Inter Region Economic Network, Nairobi, Kenya  

Home
About IREN
Media & Press
Projects
News & Newsletters
Articles
Events
Resources
Speeches and Publications
Student Outreach
Contact IREN

Chapter 21 SURA YA ISHIRINI NA MOJA



SOKO LA SERIKALI MBALI MBALI

Jonathan alibakia kanyooka pale huku kaudhika. Mices alitokea tena, akiwa katika shughuli ya kukagua majaa ya takataka mle kichochoroni. Alinusa mkate uliokuwa mfukoni mwa Jonathan lakini ukelele fulani kutoka upande wa mwisho wa kile kichochoro ulimwogofya, akakimbia kwenda kujificha kwenye vilima vya takataka.
Ng'ombe mmoja mwenye rangi ya kahawia alitembea pole pole kuelekea alipokuwa Jonathan. "Moo - o - o", ng'ombe aliroroma. Kengele iliyokuwa shingoni mwake ililia pole pole kila alipopiga hatua. Ghafula ng'ombe mwingine alitokea kule mwisho mwa kichochoro, akifuatiwa na mzee mmoja aliyevalia matambara na huku kabeba fimbo. "Rudi hapa, we hayawani mjinga", akatusi yule mchungaji.

Jonathan alifurukuta na kwa kutumia bega lake akadukua sanduku lililokuwa karibu naye.

Mzee yule alitizama kwa makini kwenye lile giza. "Nani yuko hapo?" Alipomwona Jonathan kafungwa na kudhibitiwa alimkimbilia kumwondolea kile kitambaa alichofungwa kinywani.

Jonathan aliweza kupumua kwa nafuu. "Nimeibiwa. Nifungue!" Mzee alitia mkono mfukoni mwake akatoa kisu na kukata zile kamba. "Ninashukuru", akasema Jonathan, akiendelea kusugua viwiko vyake vya mikono vilivyochubuka. Alimweleza yule mzee, kwa shauku, yaliyomkumba.

"Naam", akasema yule mkulima mwenye matambara, huku yuatikisa kichwa chake. "Lazima uwe chonjo na mtu yeyote siku hizi. Singekuja mjini leo kama si kwa vile nilivyoambiwa kuwa ninaweza kupata usaidizi kutoka serikalini."

"Unadhani serikali inaweza kunisaidia kurudisha pesa zangu?" akasaili Jonathan.

"Sidhani, lakini labda utakuwa na bahati nzuri zaidi kwenye soko la serikali mbali mbali kuniliko", akajibu mchungaji. Uso wake ulikuwa na makunyugu kama ngozi ya kifaru na alivalia nguo shaghala baghala na viatu vikubwa vya ngozi mbichi. Jonathan alianza kupata matumaini tena kutokana na utulivu wa yule mzee na jinsi alivyomsemeza kirafiki.

"Soko la serikali mbali mbali ndicho nini? Ni pahali pa kuuzia ng'ombe?" aliuliza Jonathan.

Mzee alikunja uso na kuwatazama wanyama wake wawili wapole. "Ndicho nilichokuja kuchunguza", akasema. "Ama kweli, ni namna fulani ya maonyesho ya vitu vya aina mbali mbali. Jengo lenyewe ni la fahari kuliko benki na kubwa kuliko kila kitu nilichowahi kukiona. Ndani kuna watu wanaochuuza kila aina ya serikali zinazoweza kushughulikia masuala ya mwananchi."

"Oh?" akasema Jonathan, "Ni aina gani ya serikali wanayojaribu kuuza?"

Mchungaji alijikuna shingo yake iliyounguzwa kwa jua na kusema, "kulikuweko huyu jamaa mmoja mkorofi akijiita 'Msosholisti'. Alinieleza kuwa aina yake ya serikali ingemtwaa ng'ombe mmoja na kumpa jirani yangu. Sikumjali sana. Sihitaji usaidizi wowote kumpa jirani ng'ombe - inapobidi."

"Kisha palikuwepo mwingine 'Mkomunisti' aliyevalia shati ya rangi nyekundu inayoangaza. Alikuwa na kibanda karibu na yule mchuuzi wa kwanza. Alijitia tabasamu kubwa na kila mara akawa ananisalimu mkononi, kirafiki kabisa na kuniambia jinsi alivyonipenda na alivyojali maslahi yangu. Alionekana kuwa mtu mzuri, hadi pale aliposema kuwa serikali yake ingewachukua ng'ombe wangu wote wawili. Alidai ingekuwa vizuri, kwani kila mtu angewamiliki ng'ombe wote kwa kiwango sawa na kwamba ningepata kiasi fulani cha maziwa pale anapoona ninayahitaji. Na kisha akasisitiza eti niimbe wimbo wa chama chake."

"Sharti ni wimbo fulani!" akashangaa Jonathan.

"Alikuwa hanifai chochote huyo baada ya hapo. Ninadhani angeishia kujiengulia mtindi wote. Kisha nilitanga kwenye ule ukumbi mkubwa hadi nilipokutana na 'Muasi' mwenye mavazi meusi kila mahali. Alionekana ni kama yuko njiani kuelekea kwenye maziko." Mzee alisita kwa muda wa kutosha kumwinga mmoja wa ng'ombe wake kutoka kwenye mlima wa taka taka zilizochacha.

"Huyo muasi" vile vile alikuwa na fungu kubwa la maneno matamu na mawazo mengi ya kihodari, kama wale waliotangulia. Alisema angewachukua ng'ombe wangu wote na angeniuzia sehemu ya maziwa. Nikasema 'Eti? nikulipe kutumia maziwa ya ng'ombe wangu mwenyewe?' Kisha alitishia kunipiga risasi papo hapo ikiwa singeikongowea bendera yake."

"Ala!" akasema Jonathan. "Ninadhani uliondoka hapo pahali mbio mbio sana."

"Kabla hata sijautikisa mguu, akaja 'mwana maendeleo' na kunisimulia mpango tofauti. Aliniambia kuwa serikali yake ilinuia kunilipa ili nimpige risasi mmoja wa ng'ombe wangu ili kupunguza mazao. Angemkamua aliyesalia na kumwaga kiasi fulani cha maziwa kwenye mtaro wa majitaka. Aliahidi kunisaidia kununua maziwa yangeliyosalia kwa bei nzuri ya juu. Sasa ni mahepe yupi mjinga angekubali kufanya hivyo?"

"Hufanyi jambo kama hilo linaloathiri maisha yako hivi hivi tu, mwanangu", akadai mzee. "Nani anazihitaji? Badala ya wao kuja kunielekeza cha kufanya, nimeamua kuwapeleka ng'ombe wangu kwenye soko la shamba. Nitamuuza mmojawao nipate fahali.


© Copyright 2005,
Inter Region Economic Network, Nairobi, Kenya, All Rights Reserved.