Inter Region Economic Network, Nairobi, Kenya  

Home
About IREN
Media & Press
Projects
News & Newsletters
Articles
Events
Resources
Speeches and Publications
Student Outreach
Contact IREN

Chapter 26 - SURA YA ISHIRINI NA SITA


KUTEGEMEA UHITAJI

Mvumo wa tarumbeta na mfululizo wa mapigo ya ngoma uliunyamazisha ule umati. Showman Phil aliinua mikono yake kuelekea kwenye hadhira, "Nyinyi wazazi mmekuwa mkisubiri vya kutosha. Hapa ndipo kilele chenyewe. Safari ya mwanao ya miaka kumi na miwili inaelekea kwisha. Ni mchezo wa kufuzu!"

Mziki wa kinanda ulihanikiza kwenye ule ukumbi mkubwa na ghafula milango ya kando kando ikafunguka. Mara wanafunzi wenye kuvalia vikofia na majoho marefu meusi wakatokea kwenye milango hiyo. Umati tena ukawa unashangilia shangilio kali, likiwemo vigelegele vya hapa na pale.

Jonathan akamnong'onezea mwanamke aliyekuwa amekaa karibu naye, "Mchezo wa kufuzu ndio upi?"

Alimgeukia nusu na kujibu, "Haya ni mashindano miongoni mwa vijana wa shule zetu za Baraza." Alisita kidogo kusikiza matangazo kisha akaendelea, akikazana kusikika dhidi ya kelele. "Ndicho kilele hasa cha elimu rasmi ya mtu. Kufikia sasa, nia hasa ya elimu rasmi imekuwa ni kuonesha umuhimu wa bidii na jitihada katika kusaka maarifa. Usiku huu tunawastahi wanafunzi bora kwa kufaulu kwao licha ya ushindani mkubwa, na ufanisi wao. Lakini zawadi kuu, ambayo bado haijatuzwa, ni kombe la kwaheri linalomwendea mshindi wa mchezo wa kufuzu."

Akitazama haraka jukwaani, Jonathan aliliona umbo zito ambalo ilielekea alilijua. "Ni nani yule anayewasalimu wanapokuja mbele?"

"Mbona, yule ni Bi Bess Tweed. Humtambui magazetini? Ndiye hasa hatibu wetu wa heshima. Kama mwanachama wa Baraza la Watawala na Malkia wa wanasiasa, yeye ndiye mgeni wa heshima, kama kawaida, na anaupenda huo umaarufu. Taaluma ndiyo inayosujudiwa sana na wakati huo huo ndiyo isiyoheshimiwa kabisa kisiwani. Kwa hivyo anafaa sana katika Mchezo wa kufuzu."

"Mchezo wenyewe huchezwaje?" akauliza Jonathan.

"Huwa hivi", akasema yule mwanamke huku akilijongelea sikio la Jonathan. "Bi Tweed hutoa mojawapo wa hotuba za kawaida zilizotayarishwa za kisiasa. Wanafunzi huandika pahali virai vyote ambavyo moja kwa moja ni kinyume na vile walivyozoea au walivyofunzwa shuleni. Yule anayepata virai vingi zaidi vya namna hiyo ndiye anayekuwa mshindi wa tuzo la fahari la kombe la kwaheri. Shhh, Bi Tweed ameanza. Sikiza."

"... kwa hivyo, tumejifunza kuhusu wema wa uhuru", akaroroma Bi Tweed. Sote tunajua jinsi hiari na uwajibikaji wa mtu binafsi hupelekea ukomavu na ukuaji. Hapo mko sawa na hiyo ndiyo hali ngumu ya jamii yetu nzuri. Wakati wote katika historia watu wamekuwa wakisaka uhuru. Ajabu iliyoje kuwa sasa twaishi kwenye kisiwa huru ...."

Yule mwanamke aliashiria kwenye wanafunzi nyuma ya Bi Tweed jukwaani. "Ona jinsi wanavyoandika kwa hasira. Oh, hoja nyingi sana wanazohitaji kuorodhesha!"

"Bi Tweed amesema kinyume na jinsi wanafunzi walivyofundishwa shuleni?" akauliza Jonathan.

Yule mwanamke akasema kwa bezo, "Hiari? Upuzi. Shule ni lazima. Wanafunzi hulazimishwa kuhudhuria na kila mtu hulazimishwa kulipia . Sasa kimya!"

" ... na tuna bahati kuwa na shule bora zaidi zinazoweza kufikiriwa, hasa wakati huu ambapo tunakumbana na kipindi kigumu kinachobashiriwa na wanauchumi wetu", akasema Bi Tweed kwa sauti inayoathiri. "Walimu wetu ni kielelezo cha tabia ya kutolewa mfano kwa wanafunzi wetu, huku wakimulika njia ya kuelekea kwenye demokrasia na ufanisi kwa mwanga wa ukweli na maarifa ..."

Mwanamke aliyekuwa amesimama karibu na Jonathan akamkaba mkono kwa furaha. Kisha kwa sauti nyembamba kama mlio wa paka akasema, "Binti yangu ndiye mwanafunzi wa tatu kutoka kulia kwenye safu ya pili. Anaandika; amepata hizo hoja zote, nina hakika."

"Sielewi", akauliza Jonathan. "hoja zipi?"

"Shule bora zaidi? Haiwezekani kulinganisha bila uteuzi. Bi Tweed aliwapeleka kibinafsi watoto wake vijijini kuhudhuria mafunzo, ilhali mamlaka yaliwatia watoto wetu katika shule za Baraza zilizoko karibu kabisa. Walimu walio kielelezo? Ha! Wanafunzi sharti wakae kimya na kupokea amri kwa miaka kumi na miwili. Kisha, wanapata alama za herufi na nyota za karatasi. Mwalimu akipata nyota za karatasi badala ya hundi ya malipo, atauita huo utumwa na agome! 'Kumulika njia ya demokrasia?' Haiwezekani! wanachofanya darasani ni utawala wa kimabavu."

Bi Tweed aliinamisha kichwa chake kwa unyenyekevu, "...sasa mmeifikia hii hatua maishani mwenu. Kila mmoja wetu anatambua kuwa yetu ni sauti moja ndogo tu katika wimbo mkuu wa kizazi kizima cha binadamu. Tunajua kuwa ushindani wa kutisha na mapambano katili yenye uchu katika jitihada za kufikia kilele hayafai katika ulimwengu wa leo. Kwetu, jambo jema na la hekima zaidi ni kujinyima. Kujinyima kwa ajili ya mahitaji ya wengine, kwa ajili ya wengi wasiobahatika......"

Yule mwanamke karibu apige unyende kwa furaha. "Watizame wanafunzi hao wakiondoka! Mgodi ulioje wa vinyume! 'Wimbo mkuu wa kizazi cha binadamu'? 'Kujinyima?' Shuleni, daima walifunzwa kufana, kuwa bora zaidi kila mmoja wao kwa manufaa yake binafsi. Na Tweed, mwenyewe, hajilegezi. Ndiye anapiga kelele zaidi, ndiye anayejitakia makuu zaidi, na ndiye mkosa adili kabisa kwa wote. Amefaulu kujiingiza uongozini kwa kila namna ya ujanja iwezayo kufikiriwa. Hawa wanafunzi wanaelewa kuwa hawakufikia hiki kiwango kwa kujinyima alama zao kwa ajili ya wale wanafunzi wasio werevu vya kutosha miongoni mwao."

Jonathan hakuweza kuyang'amua haya. "Unamaanisha, shuleni wanafunzi wanaambiwa kupata ufanisi kila mmoja kivyake. Na ilhali, wanapo fuzu, Bi Tweed anawaambia wajinyime kwa ajili ya wengine?"

"Sasa umegonga ndipo", akajibu yule mwanamke. "Bi Tweed huwahubiria wanaofuzu jinsi dunia yao ilivyobadilika. Kuanzia kila mmoja kulingana na uwezo na hadi kila mmoja kulingana na uhitaji. Huo ndio mustakabali wao."

"Hawangeweza kuweka muoano kati ya yale wanayofunza kabla na baada ya kufuzu?" akasaili Jonathan.

"Mamlaka yanalishughulikia hilo", akasema yule mwanamke. "Shule bado zinautumia utaratibu uliopitwa na wakati ambapo mwanafunzi hupata alama za juu anapofanya vizuri zaidi. Mwaka ujao wana mpango wa kubadili utaratibu wa kutoa alama. Wanapanga kutumia viinua-mgongo na zawadi zinazowatayarisha wanafunzi kukumbana na hali halisi mpya. Alama zitatolewa kutegemea uhitaji badala ya jinsi anavyofanya. Wanafunzi wabaya zaidi watapata A na wale wazuri zaidi watapata alama F. Wanasema kuwa wanafunzi wabaya zaidi wanahitaji alama nzuri zaidi kuliko wanafunzi wazuri."
Huku akitikisa kichwa, Jonathan aliyarudia maneno yake ili kuhakikisha kuwa ameyasikia vilivyo, "wanafunzi wabaya zaidi watapata A na wanafunzi wazuri zaidi watapata F?"

"Ndivyo", akagoteza.

"Lakini itakuwaje kuhusu viwango? Huoni kama kila mtu atajaribu kuwa mhitaji zaidi na mwenye uwezo duni?"
"Muhimu, kwa mujibu wa Tweed, ni kuwa hii itakuwa hatua ya kijasiri ya kibinadamu. Wanafunzi wazuri zaidi watajifunza wema wa kujinyima kama mwanadamu na wanafunzi dhaifu watapata funzo la wema wa kujiamini. Wasimamizi wa shule aidha wamehimizwa kufuata utaratibu huo huo katika kuwapandisha vyeo walimu."

"Walimu nao wamechukuliaje?" akauliza Jonathan.

"Baadhi wamefurahia na baadhi hawakufurahia. Binti yangu kanieleza kuwa walimu bora wametishia kuhamia kwingineko ikiwa utaratibu huo utaifadhinishwa. Tofauti na wanafunzi, walimu bado wana uhuru wa huo uteuzi - kwa sasa."








© Copyright 2005,
Inter Region Economic Network, Nairobi, Kenya, All Rights Reserved.