Chapter 35 - SURA YA THELATHINI NA TANO
MDADISI MKUU
Vivuli vilikuwa vimerefuka tayari huku alasiri ikiingia.Jonathan pamoja na wenzake wawili , Mary Jane na Doobie walitokeza uchochoroni . Kwenye sehemu fulani ya barabara, Mise alijiunga naye tena walipokuwa wakitembea kuelekea kwenye bustani moja yenye nyasi zilizonawiri. Watu waliingia pale bustanini kutoka pande zote, baadhi kwa miguu na wengine wakienda kwa magoti, wakajikusanya kukizunguka kilima kidogo kilichokuwa katikati.
"Sawasawa, " alisema Mary Jane, "hatujachelewa. Hivi punde pahali hapa patajaa wafuasi tele wakija kuusikiza ukweli wa mdadisi mkuu. Maswali yenu yote yatajibiwa ." Waliketi chini kwenye kirundo cha nyasi. Kwa kulemewa na chakula na wiski, Doobie aliegemea mara moja na kuzimika. Mary Jane alitulia kimya.Aila ziliketi chini ya miti na kungojea kwa hamu.
Jonathan alimsikia mwanamume mmoja nyuma yake akisema, "Shabash ! sikumtaraji mdadisi mkuu leo."
Mwenzake alijibu , "Hapana amtarajiaye mdadisi mkuu , ambaye vipengee vyake vikuu vya kuhibitisha ni…."
Hapo, mwanamume mmoja mwembamba kweli kweli mwenye kuvalia mavazi meusi ya kuvutia alijitoma katikati mwa ile halaiki. Pole pole macho yake yalipita kwenye nyuso zilizokuwa zikimtizama .Minong'ono ya ule umati ilikatika na wote wakanyamaza.
Sauti kali ya yule mtu ilisikika kama kwamba ilitoka ardhini kwenyewe na ilimwingia Jonathan mwilini kote. "Amani ni vita! Busara na ujuhali! Uhuru ni utumwa!"
Jonathan alitupa jicho huku na huku kwenye ule umati uliojaa hofu. Mdadisi Mkuu alikuwa ameiteka hadhira yake kabisa. Lakini hata hivyo kijana Jonathan alitoka , "Mbona unasema kuwa 'uhuru ni utumwa'?"
Akiwa ameshangazwa na utundu wa Jonathan, Mary Jane alimsuta kwa kumnong'oneza , "Nilisema maswali yako yatajibiwa -sikusema umwulize maswali."
Mdadisi Mkuu alimtizama kwa jicho kali mtahini wake mdogo. Hakuna mtu aliyewahi kuwa na ujasiri wa kumbisha hapo kabla . Bustani yote ilinyamaa kimya isipokuwa tu parakacha parakacha ya upepo kwenye majani . Kisha mdadisi Mkuu alinguruma ,akimngurumia Jonatan kwa upande mmoja na umati kwa upande mmoja,"Uhuru ndio mzigo mkubwa zaidi awezao kubeba mwanadamu." Akinguruma na kuvuma, mtu huyo aliinua mikono yake na kupitanisha viwiko vyake juu ya kichwa chake, "Uhuru ndio mnyororo mzito zaidi kwa yote!"
"Kivipi?" akasisitiza Jonathan ,huku akiishia kuhisi ujasiri wa mgeni asiyejali sana watavyomchukulia wengine.
Mdadisi Mkuu alijongea akasimama mkabala na kisha akasema kwa dhati, "Uhuru ni uzito wa kipekee mabegani mwa wanaume na wanwake kwa sababu huhitaji matumizi ya akili na hiari." Huku akinguruma kwa uchungu na adha, Mdadisi Mkuu alionya , "Hiari zenu wenyewe zitawafanya muwajibikie matendo yenu kila mmoja!" Ule umati ulitetema kwa kuyasikia maneno haya; baadhi walijipiga makofi kwenye masikio kutokana na hofu.
"Unamaanisha nini unaposema 'kuwajibika'?" aliuliza Jonathan kwa sauti imara.
Mdadisi alirudi nyuma hatua moja na akaulegeza uso kwa mtizamo wa kirafiki. Aliinama kung'oa unyasi fulani karibu na mguu wake . "kaka na dada zangu wapendwa , huenda mkakosa kuzielewa hatari ninazozongumzia .Hebu fungeni macho yenu na mjaribu kuyafikiria maisha ya mmea huu mdogo." Sauti yake iliendelea kuwa laini na ikawavutia wasikilizaji wake.
Kila mtu alifunfga yake kabisa na kumakinika , isipokuwa Jonathan . Kihaipnosia ,Mdadisi Mkuu alianza kuufafanulia ule umati pichafulani. "Huu mmea mdogo sio kingine ilakijiti hafifu ,chenye mizizi yake kwenye udongo na kilichobandikwa ardhini . Hakiyawajibikii matendo yake .Matendo yake yote yameamiliwa awali. Ah , raha ilioje kwa kijiti!
"Sausa , wapendwa , hebu mfikirieni myama .panya mdogo mzuri mwenye shughuli nyingi za kutafuta chakula kwenye mimea. Huyu kiumbe mwenye manyoya manyoya hana wajibu wowote kwa matendo yake. Kila panya atendalo huwa limeamuliwa na kuelekezwa awali na maumbile . Ah, maumbile . Mnyama mwenye raha! Hapana mmea wala mnyama alazimikaye kubeba mzigo wowote wa hiari mana hivi vyote havikabiliwi na haja ya kufanya utenzi. Daima havikosei!"
Wachache katika ule umati walinong'ona, "naam, Mdadisi Mkuu , naam, ndivyo ilivyo."
Kiongozi huyo mpendwa alinyooka, akawa mrefu zaidi kwa ghafla,kisha akaendelea, "Fungua macho yako na utizame ulipo!Mwanadamu, anayezingatia adili na uteuzi, aweza kukosea nakwambia! Adili na uteuzi mbaya waweza kukudhuru pamoja na wengineo. Hata ile hali ya kuishi uteuzi itasababisha tabu. Taabu hiyo ni wajibu."
Wale watu walitetema na kujifinyikiza pamoja.Mvulana mmoja aliyekuwa kakaa kando ya Jonathan alipaza sauti ghafla, "Oh ,tafadhali, bwana .Ni vipi tuwezavyo kujikinga na hali hii ya kimaumbile?"
"Hebu twambie jinsi ya kujiondolea huu mzigo mbovu," alisihi mwingine.
"Sio rahisi , lakini kwa pamoja twaweza kulivunjilia mbali hili tisho la kutia hofu." Hatimaye aliongea kwa sauti ya chini kabisa kiasi cha kumbidi Jonathan ainame mbele kidogo ili kumsikia. "Niaminini. Nitakufanyieni maamuzi. Kisha hamtakuwa tna na hatia wala uwajibikaji uletwao na uhuru. Kama mfanya maamuzi, nitajichukulia tabu zote."
Hatimaye Mdadisi alitupa mikono yake juu na kupaza sauti , "Sasa nendeni kila mmoja. Piteni kila barabara na kila kichochoro, mkibisha kila mlango. Tafuteni kura kama nilivyokuelezeni! Ushindi ni wangu huu , mimi mfanya maamuzi wenu kwenye Baraza la Mabasiri!" Na halaiki ilikubali kwa sauti ,ikainuka kwa pamoja kutawanyika kuelekea kila upande. Walisukumana na kupigana kumbo, kila mmoa akiwania kutangulia kufika barabarani.
Jonathan na Mdadisi Mkuu pekee ndio waliobaki -na Doobie aliyekuwa akikoroma taratibu nyasini. Jonathan alibakia kaketi kastaajabu. Alilitazama lile kundi likienda mbio kwa fujo, kisha akamkodolea macho usoni yule mtu mwenye mavazi meusi. Mdadisi alimtizama Jonathan kana kwamba alikuwa akiona maono fulani kwa mbali. Jonathan alikivunja kimya kilichokuwa kimekithiri kwa swali moja zaidi . "Ni wema uliopo katika kukuachia wewe kufanya maamuzi yote?"
"Hamna," Mdadisi alijibu huku akiibirua midomo yake kwa dharau. "wema waweza kuwepo tu iwapo pana uhuru wa kuteua. Wafuasi wangu hupendelea utulivu kuliko wema. Na wewe mwenyewe, bwana mdogo mwenye maswali tele, unapendalea nini? Wacha nikufanyie uteuzi, pia. Kisha maswali yako hayatakuwa na maana."
Kimya kabisa , Jonathan alianza kuondoka pale kwenye bustani palipokuwa pamebaki patupu. Kicheko cha Mdadisi Mkuu kilipaa nyuma yake.
© Copyright 2005,
Inter Region Economic Network, Nairobi, Kenya, All Rights Reserved.