Chapter 25 - SURA YA ISHIRINI NA TANO
IMANI YA KWELI
Shangilio lilipoanza kuishia, Joe Candidate alibakia amesimama tu pale bila kutikisika. Showman Phil, kutokana na shauku ya kuhifadhi mfululizo wa mambo, alimgusa Joe mabegani na kumwelekeza langoni. Joe alitabasamu tu na hakuonyesha dalili ya kusonga. Hapo tena Phil aliinua mikono yake kuinyamazisha hadhira.
Joe alianza kuongea. "Kuna mtu ambaye ningependa kukutana naye."
"Sawa, Joe, ama kwa kweli, lakini hatuna wakati wa kutosha."
"Itachukua dakika moja tu. Sharti niwaeleze kuhusu mmoja wa wapiga kura wetu wa ki-generic - mpiga kura wetu nambari moja wa ki-generic." Joe aligeuka upande akamsogelea mtu fulani nje ya jukwaa. Palikuwa hapaonekani mtu lakini Joe aliendelea kuashiria kwa upole, kana kwamba anamshawishi mtoto mdogo mwenye soni. Hatimaye mwanamke mmoja maj ya kunde mwenye umri wake alitokea, kwanza akifumbata mkunjo wa pazia, na kisha akifanya kujongea mbele.
Phil alikimbia mara moja kumkaribisha yule mwanamke mwenye maki ndogo na akamvuta mbele. "Mabibi na mabwana", akasema Phil haraka haraka, huku furaha yake ya uongo ikidhihirishwa na woga wa yule mwanamke, "Ama kwa kweli tuna furaha kuwa na nyongeza leo. Na hapa tunaye nani?"
Yule mwanamke mzee, akiwa amevalia kanzu sahii ya rangi nyeusi na nyeupe, alimfanya Joe aonekane kama kibonzo. Uso wake mweupe haukuonyesha hisia zozote, na macho yake yalikuwa kapa. Nywele zake zenye mvi za chumvi-na-pilipili zilikuwa zimechanwa vizuri juu ya masikio yake. Aliikamata kwa nguvu shanta ndogo ya rangi nyeusi-na-nyeupe, kama kwamba ilikuwa imebeba rasilmali yake ya muhimu kabisa.
Alipomfikia, Joe akaanza kuongea mfululizo. "Unavyojua, Phil, rekodi ya upigaji kura ya kisiwani imekuwa ya kuvunja moyo kwa miaka kadhaa sasa, lakini hilo halikumwua moyo mgeni wetu, Phoebe. Phoebe ametokea kuwa ndiye mpiga kura bora mwenye kuvunja rekodi kisiwani Korumpo!"
Macho yake Phil yalitanuka kwa mshangao. "Oh, ninajua habari zako! nimekusikia sana, mamaa. Huyu si mwingine bali ni mpiga kura bora na maarufu wa vipindi vyote; mshikilia rekodi ya upigaji kura; shujaa wa uamuzi wa kisiwani. Mabibi na mabwana, hakika tumebarikiwa kuwa naye si mwingine bali, Phoebe Simon!"
Kwa mara nyingine, umati uliwaitikia viongozi wake kwa shangilio karimu, ingawa wengine walikuwa wameanza kuhepa kupitia mlango wa nyuma. Wengine walificha miayo yao nyuma ya ratiba zao.
"Phoebe", akasema Showman Phil, "Nina swali ambalo nina hakika liko akilini mwa kila mtu." Akasita. Hadhira ilibakia tuli. Huku akipaaza sauti ili kila mtu apate kusikia, akasema, "Mbona wewe hukosi kupiga kura hata mara moja?"
Huku akionyesha ukembe kamili, Phoebe alijibu kwa sauti nyororo na tamu. "Naam, bwana, ni wajibu wangu kupiga kura. Hili Baraza linaniambia hivyo. Wanasema haijalishi ninampigia nani, bora nimepiga kura. Kwa hivyo ninapiga kura. Nimekuwa nikipiga kura kwenye kila uchaguzi kuanzia nilipohitimu kwa mara ya kwanza miaka hamsini iliyopita, hadi leo."
"Shabash!" akajibu Phil. "Miaka hamsini, si maajabu hayo, jamaa!" Kwa mara nyingine tena hadhira ilipiga makofi. "Lakini hebu nikuulize swali mpiga kura mkuu, Phoebe. Kuna msemo: 'Ovu dogo bado ni ovu.' Sasa hebu niambie ukweli, Bi Simon, huwa wapiga kura hata kama humpendi yeyote katika wagombeaji?"
"Kila mara, bwana. Wakati mmoja babangu aliniambia kuwa ikiwa sipigi kura, basi sina haki ya kulalamika kuwahusu viongozi waliochaguliwa. Mimi hupiga kura ili kuilinda haki yangu ya kulalamika."
"Hebu sikieni hilo, jamaa! Sasa hebu nambie, kusema kweli, Bi Simon, unaziamini ahadi za Joe?"
"Ama kwa kweli, ninaamini. Daima mimi huamini. Kama sikuamini, sasa ningempigia kura kwa nini?"
"Je, wajua wanavyosema wataalamu kukuhusu? Wanadai kwamba wewe ndiwe muumini wa mwisho kabisa miongoni mwa waumini wote wa kweli kisiwani Korumpo?"
"Naam, bwana, nimesikia mambo yao", Phoebe alijibu kwa sauti ya chini sana, karibu asisikike "Ninawaamini, pia. Ninakuamini. Ninamwamini kila mtu."
Akiugeukia umati, Phil alitia mkono kwenye moyo wake na kusema, "Mabibi na mabwana, je, mmewahi kusikia kitu kizuuri na cha kikembe hivyo? Si ajabu hii kweli kwamba ukembe bado waweza kupatikana kwenye hiki kisiwa chetu chenye kutojali kwa hali ya juu." Kisha akimrejelea mgeni akauliza, "Na, je, Phoebe Simon, mwakilishi wako amewahi kukuvunja.?"
"Oh, naam", akatetema, "Daima huwa anaanguka. Kila mara. Amenikasirisha mara nyingi. Lakini si mwachi, hata iweje." Aliukaba mkono wa Joe na akamjifinyilia kwa nguvu. "Na nitakuwa naye daima. Siwezi kukadiria maisha bila Joe pamoja na wawakilishi wangu wa hapo kabla yake!"
Kisha mtu mmoja kwenye hadhira akapaaza sauti, "Mbona uamini baada ya maumivu makubwa ya moyo?"
Alimtazama Joe kwa uchungu kisha akajibu, "Ninaamini ni mtu wa roho nzuri. Si mbaya. Ninaamini aweza kubadilika - Ninaweza kumsaidia kubadilika. Ninaamini kuwa kwa kweli ananijali. Ni kwamba tu hanielewi."
"Aaah!" hadhira ikapumua mtindo mmoja.
"Jamani, hili linanitia machozi machoni mwangu. Lakini, Phoebe, haya ni machozi ya hali ya kukujali na vile vile ya furaha. Baadhi ya watu kwenye aila yako wamejaribu kukufanya ujiunge na Wapiga Kura Fiche"
"Ah, la bwana!" alisema huku akisinyaa. "Wapiga kura Fiche ni kundi la watu wenye tatizo. Sina tatizo. Ama unadhani nina tatizo?"
"Phoebe, baadhi ya wataalamu hudai kwamba wapiga kura wanaotumiwa vibaya huwarudia tu wale wawakilishi wao bila kujali taabu inayowapata."
Huku akiinua uso kumtizama Joe kwa muamana akauliza, "Nina tatizo, Joe? Sidhani." Alipomwona Joe akitabasamu, akafoka, "Daima nitamuunga mkono mwakilishi wangu."
Kengele ililia nje ya jukwaa kumwashiria Phil kuwa wakati ulikuwa umepita. Phil aliwapaazia sauti wote, "Tungekuwa wapi kama hapangekuwepo waumini wa kweli kama Phoebe Simon? Haya, mabibi na mabwana, huo ndio muda wote tuliokuwa nao. Ahsanteni sana kwa kujiunga nasi. Hebu sote tuwaonyeshe Phoebe Simon na Joe Candidate jinsi tunavyowapenda wote!"
Umati ulilipuka kushangilia kwa shauku, wakiwa na furaha kuwa tamasha yenyewe ilikuwa imekaribia.
© Copyright 2005,
Inter Region Economic Network, Nairobi, Kenya, All Rights Reserved.