Inter Region Economic Network, Nairobi, Kenya  

Home
About IREN
Media & Press
Projects
News & Newsletters
Articles
Events
Resources
Speeches and Publications
Student Outreach
Contact IREN

Chapter 27 - SURA YA ISHIRINI NA SABA



UJIRA WA DHAMBI

Jonathan aliuacha ule umati uliokuwa ukishangilia kwenye ukumbi wa ikulu, na akateremkia kwenye ubebeshori mrefu. Upande wa mwisho, safu za watu zilikaa kwenye mabao, wote wakiwa wamefungwa pamoja kwa silisili za miguu. Je, hawa walikuwa wahalifu wakingojea hukumu? Labda wasimamizi wa hapa wanaweza kumsaidia akapata pesa zake zilizoibwa.

Upande wa kushoto wa bao mojawapo palikuwepo mlango wenye anwani, "Halmashauri ya Kazi Ngumu." Upande wa mwisho wa bao hilo palisimama walinzi wenye kuvalia sare wakiongea kwa sauti za chini, bila kuwajali wafungwa wao waliokuwa kimya. Silisili nzito walizofungiwa hawa mateka zilihakikisha kuwa hapakuwepo matumaini makubwa ya kutoroka.

Jonathan alimjongelea mfungwa aliyekuwa karibu zaidi, mvulani mwenye umri wa miaka kumi hivi ambaye hakuonekana kuwa mhalifu hata kidogo. "Mbona uko hapa?" akauliza Jonathan kwa ukembe.

Mvulana yule aliinua uso akamtizama Jonathan kisha, haraka haraka, akawatazama walinzi kiujanja. Kisha akajibu, "Nilikutwa nikifanya kazi."

"Ni kazi gani hiyo ambayo ingeweza kukutia matatani hivi?" Jonathan akauliza huku macho kayakodoa kwa mshangao.

"Nilipanga bidhaa rafuni katika Duka Jumuishi la Jack", akajibu yule mvulana. Karibu aseme zaidi, kisha akasita na kumtizama mwanamume mmoja mwenye mvi aliyekuwa ameketi kando yake.

"Nilimpa kazi", akasema Jack, mwanaume mzito mwenye umri wa makamo, na mwenye sauti nzito. Huyo bepari alikuwa bado kavalia msurupwenye wake wa kazi wenye mawaa - na sili sili za miguu ambazo zilitumiwa kumfunga yule mvulana pia. "Huyu mtoto alisema alitaka akikua aje kuwa kama babake, msimamizi katika bohari la kiwanda. Sidhani kama kuna kitu cha kiasilia zaidi ya hicho. Kiwanda hicho kilipofungwa babake alikuwa na matatizo ya kupata kazi nyingine. Hivyo basi, nikaonelea kwa kumpa huyu kijana kazi nitakuwa nimeisaidia aila hiyo kwa kiasi fulani. Sharti nikubali ilikuwa na manufaa kwangu pia. Hayo maghala makubwa yalikuwa yananitia hasara na nikawa ninahitaji angaa usaidizi bahasa. Basi, yameisha hivyo sasa." Hali ya kutokuwa na matumaini ilionekana usoni pake.

Yule kijana mdogo akasikika, "Shuleni sikuwahi kulipwa kusoma na kufanya hisabati. Jack hunilipa. Nilishughulika na orodha ya bidhaa pamoja na vitabu - na Jack aliahidi nikifanya vizuri angeniruhusu kuagiza bidhaa. Kwa hivyo nilianza kusoma majarida na arifa za biashara. Na niliweza kukutana na watu, sio watoto tu shuleni. Jack alinipandisha cheo na nikawa ninamsaidia babangu kulipa kodi - hata nilijipatia pesa za kutosha kununua baiskeli. Kama singelipwa chochote, ningesifiwa kwa kujitolea kusaidia. Lakini nililipwa na ndio maana nimepanuka kifua", sauti yake ilififia huku akitizama ardhi. "Na ni sharti nirudi huko kujisingizia."

"Kujisingizia si kubaya vile, mwanangu, ukizingatia badili yake", akasema mwanaume mmoja mnene mchangamfu, mwenye kikapu kilichojaa maua meupe ambayo tayari kaanza kunyauka. Alikuwa amefungwa silisili zilizopita na kuufunga mguu wa pili wa yule kijana. "Ni vigumu sana kuendesha maisha. Sikuwahi kupendelea kumfanyia kazi mtu mwingine yeyote. Hatimaye, nilifikiria nimefaulu na rukwama yangu ya maua. Nilifanya vizuri sana katika uuzaji wa 'pikaki' na 'plumeria' kwenye Eneo-Wazi la mji. Watu-yaani wateja wangu waliyapenda sana maua yangu. Lakini wenye maduka waliudhika hawakuupenda huo ushindani. Wakalipelekea Baraza la Watawala kuharamisha 'wachuuzi.' Mchuuzi! Naam, ndivyo wanavyoniita maana singeweza kuwa na duka. Vinginevyo ningekuwa 'mwenye-duka' au 'bepari.' Sinuii kukuudhi kwa vyovyote, Jack, lakini namna yangu ya kuuza ilikuwepo muda mrefu kabla ya duka lako. Haidhuru, waliniita kichukizi, kizembe na sasa haramia! Waweza nifikiria mimi na maua yangu kuwa hivyo vyote? Angaa sikuishi kwa kutegemea misaada."

"Lakini uliuzia kwenye maeneo ya wapita miguu", akabisha Jack. "Ulifaa kuyaacha wazi kwa wateja wangu."

"Wateja wako? Unamiliki wateja, Jack? Naam, hakika, nilikuwa kwenye mali ya Baraza. Yafaa kumilikiwa na kila mtu, lakini sivyo ilivyo, au vipi Jack? Kwa kweli inamilikiwa na wale wanaopendelewa na Watawala."

Jack akafoka, "Lakini hamlipi ushuru wa juu wa mali tunaohitajika kulipa sasa wenye maduka!"

"Hivyo basi ni nani afaae kulaumiwa hapo? Sio mimi!" akasisitiza mchuuzi kwa kero.

Jonathan akakatiza kwa swali, akinuia kupoza ule ubishi. "Kwa hivyo walikukamata papo hapo?"

"Oh, nilipata kuonywa mara kadhaa kwanza. Lakini sikujali kuwasikiza. Kwani wanafikiria wao ni nani, mabwana zangu? Ninajaribu kujifanyia kazi mwenyewe, na wala sio dubwana lolote. Haidhuru, mnyama yuko sawa. Sihitaji kufanya kazi na ninapata milo mitatu ya kisawa sawa kila siku na chumba, vyote vikigharamiwa na mwenye-duka. La kushangaza zaidi, Sheha anafikiria ananifanyia upendeleo. Anasema atanihawilisha ndipo niweze kuchangia maendeleo ya jamii. Anazungumza ushuru sio maua."

Kijana mdogo alianza kusinasina. "Si watanipeleka zoo pia?"

"Usijali, mtoto" akamtuliza muuza maua. "Wakifanya hivyo, bila shaka utajifunza maarifa fulani maalumu."

Jonathan aliligeukia kundi la wanawake waliovalia misurupwenye waliokuwa wamefuatia kwenye safu. "Mko hapa kwa sababu gani?"

"Tuna mashua ndogo ya kuvua samaki. Mmojawapo wa wakubwa alinisimamisha nilipokuwa na masanduku kadhaa mazito kule gatini", akasema mwanamke mmoja mwembamba aliyesawijika mwenye macho makali. "Aliniambia ninakiuka kanuni za usalama." Akiwaashiria wenzake, akaongezea, "Hizo kanuni zinadaiwa kutulinda mahali petu pa kazi. Wakubwa walituzuia mara mbili, lakini tuliwakwepa tukarudi gatini kutayarisha tanga kwa msimu ujao. Walitushika tena na wakasema mara hii watatulinda sawa sawa korokoroni."

Yule mwanamke alishangaa kwa sauti, "Watamfanyaje mwanangu jamani? Ana umri wa miaka mitatu tu lakini ni mzito kuliko hayo masanduku niliyokuwa nikibeba. Hakuna aliyelalamika kwa kuniona nikiwa nimembeba!" Huku akijikaza kuyazuia machozi yake, akaongezea, "Sasa itawabidi kumtafutia mtu mwingine wa kumbeba."

"Kupata mtu mwingine si rahisi", akasema mwanamume mmoja mwenye ndevu nyingi zilizouficha uso wake ulioduduika. Huku akimpiga kumbo kijana aliyekuwa kando yake kwenye bao, akasema, "George amekuwa akinifanyia kibarua kwa misimu miwili ya kipupwe mfululizo, kama mfanyakazi mwanafunzi hivi. Hunisaidia kuweka safi kibanda changu cha kinyozi na huwatayarisha wateja wote. Nilipojaribu kumfundisha unyoaji, tulijikuta tatani kwa sababu si mwanachama wa chama husika." Akarusha mikono yake kwa uchungu.

Kijana George, akitizama kwa huzuni, akalalamika, "Mambo yakiendelea kwenda hivi, na kuongezea kwamba sasa nimo kwenye orodha ya waliowahi kupatikana na hatia, sitawahi kupata leseni yangu."





© Copyright 2005,
Inter Region Economic Network, Nairobi, Kenya, All Rights Reserved.