Inter Region Economic Network, Nairobi, Kenya  

Home
About IREN
Media & Press
Projects
News & Newsletters
Articles
Events
Resources
Speeches and Publications
Student Outreach
Contact IREN

Chapter 18 - SURA YA KUMI NA NANE



MARUDIO YA SUNGURA NA KOBE

Jonathan alimwota yule mwanamke wa Tamasha za Nia Maalumu. Kila wakati alimpa pesa na kuzinyakua tena. Tena na tena, akimlipa na kumnyang'anya tena. Ghafula, Jonathan aliamka kwa mshtuko, baada ya kukumbuka kuwa alipaswa kupeleka taarifa ya ujira wake kwa maafisa wa ushuru .

Harufu ya kutia hamu, ya mkate uliookwa wakati huo huo ilimjaa puani. Ulikuwa wakati wa staftahi. Mzee yule alisimama karibu na meza akigawa silesi kubwa kubwa za mkate na jemu. Jonathan alimwona kijana mdogo wa kiume mwenye uso uliojaa huzuni akiwa ameketi pale mezani. Mzee alimtambulisha mvulana huyo kama mjukuu wao. Kwa jina Davy, ambaye alikuwa amekuja kukaa nao kwa muda mfupi.

"Ninakukumbuka", akasema Davy kwa uchangamfu. "Babu, huyu alitusaidia mimi na mama tulipokuwa tuondoke shambani." Hilo lilimfanya Jonathan ajihisi amechangamkiwa na kukaribishwa zaidi. Jonathan akiendelea kutakamia silesi yake yenye siagi nyingi, yule mvulana mdogo alikuwa akikiakia, akijaribu kuvuta soksi zake zenye rangi tofauti tofauti. "Bibi, tafadhali nisomee hadi thi tena", akasihi.

"Ipi, kipenzi?" Akabwaga kimanda moto kilichotawanywa kwenye sahani ya Jonathan.

"Ile niipendayo sana, ile ya sungura na kobe. Zile picha zinavutia!" akasema kwa mhemuko Davy.

"Basi, sawa", akasema Rosa huku akichomoa kitabu kutoka kwenye kabati pale jikoni. Akakaa chini kando ya ki - Davy na akaanza "Wakati mmoja ...."

"La, la, Bibi, 'hapo zamani za kale ...'" akakatiza mvulana.

Rosa alicheka. "Nilivyokuwa nikisema ....hapo zamani za kale paliishi kobe aliyeitwa Frank na Sungura aliyeitwa Lysander. Wanyama wote wawili walifanya kazi ya kupeleka barua kwa wote walioishi katika kijiji chao kidogo. Siku moja, Frank, ambaye masikio yake makali yalikuwa na uwezo zaidi kuliko miguu yake mifupi, aliwasikia wanyama kadhaa wakimsifu Lysander kwa kasi yake ya kufikisha barua. Sungura, kwa sababu ya miguu yake miepesi, angewasilisha kwa masaa machache tu barua ambayo wengine wangehitaji siku kadhaa kuiwasilisha. Kwa hasira, Frank alitambaa na kujitoma kwenye yale mazungumzo.

"Sungura", akasema Frank karibu pole pole sawa na desturi yake ya

kutembea, "Baada ya juma moja, ninadhani nitaweza kupata wateja wengi zaidi kuliko uwezavyo. Nitajiundia sifa kwa hilo.

"Hiyo changamoto ilimshangaza Lysander." 'Sifa yako? Ah! Analokufikiriria kila mtu sio lako kudhania', akatoka Sungura kwa fujo. 'Nitapambana nawe, hata hivyo!' Majirani walibeza wakisema kobe na mwendo wake wa kujivuta hangeweza. Ili kuthibitisha, wote walikubaliana kuamua mshindi pahali pale pale baada ya juma moja. Wakati Lysander akikimbia kwenda kujitayarisha, Frank alibakia amekaa kimya na kutulia kwa muda mrefu. Hatimaye aliondoka kwa mwendo wa madaha.

"Lysander alituma arifa sehemu zote za nchi kuwa anapunguza ada hadi chini ya nusu ya ile aliyotoza Frank. Uwasilishaji ungekuwa mara mbili kwa siku kuanzia sasa, hata siku za wikendi na siku kuu. Sungura alipita kila mahali kwenye ujirani akipiga kengele, akigawa barua, akiuza stempu na bidhaa, na hata akipima na kufunga vifurushi papo hapo. Kwa ada ndogo ya ziada, aliahidi kuwasilisha wakati wowote, usiku au mchana. Na daima alitoa tabasamu ya kikweli ya kirafiki isiyolipiwa ada yoyote ya ziada. Kutokana na uhodari, ubunifu na mvuto wake, orodha ya wateja wa Sungura ilipanuka haraka sana."

Daudii alikuwa katekwa kabisa na picha na alimsaidia Bibi kufunua kurasa huku akiendelea kusoma kwa sauti. "Hakuna yeyote aliyewahi kuona dalili za kobe. Kufikia mwishoni mwa juma, akiwa na hakika ya ushindi, Lysander alikimbia kwenda kukutana na waamuzi wa pale ujiranini kwake. Alistaajabu kumkuta kobe tayari yuko pale akimgojea. 'Pole sana, Lysander', alisema kobe kwa kukokota. "Wewe umekuwa ukikimbia kotoka nyumba hadi nyumba ilhali mimi nina hii barua moja tu kuwasilisha." Frank alimpa Lysander stakabadhi na kalamu, huku akiongezea, 'tafadhali tia saini hapa kwenye mstari wa dukuduku.'

"Ni nini hiki?" akauliza Lysander.

"Mfalme wetu ameniteua mimi, kobe, kuwa Afisa Mkuu wa Posta na kanipa idhini ya kuwasilisha barua zote nchini. Pole, sungura, lakini sharti uwache na ukome uwasilishaji wako wote."

'"Lakini hilo haliwezekani!' akasema Lysander, huku akigonga miguu yake chini kwa ghadhabu 'si haki!'

"Hivyo ndivyo mfalme alivyosema, pia", akajibu kobe. 'Si haki baadhi ya watawaliwa wake kuwa na huduma bora za uwasilishaji kuliko wengine. Kwa hivyo amenipa ukiritimba kamili kuhakikisha kuwa kuna ubora sawa wa huduma kwa wote.'

Kwa hasira, Lysander alimchokoza kobe kwa kusema, 'umewezaje kumshawishi akufanyie hivi? Umempa nini?'

"Kobe hawezi kutabasamu kwa urahisi, lakini aliweza kupinda gamba fulani upande mmoja wa mdomo wake. Nimemhakikishia mfalme kuwa ataweza kutuma jumbe zake zote bure. Na, ama kwa kweli, nimemkumbusha kuwa mawasiliano yote ya posta ya watawaliwa yakiwa mikononi mwa utawala itakuwa rahisi kufuatilia tabia za watawaliwa waasi. Ikitokea nipoteze barua moja au nyingine, mh, ni nani atakayelalamika?"
'"Lakini daima umekuwa ukipoteza pesa wakati ukiwasilisha barua!" akadai sungura kwa adha. "Ni nani atayelipia hapo?"

"Mfalme atatia bei kwa kuhakikisha kuwa imo faida yangu. Ikiwa watu wataacha kutuma barua, ushuru utafidia hasara zangu. Baada ya muda mfupi hakuna atakayekumbuka kuwa niliwahi kuwa na mshindani."' Bibi aliinua kichwa akaongezea, "MWISHO."

"Funzo la hadithi hii", akasoma Rosa, "ni kwamba waweza kuwaendea wenye mamlaka kila unapokuwa na matatizo maalumu."

Ki - Daudii kikarudia, "waweza kuwaendea wenye mamlaka kila unapokuwa na matatizo maalumu. Nitakumbuka kufanya hivyo, Bibi."

"Sivyo, sahibu, hivyo ni vile tu kitabu kinavyosema. Afadhali ukajitokeza na funzo lako mwenyewe."

"Bibi?"

"Naam, sahibu?"

"Wanyama wanaweza kuongea?"

"Ndege pekee ndio waongeao, mtoto. Hii ni hadithi tu ya kiajabu, sio ile maarufu ya Bard."

"Nieleze kumhusu Bard, Bibi." Alicheka. "Umekwisha kuisikia mara ngapi tayari? Bard ni tai mwenye hekima anayeranda kwenye bahari saba, kutokea vilele vyenye theluji vya High Yek hadi kwenye fuo zenye mvuke za Roth. La, la, huwezi kunibazazi nikakutambia hadithi nyingine tena. Tuwachie hapo hadi kesho."

Jonathan alimalizia chakula chake na kuwashukuru yule bibi na mumewe kwa ukarimu wao. Walipokuwa wakitoka wote kumuaga Jonathan, yule mzee alimwambia, "Ikiwa utawahi kuhitaji chochote, usiogope, tuchukulie tu kama babu na bibi yako wenyewe."








© Copyright 2005,
Inter Region Economic Network, Nairobi, Kenya, All Rights Reserved.