Inter Region Economic Network, Nairobi, Kenya  

Home
About IREN
Media & Press
Projects
News & Newsletters
Articles
Events
Resources
Speeches and Publications
Student Outreach
Contact IREN

Chapter 20 - SURA YA ISHIRINI



NIPE SIKU ZAKO ZILIZOPITA AU MUSTAKABALI WAKO

Ukumbi wa mji ulikuwa, kijumla, katika upande wa lile eneo - wazi lenye pembe nne mraba. Jonathan alifikiri angeweza kuchukua njia ya mkato kupitia kichochoro kilichojaa vilima vya masanduku na takataka za namna mbali mbali. Aliharakisha kuelekea upande wa chini wa kichochoro kile huku akijaribu kupuuza hisia za woga zilizomjia baada ya kutoka kwenye ile barabara yenye mwanga na shughuli nyingi.

Ghafula Jonathan alihisi mkono kooni kwake na chuma baridi cha bastola kimefinyiliwa kwenye mbavu zake. "Nipe siku zako zilizopita au mustakabali wako!" akanguruma yule mnyang'anyi kwa ukali.

"Nini?" akasema Jonathan huku yuatetemeka kila mahali. "Unamaanisha nini?"

"Umenielewa -- pesa zako au maisha yako", akarudia mwizi yule, huku akiendelea kuifinyilia bastola ubavuni mwa Jonathan. Jonathan hakuhitaji kuhimizwa zaidi. Alitia mkono kwenye mfuko wake wenye pesa zilizopatikana kwa taabu.

"Hizi ndizo nilizo nazo zote na ninahitaji nusu yake kumlipa mkusanyaji ushuru", akasihi Jonathan, huku akificha kwa makini zile silesi za mkate alizopewa na Bibi Rosa. "Tafadhali niachie nusu."

Mwizi yule alilegeza mshiko wake kwa Jonathan, kwa sauti ya chini lakini kali, akasema, "Kama ni lazima utoe pesa zako, ni afadhali kunipa mimi zote na wala si chochote kwa mkusanya ushuru."

"Mbona?" aliuliza huku akimwekea pesa kwenye mikono yake miepesi na stadi.

"Ukinipa mimi hizo pesa", akasema yule mwanamke mwizi, huku akiendelea kushindilia zile noti kwenye kibogosho cha ngozi alichojifunga kiunoni mwake, "kisha angaa nitaondoka na kuachana nawe. Lakini hadi siku utakapokufa, mkusanya ushuru ataendelea kuchukua pesa zako, zao la siku zako zilizopita, na atazitumia kuamulia kila kitu kinachouhusu mustakabali wako pia. Ah! Atatupilia mbali ujira wako mwingi sana kwa mwaka kuliko kiasi ambacho sisi wanyang'anyihuria sote tutachukua kutoka kwako maishani mwako mwote!"

Jonathan alionekana mwenye kufadhaika. "Lakini kwani Baraza la Watawala haliwafanyii watu mambo mazuri kwa kutumia pesa za ushuru?"

"Oh, naam", alisema kwa ukavu. "Baadhi ya watu huishia kuwa matajiri. Lakini kama kulipa ushuru ni jambo zuri, mbona mkusanya ushuru asikusihi tu kwa kukuelezea uzuri wake kisha akuache ulipe kwa kupenda kwako?"

Jonathan aliwazia suala hilo. "Labda kusihi kwaweza kuchukua muda na nguvu nyingi sana?"
"Sawa", akasema yule mwizi, huku meno yake yakionekana kwenye tabasamu pana. "Hilo ndilo tatizo langu, pia. Sote tunahifadhi muda na nguvu kwa kutumia bunduki!" Alimzungusha Jonathan kwa mkono mmoja na akamfunga mikono kwa kutumia ugwe mwembamba, kisha akamtupa chini kumshindilia kinywani kitambaa chake mwenyewe. "Hivyo. Ninadhani mkusanya ushuru atahitaji kungojea." Aliketi chini kando ya Jonathan, ambaye alifurukuta lakini hangeweza kusonga. "Wajua nini?" akasema mwizi yule huku yuaendelea kuhesabu zile pesa. "Siasa ni aina fulani ya kaida ya kujitakasa. Watu wengi wanafikiri ni vibaya kutamani, kudanganya, kuiba, au kuua. Ni kuasi tu ujirani - isipokuwa tu wakimchukua mwanasiasa kuwafanyia hiyo kazi chafu. Naam, siasa huruhusu kila mtu, hata wale bora zaidi miongoni mwetu, kutamani, kudaganya, kuiba, na hata kuua mara moja moja. Na bado twaweza kuifurahia."

Jonathan aliukunja uso wake na akafanya kelele fulani. Mwizi alicheka, "Kwa hivyo ungependa kupiga yowe, eh?"

Jonathan alitikisa kichwa chake kwa nguvu na akatizama juu kwa macho yenye majonzi. Hili lilimfurahisha mwizi. "Sawa", akasema, "Wacha tukusikie ukilia lia. Lakini isiwe kwa sauti", alionya huku akiigota pua ya Jonathan kwa nguvu kwa ncha ya bastola yake. "Ninaweza kukufanya uhisi vibaya sana." Alichuchumaa kando ya Jonathan na akakitia kile kitambaa chini ya kidevu chake.

Akipanua taya lake kwa maumivu, Jonathan alimbishia, "Lakini si vizuri kuiba!"

"Labda. Jambo muhimu ni kufanya hivyo katika kiwango cha kipekee ambapo hakuna atakaye gundua kuwa ni vibaya."

"Uibe kiasi kikubwa na pasiwepo yeyote anayegundua kuwa ni vibaya?"

"Kweli. Uongo mdogo mdogo ni mbaya. Watoto hufunzwa wasiwe waongo wadogo wadogo. Lakini waongo wakubwa wenyewe wanaishia kuwa na mitaa inayoitwa majina yao. Ukiiba kidogo waweza kuishia kwenye bustani ya wanyama iliyo ya watu lakini ukiiba chungu nzima, yaani nchi nzima, jina lako litaishia kuchongwa kwenye majengo. Na kuua vivyo hivyo."

"Kuua pia?" akahemka Jonathan.

"Kwani umekuwa wapi?" akashtuka yule mwizi. Kuua mtu mmoja au wawili kunakupeleka bustani ya wanyama iliyo ya watu au hata unanyongwa. Lakini kuwaua elfu kadhaa kunakufanya shujaa anayeimbiwa nyimbo, kuchongewa masanamu na kusherehekewa. Watoto hufunzwa kuwahusudu na kuwaiga wauaji wakubwa. Jifanye mdogo na utasutwa na kusahauliwa. Jifanye mkubwa na utaishia kuwa mtu wa tarehe katika vitabu vya shule."

"Hadithi ya awali zaidi ya wizi ninayoikumbuka", akasema Jonathan, "ni ya Robini Hudi. Alikuwa shujaa maana aliwaibia matajiri na kuwapa maskini."

"Alimwibia nani hasa - kimahususi?" Mwizi alisaili.

"Liwali wa Nothingham na rafiki zake", akajibu Jonathan. "Unaona, huyo liwali na John mwana wa mfalme waliwatoza watu ushuru na kuwatia kila mmoja katika umasikini. Kwa hivyo Robin alijaribu kuirudisha ngawira kwa walioathiriwa."

Mwizi alicheka, "Kama ni hivyo basi Robin hakuwa mwizi. Wawezaje kumwibia mwizi?" Alikunja uso na kumakinika kwa muda. "Hilo lanipa wazo fulani", akasema. "Ninadhani nitatembelea Tweed."

Ghafula mwizi alikikaza zaidi kile kitambaa mdomoni kwa Jonathan, kisha akatokomea upande wa chini wa mtaa.

Jonathan alibakia masikini kalala kichochoroni, hana wa kumwauni. Alimkumbuka askari polisi kijana ambaye alikuwa amekutana naye siku iliyotangulia. Huyo jamaa aweza kuwa wapi wakati huu anapomhitaji zaidi. Na huyu jambazi alipataje bunduki?
Wazo la kurudi kule kilabuni ili kujipa zile pesa vipya tena lilimuudhi Jonathan. Alitupa tupa miguu yake bila matumaini kila hilo wazo lilipomjia. Mmoja katika zile nyuzi alizofungiwa ilimchubua ngozi kwenye kiwiko cha mkono naye akajilegeza kidogo kuwazia mashaka yake. Aliwaza, "Sikuwahi kujua jinsi inavyofurahisha mikono yangu ikiwa huru - hadi sasa."








© Copyright 2005,
Inter Region Economic Network, Nairobi, Kenya, All Rights Reserved.