Chapter 29 - SURA YA ISHIRINI NA TISA
UKARIMU AU GHILIBA?
Ikulu ya Watawala ilikuwa na vyumba na kumbi sufufu. Jonathan alianza kupata harufu ya kitu kitamu - kahawa na mkate uliookwa wakati huo huo! Alifuata pua yake kwenye ubebeshori hadi kwenye ukumbi wa mikutano ambamo wanaume na wanawake kadhaa wa makamo walikuwa wamesimama, wakibishana kwa ghadhabu na kutikisa ngumi zao. Baadhi waliwashika mikono wengine waliokuwa wakilia kimya kimya.
"Lipi lililojiri?" akauliza Jonathan, huku akiliona kapu kubwa limetulia katikati mwa ukumbi. Lilibakia kidogo sana kufika darini. "Mbona mmekasirika sana hivyo?"
Wingi wa wale wazee walimpuuza na wakaendelea kuomboleza na kulalamikiana. Lakini mtu mmoja mwenye makini aliinuka polepole akamjongelea Jonathan. "Yule Mtawala mwenye kiburi", akafoka, "amerudia tena! Ametughilibu!"
"Amefanya nini?" akasaili Jonathan.
"Miaka kadhaa iliyopita", huyo mzee akasema kwa kejeli, "Mtawala Mkuu Ponzi alituelezea kuhusu mpango maalumu wa kumlinda kila mtu dhidi ya njaa uzeeni mwake. Wazo zuri, hmh?"
Jonathan alitikisa kichwa kukubali.
"Naam, hivyo ndivyo tulivyofikiria pia. Puka Chaka!" akamaka kwa adha. Kufuatia msiba, kila mtu, isipokuwa huyo mheshimiwa mtukufu Carlo Ponzi na Baraza lake, alipata arifa ya kuchangia mikate kwenye huu mjikapo kila wiki. Wanauita Kapu la Hazina ya Muungano."
"Kila mtu alichangia isipokuwa Mtawala Ponzi na Baraza lake?" akarudia Jonathan.
"Mhhhm, walipata ukarimu spesheli", akajibu mzee. "Tulihitajika kuweka wingi wa mikate yetu wenyewe kwenye kikapu tofauti walichotengewa wao. Sasa ninafahamu mbona walitaka kikapu chao wenyewe kando."
"Ninadhani ni jambo zuri sana kuwa na mikate uzeeni mwako", akasema Jonathan.
"Ndivyo tulivyofikiria pia. Lilionekana kuwa wazo zuri ajabu maana daima pangekuwapo mikate ya kuwalisha wazee. Kwa sababu tulitegemea Kapu la Hazina ya Muungano, wengi wetu hatukujiwekea mkate wowote binafsi kwa ajili ya mustakabali. Tulionelea pia kuwa hatukunuiwa kuwasaidia aila na majirani zetu, maana Baraza lingetushughulikia sote."
Mabega yake yalibonyea kama kwamba yalielemewa na mzigo wa maisha yake yote. Mzee alilitizama lile kundi la wazee wakongwe na watepetevu. Akimwashiria bwana mmoja wa makamo aliyekuwa ameukalia ubao hapo karibu. "Siku moja rafiki yangu, Alan, aliwatizama watu wakiweka na kutoa mikate kwenye kapu. Alan alikadiria kuwa hivi karibuni Kapu la Hazina ya Muungano lingebakia tupu. Wajua alikuwa muuza - duka hapo kabla. Basi, Alan akapiga kamsa. Alan alianza kugoteza kwa mtetemeko.
"Tulienda moja kwa moja hadi kwenye kapu na tukapandia upande. Kilikuwa kibarua kigumu ndio lakini sisi si vipofu na wanyonge kiasi wanavyofikiria baadhi ya hao Watawala vijana. Haidhuru, tulipotizama ndani tuligundua kuwa kapu la chakula lilikuwa karibu tupu. Habari hizo zilizua malalamiko. Tulimwambia Mtawala mtukufu Ponzi papo hapo kwamba achukue hatua ya haraka la sivyo ngozi yake pekee ionekane kwenye uchanguzi ujao!"
"Eh, ninadhani alitishika", akasema Jonathan.
"Kutishika? Sikuwahi kumwona mtu akikiakia kiasi hicho. Anafahamu kuwa tuna athari kubwa hasa tunapokasirishwa. Kwanza, alipendekeza kuwapa wazee mikate hata zaidi, kuanzia kabla tu ya uchaguzi ujao. Kisha angechukua mikate zaidi kutoka kwa wafanyakazi vijana, kuanzia tu pale uchaguzi unapomalizika. Lakini wafanya kazi waliungamua mpango wake na wakachafuka, pia. Wale wafanyakazi wabichi walisema walitaka mikate wakati huo. Walisema kuwa maghala yao yaliweza kuilinda mikate dhidi ya kuvu na panya vizuri zaidi kuliko kapu la Baraza. Na hawaamini kuwa watawala hawataweza kuidokoa hiyo mikate hadi watakapostaafu."
"Kisha alifanyaje sasa?" akasaili Jonathan.
"Huyo Ponzi daima huwa na mbinu mpya. Kisha alisema kuwa kila mtu angojee kwa miaka mitano, hadi umri wa miaka sabini, kabla ya kuanza kupata mikate kutoka mle kapuni. Hili liliwaudhi wale waliokuwa wamekaribia kustaafu, wale waliotarajia kuanza kuchukua mikate katika umri wa miaka sitini na mitano kama ilivyoahidiwa hapo kabla. Hatimaye Ponzi aliibuka na wazo jipya la kipekee."
"Tena kwa wakati ufaao!" akamaka Jonathan.
"Kwa wakati ufaao kutegemea siku ya uchaguzi. Ponzi alimuahidi kila mtu kila kitu! Angewapa wazee zaidi na kuchukua kidogo kutoka kwa vijana. Sawa! Aliahidi kutoa zaidi kwa kutwaa kidogo na kila mtu atafurahi!" Mzee alisita kuona kama Jonathan alikuwa akiona kilichokuwa kikiendelea. "Atakaposhikilia ni kuwa mikate itaendelea kuwa midogo zaidi kila mwaka. Yap. Mikate itakuwa midogo sana kiasi kwamba tutaweza kuwa na mlo wa mikate mia - na bado tusishibe."
"Walaaniwe maharamia!" akalipuka Alan. "Mikate hiyo ikiisha watatufanya tule picha za mikate!"
© Copyright 2005,
Inter Region Economic Network, Nairobi, Kenya, All Rights Reserved.