Chapter 22: SURA YA ISHIRINI NA MBILI
(22) TAALUMA KONGWE KWA ZOTE DUNIANI
Kisa cha yule mlisha mifugo kilimstaajabisha sana Jonathan. Habari za Soko la Serikali Mbali Mbali zilielekea kumchochea, na kwa hivyo akaamua kwenda huko akaone kama kuna yeyote awezaye kumsaidia kurejesha pesa zake.
"Huwezi kupotea", akasema mlisha mifugo huku akijitayarisha kuwaondoa ng'ombe wake. "Liko kwenye ikulu, ndicho kitu kikubwa zaidi kwa vyote katika hilo eneo - wazi. Upite kwenye lango kuu - hilo ni lako - lililo na madirisha mawili makubwa kando kando mwake, moja kulia na moja kushoto. Kwenye dirisha la kulia ndiko watu wapigako foleni kupeleka pesa zao za ushuru. Kwenye dirisha la kushoto ndiko watu wapigako foleni kuondoa pesa zao za ushuru."
"Ninaweza kukisia ni foleni ipi iliyo maarufu zaidi", akatania Jonathan.
"Hapo ni kweli. Kila mwezi foleni moja huendelea kufinyaa ilhali ile nyingine huendelea kufura kidogo kidogo." Mzee alikaza mafundo na akavuta kamba. "Hatimaye, foleni moja ikiisha, ile nyingine pia itaisha."
Ama kwa kweli, barabara zote zilielekea kwenye eneo - wazi la mji. Katika eneo-wazi palisimama jengo la fahari la ikulu. Juu ya lango kubwa palikuwepo maneno yaliyochongwa kwenye jiwe: "IKULU YA WATAWALA." Mices, huku mkia wake umesimama wima, alikuwa amemfuata Jonathan karibu karibu hadi alipofikia vidato vipana kwenye ngazi inayoelekea kwenye lile jengo. Mgongo wa huyo paka ulimwuma kidogo na manyoya yalimsimama. Hapa ndipo mbali kabisa angelipoweza kufika.
Jonathan alivipanda vile vidato mpaka alipofika na kusimama mbele ya lango kuu lenyewe. Ukumbi mkubwa wenye giza giza ulijitanua mbele yake, dari lake likiwa juu sana kiasi kwamba taa zilizokuwemo hazingeweza kumulika eneo lote la ndani yake barabara. Kama tu alivyoelezea yule mchungaji mzee, vibanda kadhaa vilijipanga ndani ya ule ukumbi, vikiwa na mabango na bendera tofauti tofauti. Watu walijitembeza mbele ya hivyo vibanda wakimwita kila mpitaji na kumshawishi kuchukua vikaratasi fulani.
Upande mmoja wa ukumbi huo palikuwepo mlango mkubwa wa shaba nyeusi, ukiwa na sanamu za mawe ya marmar na nakshi za mifuo kila upande. Jonathan alianza kutembea ndani ya ukumbi ule, akinuia kuwakwepa wachuuza serikali. Hata kabla ya kwenda hatua mbili, alivamiwa na mwanamke mmoja wa makamo aliyevalia bangili za dhahabu kwenye viwiko vyake na herini kubwa.
"Je, ungependa kujua mustakabali wako, bwana mdogo?" aliuliza huku yuamkurubia.
Jonathan alimtazama kiupembe yule mwanamke mwenye hanjamu aliyevalia shali zenye rangi ya kung'ara na mapambo mazito. Alikagua
mifuko yake haraka, ingawa hakuwa amabakia na chochote ambacho angeweza kupoteza.
Akaendelea kwa ushupavu, "Nina kipawa cha kuona mustakabali. Labda ungependa kutazama kesho yako kidogo ili kutuliza wasiwasi wako kuhusu mustakabali wako?"
"Kweli unaweza kuuona mustakabali?" akauliza Jonathan huku akirudi nyuma iwezekanavyo bila kumuudhi. Alimshuku sana huyu mwanamke shupavu.
"Naam", akajibu huku macho yake yakionyesha kujiamini, "Ninachunguza ishara kisha ninaamua, ninathibitisha, na kutangaza ninaloliona kuwa kweli. Ah, naam, hii yangu ndiyo taaluma kongwe kwa zote ulimwenguni."
"Mpiga ramli?" akasema Jonathan, akiwa ameshangazwa na dai hilo. "Huwa watumia kitufe cha 'jiwe - kioo' au majani - chai au ..."
"Shetani, la!" akafoka yule mwanamke kwa adha. "Nimetokea kuwa changamano zaidi. Siku hizi ninatumia chati na makadirio ya hesabu." Huku akiinama kabisa aliongezea, "Mwanauchumi tayari kukuhudumia."
"Ajabu ilioje. M-ana-uchu-mi", akarudia Jonathan, akibingirisha hilo neno refu ulimini kwake. "Kuniradhi, nimeibiwa tu sasa hivi na hivi sina pesa za kukulipa."
Huyo mwanamke alionekana ameudhika na akageukia kwingineko kutafuta wateja wengine.
"Tafadhali mamaa, waweza kuniambia kitu kimoja", akasihi Jonathan, "hata ingawa sina cha kukulipa?"
"Mh?" akasema yule mwanamke.
"Ni lini hasa watu wakujiapo kwa ushauri?"
Alichunguza kuona kama mtu yeyote angeweza kuwasikia. Kisha akanong'oneza, "Kwa sababu huna pesa za kunilipa, ninaweza kukupa siri ndogo. Wateja huja kila wanapotaka kuondoa wasiwasi kuhusu mustakabali. Haijalishi kama utabiri huo ni wenye mwanga au giza - hasa unapokuwa na giza - huwafanya watu wajihisi vizuri zaidi wanapotegemea makisio ya mtu mwingine."
"Na ni nani hulipia makisio yako?" akasaili Jonathan.
"Baraza la Watawala ndiyo mteja wangu mkuu", akajibu kwa fahari. "Mabasiri hunilipa vizuri, ama kwa kweli, kwa pesa za watu wengine. Kisha hutumia utabiri wangu katika hotuba zao kuhalalisha uchukuaji wa pesa zaidi ili kujiweka tayari kukumbana na huo mustakabali wenye giza. Mambo hutuendea vizuri sana pande zote mbili."
"Huo basi ni wajibu mkubwa sana", akasema Jonathan. "Tabiri zako zimetokea kusadifu ukweli kwa kiasi gani?"
"Waweza kushangaa jinsi ninavyoulizwa hilo swali na watu wachache sana", akacheka mwanauchumi. Akasita na kumtizama Jonathan kwa makini machoni. "Kusema kweli, waweza kupata utabiri bora kupitia urushaji wa sarafu. Kurusha sarafu ni kitu ambacho mtu yeyote aweza kufanya kwa urahisi, lakini hakumsaidii tu mtu yeyote. Hakuwezi kumfanya mtu mwenye wasiwasi awe na furaha, hakuwezi kunitajirisha, na wala hakuwezi kuwapa nguvu Watawala. Kwa hivyo waona, ni muhimu nibuni tabiri nzuri na changamano ili kuwafaa, la sivyo watamtafuta mtu mwingine atakayefanya hivyo."
"Hmm", akawaza Jonathan. "Ndiyo taaluma kongwe kwa zote duniani."
© Copyright 2005,
Inter Region Economic Network, Nairobi, Kenya, All Rights Reserved.