Chapter 28 - SURA YA ISHIRINI NA NANE
WAGENI WAPYA
"Mnadhani mna matatizo?" akasema mwanamke mmoja aliyeonekana mwenye madaha, huku akionyesha kuudhika kwa kufungwa pamoja na watu aliowaona kuwa wa kima cha chini sana. Huku machozi yakikaribia kumtoka, alitia kitambaa chororo machoni pake na kusema, "Waandishi wa habari wakigundua kuwa mimi Bi Ins, nimekamatwa, kazi ya mume wangu itakuwa imekwisha. Sikudhani nilikuwa nikifanya cho chote kibaya. Je, nyinyi mlifanya nini?"
Akiwakumbatia mume na mke mmoja vijana waliokuwa wamefungwa kando yake, Bi Ins aliendelea, "Miaka kadhaa iliyopita nilikuwa na maskani kubwa, watoto watatu waliosomea shule bora kabisa, na nilitaka kuirejelea kazi yangu. Jirani yangu alikuwa daima yumo safarini na hivyo nikamwambia aniangalilie watu wanaoweza kunisaidia kazi za nyumbani. Aliwapendekeza hasa Jiyo na Shar nami nikawachukua mara moja. Shar ni mzuri sana kwenye bustani na uchukuzi. Ni msichana awezaye kutengeza cho chote nyumbani na anatumika bila kuchoka."
"Naye Jiyo, sahibu kweli, amekuwa mwokoaji wangu. Ni mzuri sana upande wa watoto mvulana huyo. Daima huwepo kila nikimhitaji. Hupika, husafisha, hunyoa - hufanya shughuli alf-lela-u-lela vizuri zaidi kuliko ningelivyoweza. Wavulana wangu wanaupenda uokaji wake wa biskuti ajabu. Nifikapo nyumbani huweza kubarizi na mume wangu na kucheza na watoto."
"Ama kwa kweli huo ni msaada ambao kila mtu angependa kupata", akasema Jonathan. "Palitokea nini?"
"Kila kitu kilikuwa sawa tu mwanzoni. Kisha mume wangu akapata cheo kipya kuwa msimamizi wa Halmashauri ya Hiari Njema. Mahasimu zake waliyachunguza masuala yetu ya kifedha na wakagundua kuwa hatukuwahi kuwalipia Jiyo na Shar ushuru wa kustaafu."
"Mbona hamkufanya hivyo?" akauliza Jonathan.
"Huku ushuru ukiwa juu na mapato yangu yakiwa chini hatungemudu wakati huo. Na hawaruhusiwi kuchukua malipo ya kustaafu hata hivyo."
Jiyo aligutuka akasema, "Ripoti sana shida kubwa yetu."
Mkewe alimdukua na kunong'oneza, "Chunga, Jiyo. Hatari kubwa."
Jiyo akamjibu mkewe kwa ujasiri, "Bibi tusaidie. Tumsaidie sasa." Kisha akamwambia Bin Ins, "Yaokoe maisha yetu. Tunatoka kisiwa cha kwetu cha El Saddamadore. Njaa na vita vibaya sana. Sisi hapana chaguo - kuondoka, njaa au sisi uawa. Hivyo nakuja sisi Korumpo. Bibi pana saidia sisi kufa."
"Hizo kweli", akasema Shar, kwa sauti hafifu. "Sasa mimi sikitika sisi mpa bibie taabu."
Bi Ins alipumua mpumuo mzito akasema, "Mume wangu atapoteza cheo chake kwenye Halmashauri ya Hiari Njema na labda kazi yake ya zamani pia. Amekuwa mkuu wa Sisi Tume Kuu, akiendeleza fahari ya kitaifa. Maadui zake watamtuhumu kwa unafiki."
"Unafiki?" akauliza Jonathan.
"Naam. Sisi Tume Kuu haipendelei wageni wapya."
"Wageni wapya?" akarudia Jonathan. "Wageni wa zamani ndio wepi?"
"Wageni wa zamani? Hao ni sisi wengineo", akasema Bi Ins. "Hiki ni kisiwa. Kwa miaka mingi, mababu zetu wote walikuja kama wageni kutoka kwingineko, ama wakiyatoroka mateso au wakijaribu kuboresha maisha. Lakini wageni wapya ni wale waliowasili juzi. Wamepigwa marufuku na sheria ya Pulluptheladder."
Jonathan aliyapokea hayo kwa taabu. Hakupenda kuwazia kile ambacho kingetokea mamlaka yakigundua kuwa yeye pia ni mgeni mpya. Akijaribu kutoonekana kuwa na shauku sana, aliuliza, "Kwa nini hawawataki wageni wapya?"
Mwanamke mvuvi alikatiza, "wageni wapya wanakubaliwa ikiwa watatumia pesa zao huku na kuondoka mara moja. Ni watalii au wafanya biashara. Lakini Baraza la Watawala lina tashwishi kuwahusu wageni wapya masikini, wale ambao huenda wakatuama. Wengi wao hufanya kazi kwa bidii zaidi, masaa mengi zaidi, kwa gharama ndogo zaidi, vizuri zaidi, na bila kujali sana masilahi kama wenyeji. Wote hufanya kazi ambazo Bi Ins hawezi kugusa."
"Hebu ngoja kidogo tu!" akasema Jack. "Kuna malalamiko mengi ya kweli dhidi ya wageni wapya. Wageni wapya huwa daima hawafahamu lugha, utamaduni au desturi za kisiwani kwetu. Ninaupenda moyo wao wa kujitolea - wana ujasiri kiasi cha kuhatarisha maisha yao kuja huku kama wageni - lakini huchukua muda mrefu kujifunza kila kitu na hakuna nafasi ya kutosha. Hali hii ni changamano zaidi kuliko mababu walipovihama visiwa vya mbali."
Jonathan aliiwazia nafasi yote aliyoiona kisiwani Korumpo, misitu kusikokaa yeyote na makonde matupu. Watu wengi hawakupendelea nyika; walipendelea misongamano na shughuli za maisha ya mjini.
Bi Ins akamjibu Jack, "Mume wangu alitoa hoja hizo hizo dhidi ya wageni wapya. Daima alisema kuwa wageni wapya walihitaji kujifunza lugha na desturi zetu kabla ya kuruhusiwa kukaa. Sharti pia wawe na pesa, maarifa na wawe wanaweza kujitegemea, na wasichukue nafasi yoyote. Mume wangu alipendekeza sheria mpya ya kuwatambua na kuwarejesha kwao wale wasiokubalika, lakini pakawapo mkwamo. Ufafanuzi wa wageni wapya haramu uliwahusu zaidi watoto wetu kuliko watu wenye vipawa kama Jiyo na Shar."
Wanaume wawili wenye sare ngumu waliingia ghafula, kila mmoja akivutwa na mbwa mkali mweusi. Moja kwa moja walimwendea Bi Ins, ambaye alisinyaa kwa woga kutokana na mpumuo mzito wa wale majibwa pamoja na meno yao makali yaliyokuwa yakidondokwa mate. Mmoja wao alimwashiria mlinzi kuzifungua silisili kwenye miguu ya Bi Ins. Kwa sauti nzito alisoma stakabadhi fulani mtindo mmoja, "Sahibu Bi Ins, tungependa ...." Alisita kumwonyesha mwenzake ile barua, akanong'oneza, kisha akaanza tena. "Sahibu Bi Ins, tungependa kukuomba msamaha kwa huku kutoelewa kulikotokea kwa bahati mbaya. Bi Ins, tungependa kukuhakishia kuwa suala hili lote zima linashughulikiwa katika viwango vya juu kabisa."
Akionekana mwenye nafuu, aliwafuata wale watu kupitia kwenye ukumbi mkubwa bila kuthubutu kuwaangalia Jiyo na Shar kule nyuma. Wengine walitizama kwa kimya kizito ambacho kilikatizwa tu na mgoto wa silisili. Bi Ins alipotoweka, wale walinzi waliwageukia Jiyo na Shar, wakawafungua na kuwatenga na lile kundi na pia wakawatenganisha wao wenyewe. Huku wakiwasukumia upande mwingine, walinzi wakafoka, "Kwendeni, washenzi nyinyi. Rudini mlikotoka."
"Sisi hapana mbaya!" akasihi Shar. "Sisi nakufa!"
"Hainihusu mimi", akabwabwaja mlinzi.
Mwanamke mvuvi alingojea hadi wakateremka ngazi na mlango ukajifunga nyuma yao, kisha akaboboja kwa sauti ya chini, "Naam, ndivyo ilivyo."
Jonathan alitetemeka kidogo akiyafikiwa yaliyokuwa yamewangojea yule mwanamke na mumewe na labda hata yeye mwenyewe. Aliinua uso akamuuliza yule mwanamke, "Kwa hivyo kila mtu kwenye hii silisili yuko hapa kwa sababu hakukubaliwa kufanya kazi?"
Akimwashiria kidole kijana mmoja mwanamume aliyekuwa kaufutika uso mikononi mwake, mwanamke akajibu "Kwa mtizamo huo yeye pekee ndiye kighari. Wakubwa walisisitiza akubali kufanya kazi ya uanajeshi. Alikataa - kwa hivyo akafungwa pamoja nasi kwenye hizi silisili."
Jonathan hakuweza kuuona hasa uso wa yule kijana, japo alishangaa mbona wazee wa mji wamtake kijana mmoja mbichi kama huyu kuwapigania vita yao. "Mbona
wamlazimu kuwa mwanajeshi wao?"
Mwanamke mvuvi akamjibu Jonathan, "wanasema ndiyo njia ya pekee ya kulinda jamii yetu huru." Maneno yake yalipiga mwangwi katika masikio ya Jonathan, dhidi ya kelele za silisili.
"Kuilinda dhidi ya nani?" akasaili Jonathan.
Mwanamke yule akakunja uso, "Dhidi ya wale wanaoweza kutufunga silisili."
© Copyright 2005,
Inter Region Economic Network, Nairobi, Kenya, All Rights Reserved.