Chapter 17 - SURA YA KUMI NA SABA
MJOMBA SAMTA
Kufikia wakati Jonathan aliporejea kwenye hema la tamasha, alikuwa amepata zaidi ya shilingi hamsini. Mwanamke yule alifurahia sana kumpata mtu aliyezingatia kazi ipasavyo na kwa hivyo akamwomba arejee tena usiku ufuatao. Jonathan, baada ya kukubali kurudi ikiwezekana, aliondoka kwenye tamasha ili kutafuta pa kulala usiku huo. Hakujua hasa cha kufanya kwa hivyo aliranda tu ovyo mjini. Aliposita katika mwanga hafifu wa taa ya barabarani, mwanamume mfupi mzee aliyevalia nguo ya kulala alitokea akaelekea kwenye sebule ya mbele ya nyumba iliyokuwa karibu. Alitupa jicho na kutizama kwa makini juu ya paa za safu ya nyumba zilizopakana na ile barabara. Jonathan akauliza kwa utunduizi, "Unaangalia nini?"
"Paa ya ile nyumba", akanong'oneza yule mwanamume huku akiashiria kwenye giza. "Unamwona yule jamaa mnene mwenye kuvalia mavazi ya rangi nyekundu, nyeupe na nili? Mkoba wake wa ngawira unaendelea kuumka kila atokapo nyumba moja hadi nyingine."
Jonathan alitizama kule alikoashiria huyo mwanamume. Umbo fulani lililoonekana kama kivuli lilikuwa limekazana juu ya paa ya mojawapo wa zile nyumba. "Mbona, naam, ninamwona! Mbona usipige kamsa kuwaonya watu wanaoishi humo?"
"Oh, siwezi katu kufanya hivyo", akatetema huyo bwana. Mjomba Samta ana hasira mbaya sana na humwadhibu vikali sana mtu yeyote anayemuudhi."
"Unamfahamu?" akabisha Jonathan. "Lakini....."
"Shhh! usiongee kwa sauti." yule mzee akasema huku akigusisha kidole kwenye midomo yake. "Mjomba Samta huwafanyia ziara ya ziada wale wanaopiga kelele nyingi. Watu wengi hujitia kulala usiku huu wa kuogofya - ingawa haiwezekani kupuuzilia mbali utatizaji wa faragha kama huu."
Huku akijaribu kuzungumza kwa sauti ya chini, Jonathan aliegemea kwenye sikio la huyo mwanamume. "Sielewi. Mbona kila mtu afumba macho wakati anapoibiwa?"
"Watu hubakia kimya usiku huu hasa wa mwezi wa nne", huyo mzee akaeleza. "La sivyo burudani wanayoipata Mkesha wa Krismasi, wakati Mjomba Samta anaponyunyiza vichezo vya watoto na vijipambo kadhaa kwenye kila nyumba , huenda ikaharibika."
"Oh", akasema Jonathan huku akionekana kupumua. "Kwa hivyo Mjomba Samta hurejesha kila kitu tena?"
"Sio rahisi! Lakini watu hufikiria kuwa huwa yuarudisha. Huwa ninajaribu kukaa macho ili nione hasa ni nini anachotwaa na nini anachorejesha. Twaweza kusema ni kama uraibu wangu. Kwa makadirio yangu, wingi wa vitu anavyopata Mjomba Samta hujitwalia yeye mwenyewe pamoja na nyumba chache anazozipendelea hapa mjini. Lakini", akasema mzee huku yuagonga kiganja chake kwenye chuma kwa adha, "Mjomba Samta huhakikisha angaa amempa kila mtu kidogo kidogo ili kuwafurahisha. Hivi humfanya kila mtu kubakia usingizini April ijayo anaporudi tena kuchukua atakacho."
"Sielewi", akasema Jonathan. "Mbona watu wasibakie macho, wamripoti mwizi, na wabakie na vitu vyao? Kisha wajinunulie vijipambo vyovyote vile watakavyo na kumpa ye yote wapendaye."
Mzee aliuchekelea ujinga wa Jonathan kisha akatikisa kichwa. "Mjomba Samta ni mtu anayependwa sana na kutamaniwa na kila mtoto. Wazazi daima wamewafundisha watoto wao kuwa vichezeo na vijipambo vya Mjomba Samta huja kimazingaombwe kutoka angani na bila ya kumgharimu yeyote chochote."
Alipoona jinsi Jonathan alivyosawajika sura, mzee akasema, "yaonekana umekuwa na siku mbaya, kijana."
"Nilikuwa ninatafuta mahali mwa kulala usiku huu", Jonathan akasema kwa zaibaki za uso.
"Basi, unaonekana kama kijana mzuri", akasema mzee, "njoo ukae nasi . Huku kwote ni kwetu mie na Rosa."
Jonathan aliukubali usaidizi wa yule mzee. Alipoingia kwenye ile nyumba alimkuta Rosa, mwanamke mmoja aliyenoneana - mkewe yule mzee. Huku akionekana mchangamfu na mwenye furaha, Rosa alimkaribisha Jonathan kwa kikombe cha kakao na vitumbua vilivyoisha kuokwa sikitambo kirefu kabla. Baada ya kukila tu kikombo cha mwisho, Jonathan alijinyosha kwenye kochi ambalo wenyeji wake walikuwa wameliandaa kwa mablanketi na mto. Mzee aliwasha toza ndefu na akaegemea kwenye mito ya kiti chake.
Maskani ya wenyeji wake Jonathan haikuwa kubwa, ya kitajiri wala mpya. Lakini kwa yule kijana mgeni, ilikuwa kimbilio zuri sana. Moto kidogo uliowaka mahali pake mle, ulikiangaza kile chumba kilichozungukwa na mbao, fremu mbili zilininginia juu ya ubao, moja yenye picha ya familia na nyingine ya ngoe ya familia. Kwenye ile sakafu sahili ya mbao kulikuweko tambara bovu lenye umbo la duara - dufu. Huku akijituliza, Jonathan aliuliza, "Hivi huu utamaduni wa Aprili ulianzaje?"
"Zamani tulikuwa na sikukuu iliyoitwa 'Krismasi.' Ama kwa kweli hii ilikuwa ni siku ya kipekee mwakani. Ilikuwa sikukuu ya kidini iliyowakilishwa kwa upeanaji zawadi na usherehekeaji. Kila mtu aliichangamkia sana na hili likalifanya Baraza la Watawala kuamua kuwa hii ilikuwa ni siku muhimu sana ambayo haingeweza kuachwa ijipitie hivi hivi tu na kusherehekewa kwa fujo fujo. Waliichukua na kuanza kuisimamia ndipo iende sawa sawa." Hapo sauti yake yenye kejeli ilionyesha kutoridhika. "Kwanza kabisa, ishara za kidini zisizofaa ziliondolewa. Watawala wakabadili kirasmi jina la siku kuu hiyo na kuwa 'Eksmasi.' Na yule mtoa - zawadi maarufu aliyetajwa hata kwenye ngano alipewa jina jipya akawa 'Mjomba Samta', huku mkusanya ushuru naye akijivika vazi lake maalumu."
Mzee alisita kidogo akapiga mikupuo kadhaa mirefu na kushindilia tumbaku tozani. Akaendelea tena, "Fomu za ushuru wa Eksmasi sasa ni sharti ziwasilishwe kwa Halmashauri ya Hisani zikiwa nakala tatu tatu kila moja. Halmashauri ya Hisani , kwa kutumia kigezo kilichotiwa na Watawala, huamua ukarimu unaohitajika kutoka kwa kila mlipa - ushuru. Uliouona sasa hivi ndio ukusanyaji ufanywao kila mwaka.
"Hatimaye kuna Halmashauri ya Watundu na Wema. Kwa kusaidiwa na Mhasibu rasmi wa maadili, kila mtu hujaza fomu akielezea kwa tafsli tabia nzuri na mbaya katika huo mwaka wote. Halmashauri ya Watundu na Wema huajiri jeshi la makarani na wapelelezi ili kuchunguza kama kweli wale wanaodai zawadi mwezi wa Desemba wanafaa kupewa.
"Mwisho, Tume ya uteuzi ufaao huamua na kuidhinisha tambo, rangi na mitindo inayokubalika ya uteuzi wa zawadi, na kutoa zabuni zisizoshindaniwa kwa bei kwa watengezaji bidhaa wenye mwegemeo mzuri kisiasa, ambao huwa wameteuliwa mapema kabla. Bila kubagua, kila mtu hupata mapambo yale yale kutoka serikalini, ayatumie kuipamba maskani yake. Katika mkesha wa Eksmasi, wanajeshi huagizwa kuimba nyimbo mwafaka za tamasha.
Kufikia wakati huu, yule mtunduizi mchovu alikuwa ashalala kabisa. Wakati mzee akivuta blanketi begani kwa Jonathan kumfunika, mlio wa paka ulisikika nje ya dirisha. Rosa akanong'ona, "Eksmasi Njema."
© Copyright 2005,
Inter Region Economic Network, Nairobi, Kenya, All Rights Reserved.