Chapter 24 - SURA YA ISHIRINI NA NNE
KIPIMO SHANGILIO
Kurunzi moja ilitupa duara ya nuru kwenye lile jukwaa na hadhira ikaanza kunong'ona. Mtu mmoja alianza kupiga makofi kwa wizani na papo hapo umati ukajiunga naye. Ukumbi wote ulivuma kwa shangwe. Hatimaye, mtu mmoja mnene mwenye nywele nyepesi na nyeusi kama mpingo, aliruka akaingia jukwaani. Alivalia suti yenye mng'ao wa dhahabu. Usoni pake palionekana tabasamu ambayo ndiyo ya kiafkani kabisa kwa zote alizowahi kuziona Jonathan. Mwanamume huyo alitanga huku na huku kama paka pale jukwaani katika harakati za kuusalimu ule umati uliokuwa na furaha tele.
"Karibuni, karibuni, karibuni! Mimi ni Showman Phil na nina furaha kubwa kuwa nanyi wapendwa, hapa katika onyesho letu, Mpo! Na ni onyesho zuri lililoje leo! Baadaye tutazungumza naye - naam umekisia kweli - mgombeaji mwenyewe!" Wanawake waliovalia mavazi yaliyoacha wingi wa maungo yao wazi, waliokuwa wamesimama pande zote mbili za jukwaa, walianza kupunga mikono yao kwa jazba na umati wote ukalipuka kushangilia.
"Ahsanteni, ahsanteni, ahsanteni sana. Kwanza, nina jambo zuri, zuri sana kwenu. Tunaye si mwingine bali mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Korumpo ambaye yupo hapa kutuelezea taratibu mpya za kimapinduzi za uchaguzi ambazo tumekuwa tukizisikia hapa na pale." Hapo, mwalishi aligeuka na, huku akipisha mkono wake kwa nguvu mbele ya jukwaa, akapaaza sauti, "Sote tumkaribishe Daktari Julia Parlov!"
Wale waliokuwa jukwaani pamoja na umati wote walipiga makofi kwa kishindo tena, huku wakishangilia na kupiga miluzi kwa mhemuko. Showman Phil alimsalimu mkononi Dk Parlor na akatoa ishara kwa hadhira itulie. "Naam, naam. D.K. Parlor, yaonekana kwa hakika umejipatia ufuasi mkubwa kwa miaka kadhaa iliyopita." "Shukurani, Phil", alisema yule mwanamke. D.K. Phil alivalia miwani mizito, suti ngumu ya kijivu, na uso wake wa mraba ulionyesha kuridhika.
"Ninadhani ni shauku ya karibu 5.3."
"Eeh, eeh, hapo umenipata", akasema mwalishi Walinda jukwaa waliifanyia hadhira ishara ya ghafula nayo yote ikaachilia kicheko chepesi cha ghafula. "Unamaanisha nini ukisema 'shauku ya 5.3'?" akasaili Phil.
"Naam", akasema Dk Parlor. "Hapa nina kipima-shangilio rasmi. Daima mimi hubeba kimoja kila niendako. Huwa chanambia hasa ni shauku kiasi gani inayoonyeshwa na halaiki za watu."
"Ajabuu hiyo, au vipi jamaa?" Kufuatia ishara, umati ukashangilia tena kwa uchangamfu.
Punde tu kelele zilipopusa, Dk Parlor akaendelea, "Hapo ni 2.6 hivi."
"Lo!" akasema mwalishi. "Utakuwa ukifanyia nini hiki kipima-shangilio? Je, utakitumia kwenye uchaguzi ujao?"
"Ndivyo, Phil. Sisi katika Tume ya Uchaguzi ya Korumpo tumeonelea kuwa kuhesabu kura hakutoshi. Sio nambari tu pekee zilizo muhimu katika kuamua adili, nguvu, mali na haki. Tunaonelea kuwa shauku ni muhimu vile vile."
"Ajabu hiyo!" akasema kwa sauti ya kupaaza Showman Phil. Kila mtu akashangilia.
"4.3", akasema Dk Parlor kwa utulivu.
"Utawezaje kufanya hivyo, Daktari?"
Nyusi zake kubwa ziliinuka juu ya miwani yake na kwa mara ya kwanza mmuliko wa tabasamu ukapita kwenye uso wake mkavu. "Hii itakuwa mara ya kwanza kutumia vipima-shangilio kwenye uchaguzi mjini humu. Badala ya kujaza fomu za kura, wapiga kura watasimama tu kwenye vibanda na kushangilia taa fulani ikiwaka kando ya jina la mgombeaji wanayempenda."
"Wagombeaji wana maoni yapi kuhusu huu utaratibu mpya wa uchaguzi?" akauliza Phil.
"Oh, wanaupenda, Phil. Inaonekana hata tayari wamekuwa wakiwatayarisha wafuasi wao kwa mabadiliko hayo. Wanatumia vikao virefu wakiahidi kutumia pesa za watu wengine kwa wafuasi wao na hizo ahadi daima hulidhalilisha bunge."
"Naam, ahsante sana kwa kuwa nasi leo na kwa kutupa utangulizi wa mustakabali bora. Tafadhali jiunge nasi tena, au vipi? Mabibi na mabwana, hebu sasa tumsikilie Dk Julia Parlor!"
Hatimaye shangilio ilipofifia na kwisha, mwalishi alipunga mkono tena kuelekea nyuma ya jukwaa. "Na sasa ndio ule wakati ambao nyote mmekuwa mkiungojea. Naam, right off the busy compaign trail - huyu hapa ni Joe Candidate! Hebu tusikie!"
Joe Candidate alipita jukwaani kwa madaha akiwa ameitanua mikono, huku akiuchangamkia na kuuchangamsha umati. Mgombeaji huyo alivalia suti ngumu ya mchanganyiko wa rangi nyeusi-na-nyeupe. Jonathan alidhani ndiye aliyekuwa na nywele nyeusi kabisa na meno meupe zaidi kuwahi kung'aa kwenye mwanga. "Shukrani, Phil. Hii ni fursa ya kipekee kwangu kuwa hapa nanyi watu wazuri nyote."
"Sasa Joe, ni sharti tu utwelezee hasa kisa kinachopelekea kisa kikuu chenyewe. Ulimshangaza kila mtu na ukagonga vichwa vya habari kwa kwa habari moto moto kwa zote humu kisiwani kwa zaidi ya mwongo. Sasa basi ; hebu fukua!"
"Penyewe, ah, Phil? Hapo ndipo nikupendeapo na kupenda tamasha hii! Ama kwa kweli nilishtuliwa sana na gharama kubwa ajabu ya kampeni za kisiasa katika miaka ya juzi. Kwa hivyo nikaamua kuchukua hatua fulani. Ninaamini kabisa kuwa wapiga kura wa hiki kisiwa maarufu wana haki ya kupiga bei wapate zaidi ya kitu kile. Hapo ndipo nilipoanzisha chama cha Generic."
"Chama cha Generic! Wazo zuri la kipekee sana! Na hata ukabadili jina lako, sio?"
"Hapo ni kweli, Phil. Kwa jina langu lenyewe, Elihu Root, singekuwa hasa mtu wa watu. Ni sharti ufunike mizizi yako ..." Huo mchezo wa maneno wa ghafula ulisababisha mngurumo wa kicheko kutoka kwa kila mtu, akiwemo Phil na Joe Joe akaendelea, "Sharti uwe na mvuto mkubwa ukitaka kuaminika."
"Umechukua hatua zipi ili habari ziwafikie watu, Joe?" "Chama cha Generic hivi karibuni kitasambaza vifaa vyake vya kimsingi, yaani vikaratasi vya rangi nyeusi-na-nyeupe, vifungo na mabango, katika vituo vyote. Ni tumaini letu kuwa tutaweza kupunguza hadi nusu gharama ya kawaida ya kampeni, kwa kutumia maarifa yetu.
Showman Phil akakatiza, "Lakini mna msimamo kamili katika masuala yenyewe?"
"Hakika, kama tu vyama vingine vyote", akasema Joe. Alitia mkono kwenye koti lake akatoa kitita cha karatasi. "Hii hapa stakabadhi yetu maalumu kuhusu uhalifu na hii hapa stakabadhi yetu maalumu kuhusu umasikini."
"Lakini, Joe, hakuna chochote kwenye hizi karatasi", akasema Phil, huku akizitazama kwa mshangao. Hizo zilikuwa zikisemwa kuwa ni stakabadhi maalumu, zilikuwa tu karatasi safi na tupu.
"Huo ndio urembo wake, Phil. Huelewi wewe? Ya nini kupoteza wakati ukimwahidi kila mtu kila kitu? Mbona usiwaache wapiga kura wakajaza hizo karatasi wenyewe? Ahadi na utekelezaji utakuwa tu kama hapo awali-tofauti ni kuwa tu tunaondoa gharama ya kupiga chapa."
"Uerevu ulioje! Huku wagombeaji wengine wakizungumzia kupunguza gharama za kampeni, wewe unafanya hasa jambo. Haya, wakati wetu unaendelea kudidimia. Tafadhali tupe muhtasari tu wa mambo muhimu kuhusu chama chako."
"Kweli, Phil. Tayari kinapata umaarufu kisiwani kote. Kauli-mbiu yetu ya chama cha Generic ni, 'Tunaamini mnavyoamini'!"
"Ahsante sana, Joe. Mabibi na mabwana, sasa hebu tushangilie mkondo mmoja mkubwa kweli kweli, kima cha 5.5, kwake Joe Candidate, stadi wa mfululizo huu wa kampeni.
© Copyright 2005,
Inter Region Economic Network, Nairobi, Kenya, All Rights Reserved.