Inter Region Economic Network, Nairobi, Kenya  

Home
About IREN
Media & Press
Projects
News & Newsletters
Articles
Events
Resources
Speeches and Publications
Student Outreach
Contact IREN

Chapter 19 - SURA YA KUMI NA TISA


KUCHUKA KUYEYUSHA CHAKULA TUMBONI

Kabla ya kuondoka, Jonathan aliomba maelekezi ya kwenda hadi kwenye ukumbi wa mji. Rosa, huku akionekana mwenye wasiwasi, aliweka mkono begani kwa Jonathan, "tafadhali, Jonathan, usimwambie yeyote kuhusu chakula ulichokila huku. Hatuna kibali."

"Nini?" akasema Jonathan. "Mnahitaji kibali kula chakula?"

"Mjini, naam", alijibu. "Na yaweza kuwa shida kubwa kwetu kama mamlaka yakigundua kuwa twala chakula bila kibali."

"Kibali ni cha nini?"

"Ni cha kuhakikisha kiwango fulani cha chakula kwa wote. Miaka iliyopita, watu wa mjini walikuwa wakinunua chakula chao kutoka kwa walanguzi wa barabarani, kutoka mikahawani au wangepata chakula kutoka kwenye maghala na kujipikia majumbani kwao wenyewe. Kisha Baraza la Watawala likadai kuwa ilikuwa si haki kwa watu kadhaa kula vema zaidi kuliko wengine na kwamba watu sharti walindwe dhidi ya uamuzi wao wenyewe usiofaa. Hivyo basi walianzisha mikahawa ya kisiasa ambako kila mtu mjini angekula chakula cha kiwango cha kisawa sawa bure."

"Sio bure kabisa, ama kwa kweli", akasema Babu, huku akitoa kishanta na kukipunga pole pole mbele ya pua ya Jonathan. "Gharama ya kila mlo imepanda zaidi kuliko ilivyowahi kuwa hapo kabla, lakini hapana alipaye mlangoni. Mjomba Samta alilipia kwa ushuru wetu. Kwa sababu vyakula kwenye mikahawa ya kisiasa, au 'Mikasiasa', vilikuwa tayari vimelipiwa, watu wengi walikoma kwenda kwa wenye vyakula wa kibinafsi ambako wangelipa zaidi. Mikahawa ya kibinafsi, kwa sababu ya kuendelea kupungua kwa wateja wake, iliongeza bei ili kufidia gharama. Mingine iliponea chupu chupu kwa sababu ya wateja wachache matajiri au watu waliohitaji chakula maalumu kwa sababu za kidini, ingawa mingi iliishia kufungwa."

"Mbona mtu yeyote yule alipie chakula ilhali kinapatikana bure katika mikasiasa?" Jonathan akashangaa kwa sauti.

Rosa alicheka. "Kwa sababu mikasiasa iliishia kuwa ya kutisha wapishi, chakula chenyewe, mazingira kunakopikiwa, na ..... wapishi wabaya hawafukuzwi kamwe kutoka kwenye mikasiasa. Chama chao kina nguvu sana. Na wapishi wazuri hasa ni nadra kutuzwa maana wapishi wabaya wana wivu. Majengo yenyewe yanajiporomokea - uchafu na takataka ziko kila pahali. Motisha iko chini, chakula nacho hakivutii, na Halmashauri ya myeyusho ndiyo inayoamua watu wale nini na lini."

"Hapo ndipo panapo mushkeli hasa", akadai Babu. "Wanajaribu kuwafurahisha marafiki zao na wala hakuna anayeridhika kamwe. Ungeona vita vya tambi na wali. Tambi na wali siku nenda siku rudi, kwa miongo. Kisha 'washawishia viazi' wakaandaa kampeni yao ya mikate na viazi. Unakumbuka hayo?" alisema akimgotezea mkewe. "Wapenzi wa viazi walipoishia hatimaye kuwaweka watu wao kwenye Halmashauri, ndio uliokuwa mwisho wa kusikia, wacha kuona, tambi na wali."

Daudii alitoa sauti kama ya mtu anayesakamwa na kitu kooni. Huku akiangalilia nyuma ya sketi ya nyanyake, pua ya Daudi ilibetuka kwa adha. "Viazi vinaniudhi, Bibi."

"Afadhali uvile, sahibu, au Maafisa wa Lisho watakupata."

"Maafisa wa Lisho?" akasaili Jonathan.

"Shhh!" akasema Babu huku yuatia kidole kwenye midomo yake. Akatizama nyuma ya bega lake na kisha mbele ya mtaa kuchunguza kama yeyote alikuwa akiwaona. "Wale wanaokwepa chakula kilichoidhinishwa kisiasa huishia kujikuta mikononi mwa Maafisa wa Lisho. Watoto huwaita 'Malish' kwa ufupi. Malish hufuatilia uhudhuriaji wa maakuli na humwinda yeyote asiyehudhuria. Wanaoasi Lisho hupelekwa katika mikahawa maalumu ya vizuizi ili kulazimishwa kula."

Daudii alitetema. "Lakini mbona tusile tu nyumbani. Upishi wa Bibi ndio mwema zaidi!"

"Hairuhusiwi, sahibu", akasema Rosa akimpapasa Daudii kichwani. "Watu wachache wana vibali maalumu, lakini Babu nami hatuna ujuzi mahususi. Na hatuwezi kugharamia vifaa vingi maalumu vya jikoni ambavyo vitafikia matakwa yao. Unaona, Daudi, Watawala wanaamini kwamba wanajali mahitaji yako zaidi kuliko tunavyofanya mimi na Babu."

"Licha ya hivyo", akaongezea Babu, "sote wawili tunahitajika kufanya kazi ili kuvilipia ushuru hivi vyote." Babu akaranda mle sebuleni, kwa kiasi fulani akijizungumzia, akinung'unika, "wanatwambia eti sasa tuna makadirio ya chini ya digester - to - cook kuliko wakati mwingine wowote katika historia, ingawa nusu ya idadiwatu ina ukosefu wa lisho bora. Mpango wa awali wa kuwapa maskini lisho bora umeishia kuwa wa lisho duni kwa wote. Waasi kadhaa wamekataa kula na wanaelekea kuumia vibaya kwa njaa, hata ingawa chakula chao ni cha bure. Kuifanya hali iwe mbaya zaidi, wadokozi na majambazi huranda kwenye mikahawa ya kisiasa na wala hakuna anayejihisi salama huko tena."

"Tafadhali wachia hapo!" Rosa akamwambia mumewe baada ya kuuona mshangao uliojitokeza usoni mwa Jonathan. "Atatishika ghaya ya kutishika atakapokwenda kwenye mkasiasa." Akimgeukia Jonathan, akaonya, "Bora tu uwe na kitambulisho chako tayari unapowasili mlangoni. Hutakuwa na shida."

"Ahsante kwa kunijali, Bibi Rosa", alitamka Jonathan, huku akishangaa kitambulisho ndicho kitu kinachokaaje na jinsi ambavyo angeweza kupata chakula bila kitu hicho. "Ninaweza kujitilia mfukoni silesi kadhaa za ziada kabla ya kuondoka?"

"Usitie shaka, sahibu. Chukua nyingi upendavyo." Bibi akarudi jikoni na kurejea na silesi kadhaa zilizofungwa vizuri kwenye kitambaa. Alitazama kwa makini pande zote kuchunguza kama yeyote miongoni mwa majirani zake alikuwa akimwona, kisha akampa Jonathan zile silesi, akisema, "Zitunze vizuri. Kijana mkwe wangu alikuwa akitupandia chakula cha ziada. Lakini Polisi wa Chakula ....."

"Ninajua", akasema Jonathan. "Nitakuwa chonjo mtu yeyote asikione chakula hiki. Ahsante kwa yote." Huku akipungiwa mikono ya kwaheri, Jonathan aliingia kwenye barabara akiwa mwenye furaha kwa wazo kwamba, ikibidi, alikuwa na maskani kwenye hiki kisiwa kigumu.










© Copyright 2005,
Inter Region Economic Network, Nairobi, Kenya, All Rights Reserved.