Inter Region Economic Network, Nairobi, Kenya  

Home
About IREN
Media & Press
Projects
News & Newsletters
Articles
Events
Resources
Speeches and Publications
Student Outreach
Contact IREN

Chapter 30 - SURA YA THELATHINI



WAZO ZURI LA NANI?

"Huree, huree!" akapiga kelele mwanamume mmoja kwa mshtuko, wale wanaume na wanawake wa makamo walikodoa macho wakishangaa huo usumbufu mkubwa. Mtu mwenyewe alikuwa nadhifu, masharubu yakiwa yamenyolewa vizuri na amevalia mavazi ya meli. Alijitoma mle chumbani, akiliongoza kundi la wanaume waliovalia suti za kuvutia za rangi ya giza, wote wakiwa wamebeba visanduku.

Walimtizama kwa upendo kwamba maisha yao yalimtegemea. Kiongozi wao alienda hadi kwenye meza kujipa kikombe cha kahawa, huku akiwafukuzilia mbali wafuasi wake kwa kuwapungia mkono kwa ukali. Wakiandamana kama kondoo, walielekea pambizoni mwa kile chumba kungojea amri zake.
"Hongera", akasema Jonathan, "kwa kila mnachosherehekea." Jonathan alitamani kumtilia kahawa huyu mtanashati, huku akiichunguza mistari mikali ya mavazi yake. "Sijui utachukuliaje nikiuliza mbona mmefurahi sana?"

"Hamna ubaya", mwungwana akasema kwa fahari. "Ahsante kwa kahawa. Oh! ni moto! Kumbuka hilo, Nambari Mbili", akamwambia mfuasi aliyekimbia kuchomoa kijitabu mfukoni mwake. Akirudisha kahawa chini, bwana huyo alimnyoshea Jonathan mkono akisema, "Jina langu ni George Selden. Lako je?"

"Jonathan. Jonathan Gullible. Nimefurahia kukutana nawe."

George alimsalimu Jonathan mkononi kwa nguvu na uchangamfu. "Jonathan, leo sina tashwishi kuhusu utajiri wangu. Nimeshinda kura ya maoni.

"Kura ipi?"
"Kutokana na ushindi wa kura tatu kwa mbili, mahakama kuu iliniidhinishia hati kiritimba ya kijichumakali."

"Hati kiritimba ndiyo nini?" akauliza Jonathan. Huku akiinua kifua kwa madaha,George akajibu, "Ndiyo karatasi yenye thamani kubwa kabisa kwa zote kisiwani Korumpo.Baraza lilitoa waraka wa kunipa mimi pekee haki ya kutumia maarifa mapya ya kimapinduzi katika upasuaji mbao.Hakuna yeyote atakayetumia kijichumakali bila idhini yangu. Nitakuwa tajiri vibaya sana!"

"Ni lini ulipofanya uvumbuzi huo?"
"Ah,si mimi niliyejitokeza na wazo hilo.Marehemu Charlie Goodyear, ndiye aliyefanyiza kila kitu na kupeleka karatasi kwa Halmashauri ya Kusimamia Maarifa.Alifariki kabla ya utaratibu wote kumalizika na nikamlipa mjane wake ruzuku kiasi kwa sababu ya haki ya Charlie kwa hayo maarifa.Yataleta mapato hivi karibuni!" Huku akiwagotezea kichwa wanaume waliorundikana pembeni, George aliongezea "Charlie hangemudu gharama ya kulikodi jopo hilo la wanasheria kivyake"

"Kwa hivyo ni nani aliyepoteza kura?" akasaili Jonathan.

"Watu tele!"George alitizama darini, huku akihesabu kichwani mwake. "Sharti wawe, naam, angaa wengine thelathini na wane walidai kuwa walikuwa walikuwa wamekiwazia kitu hiki kabla yangu, oh,yaani kabla ya Chrlie.Baadhi walidai kwamba kimantiki ulikuwa ndio uvumbuzi wa moja kwa moja baada ya ule wakijitijiwe.Ah! hata nyanyake Charlie aliwasilishia malalamiko yake akidai kuwa ndiye aliyeuwezesha uvumbuzi wake kufaulu.Naye mwandishi bunilizi fulani wa sayansi alijaribu kujifinyikiza ndani akidai kuwa Charlie aliiba maarifa kutoka kwake."

George alisita vya kutosha kugugumia kahawa yake
"Lakini hiki kikwazo cha mwisho cha mahakama ndicho kilichokuwa kikali zaidi.Mlalamishi alidai kwamba babake ndiye aliyekuwa wa kwanza kutia chuma kwenye mbao.Hata silikumbuki jina lake mwanamke huyo tena".

Jonathan aliguna huku akijaribu kukumbuka pale alipokutana na wafanyikazi wa mbao "Huyo mwanamke aliitwa Drawbaugh?" Alikumbuka kadhia ya kwanza na mfanyakazi wa mbao wa kwanza wa kike pale Kisiwani.

"Haijalishi hata. Jina-Lake-Nani alikuwa na mashahidi wa uongo zaidi ya … ishirini wakiungama kuwa alikuwa na hayo maarifa mda mrefu kabla.Alisema baba yake alikuwa mfua bati kwa kuzalika.Akasema yeye na babake walikuwa wakijaribu tu kuirahisisha kazi yake kwa kasi fulani.Kisha akajitafuta huruma kutoka wa mahakmu kwa kudai eti yeye jinsi alivyokuwa mfanyakazi maskini wa mbao hakuwa na fedha za kugharamia hati kiritimba na huduma za wanasheria.Lakini nilimharibia mambo kwa kutoboa siri ya rekodi yake ya kukamatwa juzi.Hapo nikavuruga kabisa muamana wa mahakimu kwake. Bahati ilioje,ah!"
"Bahati?" Akauliza Jonathan.
"Ninadhani alitaka kuingia kwenye vitabu vya historia.Sasa hakuna atakayemsikia tena." Huku akikirudisha kikombe chake chini tena,George aliuegemea ukuta na kuyatazama makucha yake yaliyopambwa vizuri huku akiuchangamkia tena ushindi wake. "Kila kimojawapo cha hivi vikwazo kinakuja kwa namna yake," akaendelea George. "Baadhi wanasema siwezi kumiliki matumizi ya maarifa __kwamba huko ni kuwanyima wengine uhuru.Lakini mahakama inasema ninaweza kwa sababu Charlie ndiye aliyekuwa wa kwanza kuwasilisha na hapana nafasi ya waja _kuchelewa. Ninayamiliki kwa miaka kumi na saba."
"Miaka kumi na saba? Mbona miaka kumi na saba?" akauliza Jonathan.
"Ni nani ajuaye?" akacheka. "Nambari ya kimwujiza, ninadhani".
"Lakini kama unayamiliki matumizi ya maarifa, mbona miliki hiyo iishe baada ya miaka kumi na saba? Kwani unapoteza mali yako yote baada ya miaka kumi na saba?"

"Hmmm". George alisita na kuchukua kahawa yake tena. Alianza kuikoroga huku akionekana kuwaza. "Swali zuri. Kwa kawaida hakuna vikwazo vya kiwakati kumiliki mali, isipokuwa tu Baraza likiichukua kwa sababu bora ya kijamii. Ngoja kidogo". Aliinua mkono wake na Nambari Mbili akaja mbio mara moja kutoka kwenye pambizo yake ya chumba kile. Huyu mwanamke aliyekuwa kama kijibwa ama kweli alidunda ubavuni kwa George kama mpira.
"Nikufae vipi, bwana?"
"Nambari Mbili, mweleze huyu kijana rafiki yangu ni kwa nini siwezi kumiliki hati-kiritimba kwa zaidi ya miaka kumi na saba".
"Sawa, bwana. Naam, ni hivi. Hapo zamani hati-kiritimba ama kweli iliwapa marafiki za mfalme idhini ya ukiritimba kutoka kwa mfalme mwenyewe. Hata hivyo siku hizi dhima ya hati-kiritimba…", akasema Nambari Mbili kwa mvumo wa sauti maalumu, "ni kuwamotisha wavumbuzi ambao, la sivyo, wangeishia kutovumbua vitu muhimu na kutokuwa na sababu yoyote ya kutoa siri zao. Karne moja iliyopita, mvumbuzi mmoja mwenye itikadi kali alilisihi Baraza la Mabasiri kwamba miezi sita chini ya vipindi viwili unusu vya mafunzo, kila kimoja kikidumu miaka saba, ingewezesha upendeleo wa kikiritimba wa kutosha kuwamotisha wavumbuzi".
"Tafadhali nisawazishe kama sikukuelewa barabara", akasema Jonathan, huku akijitahidi kuelewa. "Unasema kuwa kitu pekee kinacho wamotisha wavumbuzi ni ashiki yao ya kutajirika kwa kuwazuia wengine kutumia maarifa?"

George na Nambari Mbili walitazamana mtizamo isiyoonyesha hisia zozote. George akajibu, "kwani kuna sababu ipi nyingineyo?"
Ukosefu wao wa mawazo ya kibunifu ulimsikitisha sana Jonathan. "Kwa hivyo kila anayeunda kijichumakali sharti akulipe?"
'Ama hivyo au niviunde, mwenyewe, - vichache kwa kila kipindi maalum na kwa gharama kubwa', akasema George.

Namabari Mbili alicheka kicheko cha wasi wasi huku akimtizama George kiupande. "Ahem, bado hatuna hakika kulihusu hilo, bwana. Tayari tunalo jopo linalolishughulikia. Nadhani unakumbuka kuwa ni sharti tulishughulikie kwanza suala tata la sheria ya wafanyi kazi wa mbao inayopiga marufuku matumizi ya zana mpya. Kikao kingine na Bi Tweed kimepangiwa leo. Tukifaulu kuruhusiwa kuwa nje ya mipaka ya sheria hiyo, hapo labda wafanya kazi wa mbao watatufaa kwa kuyakalia maarifa hayo kwa miaka kumi na saba."

Akimgeukia Jonathan Nambari Mbili alieleza, "Wafanya kazi wa misitu wana wazo zuri lakini la kizamani kuwa matumizi yao ya maarifa ya kizamani sharti yalindwe dhidi ya matumizi yetu ya maarifa mapya. Kwa maoni yao, sisi ni waja-kuchelewa."

George alikuwa kazama kwenye mawazo. Bila kuzingatia mambo sawasawa, alitoa maoni, "Bila shaka hiyo sheria ya wafanya kazi wa misitu inakwenda kinyume na maendeleo, kwani hufikirii Nambari Mbili? Ninajua ninaweza kukutegemea. Daima uko mbele mchezoni".

"Lakini, bwana," akasisitiza Jonathan, "ingekuwaje kama hukushinda hati-kiritimba yako mahakamani leo?"
George aliwakumbatia mkumbatio mkubwa Jonathan na Nambari Mbili mabegani na kuwaelekeza kunako mlango. "Kijana, waweza kukisia kuwa bila hati-kiritimba singeweza kupoteza wakati nikipayuka nawe. Ningekimbilia kiwanda bora zaidi kuunda kijichumakali bora zaidi na haraka sana kuliko mtu mwingine yeyote. Naye Nambari Mbili angekuwa akitafuta kazi nyingine. Kweli au si kweli, Nambari Mbili? Labda uzalishaji, mauzo, au utafiti, badala ya sheria. Kila kijichuma kali kipya kingefaa kuwa na ufundi mpya kidogo sana ili kuwa tu hatua moja pekee mbele ya maarifa mapya!"

"ugh! Yatisha hayo!" akacheka Nambari Mbili.
"La, ningepata nafasi katika eneo lingine la sheria- mikataba au ufisadi, labda".

















© Copyright 2005,
Inter Region Economic Network, Nairobi, Kenya, All Rights Reserved.