Chapter 34 - SURA YA THELATHINI NA NNE
KASUMBA
Jonathan alikuwa hajaamua aende wapi sasa, wakati mwanamke mmoja mnene tipwa tipwa na aliyevalia ovyo ovyo alipomkurubia kwa makini. Nywele za yule mwanamke zenye mafuta mengi na zisizochanwa zilimuudhi. Alikuwa na harufu kama ya kinamasi kilichovunda. Mise alikimbia akajiendea hamsini zake. "psst! Waweza taka kuhisi vizuri?" akanong'ona yule mwanamke kwa kusita sita. Jonathan alisita kwa kero. Akarudia kwa sauti iliyoelekea kuvunja, "wataka kuhisi vizuri?"
Kutokana na maelezo ya yule afisa wa polisi kuhusu utovu wa adili. Jonathan hakuwa na hakika aseme nini. Hata hivyo, hakudhania kuwa huyu mwanamke wa kuudhi alikuwa akijaribu kuuza ngono. Kwa hivyo Jonathan, alivyokuwa mtoto mwaminifu na mwenye busara, alijibu kwa dhati, "Lakini si kila mtu hutaka kuhisi vizuri?"
"Nifuate," alisema yule mwanamke huku akimkaba mkono. Alimwongoza kupitia kwenye kichochoro hadi kwenye chumba kimoja kichafu na chenye kiza. Jonathan aliukumbuka wizi aliofanyiwa na hapo akasita - huku akizizuia pumzi zake ili kujikinga na uvundo wa yule mwanamke. Kabla ya kufanya pingamizi yoyote, yule mwanamke aliufunga mlango nyuma yake na akautia komeo. Alimwashiria Jonathan akae mezani. Alitoa paketi ya sigara kubwa kubwa mkobani mwake. Aliteua moja, akaiuma upande mmoja na kuiwasha upande ule mwingine kwa kiberiti. Kisha aliipiga mkupuo mmoja mrefu wa kuridhisha.
Jonathan alifurukuta kitini mwake kisha akauliza, "Wataka nini kwa hakika?"
Aliachilia wingu la moshi kwa fujo kisha, kwa kiburi, akasema, "Unataka forsadishangwe?"
"Forsadishangwe ni nini hasa?" akasaili Jonathan.
Macho ya yule mwanamke yalisinyaa kwa shaka.
"Hujui forsadishangwe?"
"La," alisema Jonathan huku akianza kuinuka kitini pake, "na wala sidhani kama nina haja ya kujua, ninakushukuru".
Yule mwanamke alimwamuru kuketi naye akasalimu amri shingo upande. Baada ya kupiga mkupuo wa sigara yake na kumtizama kwa makini, akisema, 'Tuseme wewe hukai hapa, au vipi?"
Jonathan alisita, kwa wasiwasi kuwa huenda yule mwanamke kakisia yeye alikuwa mgeni mpya. Lakini kabla hajajibu, yule mwanamke alifoka, "Wasiwasi wa uongo! Njoo hapa, Doobie."
Mlango uliokuwa umefichika nyuma ya kioo kirefu chembamba ulifunguka ghafula na afisa wa polisi mwenye sare akajitoma ndani. "Uhali gani?" akasema yule polisi akimwelekezea Jonathan mkono kumsalimu. "Mimi ni Doobie na huyu ni mwemzangu Mary Jane. Pole kwa kukutatiza lakini sisi ni mawakala wa kisiri wanaopambana na biashara ya forsadishangwe". Akimgeukia Mary Jane aliongezea, "Nina njaa sana. Hebu tumfidie huyu bwana mdogo kwa burudani ndogo, angaa".
Walianza kuvuta makasha, vifurushi, chupa, na magudulia ya kila tambo na umbo, kutoka kwenye kabati chakula! Jonathan alishusha pumzi kwa shufaa na akaanza kudondokwa mate kwa kuiona karamu iliyokuwa ikiandaliwa. Wenyeji walianza kula vyakula vitamu vitamu vilivyokuwa vimetatapakaa mezani. Palikuwepo vyakula vya kila namna - mikate iliyookuwa si muda mrefu kabla, siagi na jemu, silesi za jibini, vipochopocho vya chakleti, na vinginevyo vya ladha ya kupendeza.
Doobie alinyakua pande la biskuti na akalipaka siagi na jemu nyingi kwa kutumia vidole vyake. "Fakamia bwana mdogo". Alisema huku chakula kimemjaa mdomoni. Aliupunga mkono wake mezani, "Hapana mikahawa kwa kikosi cha Forsadishangwe, au sivyo Mary Jane?" Aligoteza tu huku mashavu yake manene yakiumka kwa jinsi yalivyojaa chakula.
Jonathan alitwaa silesi ya mkate wa jemu na kuila kwa hamu kubwa. Alisita kuzindua mazungumzo, akauliza tena, "Forsadishangwe ndizo nini hasa?" Mary Jane alimwaga kikombe cha kahawa na akamwaya vijiko vitatu vya sukari ndani yake. Huku akiukorogaea mtindi mzito kwenye kile kikombe, alijibu, "Kwa kweli hujui? Forsadishangwe ni tunda haramu. Kama ungejaribu kununua forsadishangwe kwangu, ungekwenda korokoroni kwa miaka kumi au ishirini".
Jonathan aliduduma kwa sauti ya kusikika chumba kizima. Alikuwa ameponea chupuchupu kwenda korokoroni! Mary Jane na Doobie waliangaliana kwa mda mfupi kisha wakaangua kicheko.
"Lakini ubaya hasa wa forsadishangwe ni upi? Akataka kujua Jonathan. "Je,huwafanya watu kuugua? Au wawe na fujo?"
"Athari mbaya zaidi ya hizo,"alisema Doobie huku akiutumia mkono wa shati yake kupangusa jemu na siagi iliyojipaka kwenye mashavu yake. Forsadishangwe huwafanya watu kuhisi vizuri. Wanakaa tu kimya na kuota."
"Inaudhi sana," akaongezea Mary Jane huku akiwasha sigara nene na kumpa Doobie. Huku akichukua biskuti iliyojaa siagi na kuipaka jibini nyingi, aliboboja, "Ni kuukwepa ukweli halisi."
"Naam," akasema Doobie, akiendelea kuusogeza ukanda wa bunduki yake ukae sawasawa na huku biskuti nyingine imemjaa kinywani. Jonathan alikuwa hajawahi kumwona mtu akifakamia chakula haraka haraka namna ile. "Vijana siku hizi hawana uwajibikaji wowote kwa maisha yao. Kwa hivyo wanapoanza kujihusisha forsadishangwe kama njia ya kukwepa, tunawarejesha kwenye uhalisi.Tuunawakamata na kuwatia mbaroni." "Na hivyo ni bora kwao?" akauliza Jonathan, huku akimpa Doobie kitambaa cha mkono wakati hasa alipokihitaji.
"Ama kwa kweli", akajibu Mary Jane "utapiga pegi ya wiski, Doobie?" Doobie alitabasamu na kumsogezea glasi yenye mafuta mafuta. Aliijaza kitu fulani maji maji cha rangi ya hudhurungi kutoka kwenye dumu lisilo kibandiko. Akilirejelea swali la awali la Jonathan, alijibu, "Unajua forsadishangwe huwa na usugu".
:Hivyo ni kusemaje?"
"Hivyo ni kusema daima utaendelea kutaka zaidi.Unahisi kana kwamba ili kuendelea kuishi ni sharti upate ".
Jonathan alizingatia hilo. "Yaani kama chakula?" alisema kwa sauti iliyoinuka juu ya mteuko mzito wa Doobie.
Dobbie alicheka kicheko cha kuridhika huku akimalizia pegi yake ya pili ya tembo na katika mtipuo mrefu wa sigara yake. "La ,la .katika forsadishangwe hamna lishe yoyote na yamkini hatari kwa afya .Hebu nipe kibakuli cha jivu, Mary Jane".
"Na kama forsadishangwe ni hatari kwa afya,"alisema Mary Jane huku akiikoroga kahawa yake kwa kipande cha halua , "basi sote tutalazimika kulipia matibabu ya hao watu ambao hatukuwajali kabla,haijalishi tabia na mienendo yao ilikuwa ya kijinga kiasi gani. Walaji forsadishangwe wasipodhibitishwa wataisha kuwa mzigo kwetu sote."
Jonathan aliboboka, "Mbona ugharamie ujinga wa watu wanaojidhuru wenyewe?"
"Ndicho kitendo cha kiutu kabisa uwezacho kutenda,"alisema Doobie, ambaye tembo ilishaanza kumtwaa kwa kiasi fulani. Mikono yake ilielea na kutikisika hewani sambamba na kila wazo lililopita akilini mwake . "Sisi hutatua matatizo ya wanadamu. Watawala wapaswa kutulipa kwa matatizo mengi ,unacheka, kama vile mishahara yetu na korokoro kubwa kubwa .Na usisahau kuwa mwaka uliopita , Baraza la Watawala liliwasaidia wakulima wa tumbaku na sukari kuupitisha mwaka mbaya . Wapaswa kuwalisha watu ,si wajua? Ushuru hutatua haya matatizo na mengineyo mengi . Ushuru huwafaa wagonjwa . Ndicho uwezacho kufanya .Leta Wiski, Mary Jane."
Mary Jane alimpa lile dumu na akatikisa kichwa kukubaliana naye. Aliwasha sigara mpya kutoka kwenye paketi yake kwa kuigusisha kwenye kibini cha ile iliyotangulia. Doobie alikuwa anaelekea kufikisha bumba zima. "Kwa sababu tunapaswa kumsaidia kila mtu ,ni sharti kuchunguza na kudhibiti kinachofanywa na kila mtu."
"Sisi?"aliuliza Jonathan.
"Eek! Aliteuka Doobie . "Kumradhi !" Alichomoa chupa ya dawa kutoka mfukoni mwa shati yake.
"Ninaposema sisi simaanishi wewenami kama watu binafsi. Ninachomaanisha ni kuwa Mabasiri hutuamlia tabia nzuri ni ipi hasa na nani atakayegharamia tabia mbovu. Kwa hakika ,ni tabia nzuri inayopaswa kugharamia tabia mbovu. Sijui kama inaleta maana, Mary Jane? Haidhuru ,Watawala hawakosei katika haya maamizi kama tungelivyoishia kufanya sisi." Doobie alisita kumeza tembe kadhaa nyekundu. Maneno yake yalikuwa yameanza kukokota. "Inachekesha jinsi ambavyo daima husema 'sisi' ninapowazungumzia wao.Mary Jane, sijui kama ungehitaji tembe hizi kadhaa kutuliza neva zako?"
"Ninashukuru hata hivyo ,sihitaji," alisema kwa fahari. Alimsogezea sanduku changamano la chuma na kuongezea ,"Hivi vitulizi vyangu vizuri vya urujuani hufanya kazi haraka zaidi . Ni vigumu kwangu kuanza siku bila kikombe cha kahawa na kimoja wapo. Chukua kimoja ujaribu ukipenda . Ndicho kinachopendekezwa kwenye maagizo ya kikemia waleo."
Jonathan aliwatafakari wanasiasa wote aliowahi kukutana nao hadi sasa. "Kweli Mabasiri wana busara vya kutosha kuwaelekeza watu kwenye tabia ifaayo?"
"Sharti awepo mtu wa kufanya hivyo!" aliboboja Doobie, huku akinununika kidogo kitini mwake . Alipiga funda lingine la wiski ili kusafisha mdomo wake uliojaa keki na tembe za urujuani, kisha akamkodolea macho Jonathan. "Watu wasipokuwa na tabia ifaayo, basi hatutakosa kuwafundisha hao malofa uwajibikaji wafikapo korokoroni! "Doobie alianza kuwasihi wenzake wajiunge naye katika dumu ya vinywaji.
"La shukrani ,"akasema Jonathan. "Una maana gani kwa kusema uwajibikaji?"
Mary Jane alisogea kumwaga wiski kidogo kwenye kahawa yake kabla ya kuongeza tena sukari na mtindi zaidi. "Sijui jinsi ya….haidhuru ,hebu eleza wewe Doobie."
"Hmmmm. Ngoja nifikirie ."Doobie alisogeza kiti chake nyuma kidogo kisha akaendelea kuvuta sigara yake . Angeweza kuonekana mwenye busara kama si kuelekea kuyumbayumba. Alipojidhibiti tena , akasema, "Uwajibikaji sharti uwe ni kukubali matokeo ya matendo yako mwenyewe . Naam , ndivyo hasa! Ndivyo njia pekee ya kukua , ushafahamu, kujifunza." Moshi uliomzunguka doobie uliendelea kujenga wingu zito huku akivuta sigara yake haraka haraka, akiaribu kufikiria kwa makini zaidi kuhusu uwajibikaji.
"La ,la "alikatiza Mary Jane . "Huo ni ubinafsi mkubwa . Uwajibikaji ni kuwashughulikia wengine . Mhm- tukiwakinga dhidi ya Madhara, tukiwalinda dhidi yao wenyewe."
Jonathan aliuliza, "Ni lipi lililo na ubinafsi zaidi? Kujiangalia mwenyewe au kuwashugulikia wengine?"
"Kunayo njia moja tu ya kupata huo ukweli ."aliamua Doobie . Aliinuka kutoka kitini pake kusimama wima kabisa huku akikigota sakafuni. "Bora tumpeleke kwa mdadisi mkuu. Kama kuna mtu awezaye kueleza uwajibikaji, ni yeye!"
© Copyright 2005,
Inter Region Economic Network, Nairobi, Kenya, All Rights Reserved.