasamu kwa sifa aliyopewa na Jonathan. "Ngoja, usimshike kwa nguvu hivyo", akamwambia mwelekezi. "Huyu ni mtoto tu. Kwa hivyo ulifurahia tamasha?"
"Oh naam, Ma'am!" alisema Jonathan huku akigoteza kichwa kwa nguvu. "Sasa, vipi ungependa kujipatia angaa pesa kwa urahisi? Ama ni hivyo au", sauti yake iligeuka ikawa ya kutisha, "Nitakufanya sungusungu wa tamasha."

"Oh, vizuri sana", alisema Jonathan bila ya kuwa na hakika." Unataka nifanye nini?"

"Ni rahisi", akatabasamu tabasamu tamu tena. "Nenda utembee ukigawa hivi vikaratasi mjini jioni hii na umwambie kila mtu furaha watakayopata katika tamasha yetu. Chukua hii pesa kwa sasa na utapata nyingine kwa kila mshiriki atakayefika mlangoni akiwa na kimojawapo cha hivi vikaratasi. Sasa iendee hiyo shughuli na usinikasirishe."

Huku Jonathan akiutupa mkoba wa vikaratasi mgongoni, yule mwanamke alimtahadharisha, "Jambo lingine. Mwishoni mwa tamasha usiku wa leo, nitatoa ripoti ya ujira wako. Jambo la kwanza asubuhi, ni sharti upeleke nusu ya ujira kwenye ukumbi wa mji kama ushuru wako."

"Ushuru?" akarudia Jonathan. "Mbona?"

"Watawala wanahitaji sehemu ya ujira wako."

Jonathan hakupenda hilo wazo . Akaongezea kwa matumaini." "Usipopeleka taarifa ya ujira wangu, huenda nikafanya kazi kwa bidii zaidi. Labda kwa bidii maradufu."

"Watawala ni werevu kwa hilo, mtoto. Wana makachero kila mahali, wanaotutizama kwa makini. Wakituona tukiuficha ujira wako, paweza kuwepo tatizo kubwa, wanaweza hata kuifunga biashara yetu;" akasema huyo mwanamke. "Kwa hivyo usilalamike. Ni sharti sote tulipie dhambi zetu."

"Dhambi?" akarudia Jonathan.

"Oh, naam. Ushuru huwaadhibu watenda dhambi. Ushuru wa tumbaku huadhibu uvutaji sigara, ushuru wa tembo huadhibu unywaji, ushuru wa faida huadhibu uwekaji akiba, na ushuru wa mapato huadhibu ufanyaji kazi. Bora zaidi kwa Baraza", akacheka mwanamke huyo huku akimkonyezea yule Mkuu wa Duara aliyekuwa kando yake, "ni kuwa na siha, kuwa na busara, utegemezi, na uzembe. Sasa anza kwenda, mtoto!"








© Copyright 2005,
Inter Region Economic Network, Nairobi, Kenya, All Rights Reserved.