Chapter 36 - SURA YA THELATHINI NA SITA
SHERIA POTEZI
Jonathan alitumaini ulikuwa wakati wa kukutana na Elisa. Alimfikiria mara kwa mara .Aidha , alinuia kumwelezea yote aliyokumbana nayo. Kwa shauku , alichapua miguu.
Akikirejelea kijia alichokijia , Jonathan aliusikia msururu wa watu ukipiga kelele na vigelegele.
Kwenye eneo wazi baada ya JENGO A , JENGO B,na JENGO C, palikuwa pamejengwa jukwaa refu lililozungushiwa kamba.Umati mchangamfu ulipiga kelele ukijongea kabisa mzingo wa jukwaa hilo. Aligundua kuwa kila mmoja katika lile kundi alijifunga mshipi mpana au ukanda mgongoni mwake.
Katikati pa lile jukwaa ,mtu alikuwa akipaza sauti. "Hapa pembeni-uzito wa ratili 256-miezi mitano bingwa wa Mashindano ya Kimataifa ya Wafanyi Kazi- simba marara asiyeshindwa- Karl 'Msagadi Marlow!" Umati ulipagawa.
Upande mmoja, palikuwepo mtu mmoja mwenye kovu usoni aliyekuwa kakaa kwenye meza rege rege, akipitapitia nundo ya karatasi na vitopa vya pesa kwa ustaadi . Mtu huyo alimtizama Jonathan kisha akabweka, "Fanya kisio lako, mwanangu. Zimesalia sekunde chache duru ifuatayo ianze."
Mwanamke mmoja mzee ,alimpiga kumbo Jonathan na kuzipiga hati kadhaa za fedha mezani. "Hamsini kwa bingwa , haraka ! "aliagiza .
"Sawa sawa,bibie," akasema karani. Alipiga muhuri kwenye tiketi, akararua nakala kutoka kwenye daftari na kumpa.
Mtangazaji alipita jukwaani akapaza sauti, "Na upande ule Mwingine- ama kwa kweli changamoto- na uzito wa ratili 270 za misuli mitupu- kilimgegeda -konzi…."
Akimgeukia yule mtu pale mezani,Jonathan aliuliza ,"Kuna vurugu la namna fulani hapa? Je , Patakuwepo pigano?"
"Ama kweli pigano ,lakini sio vurugu la namna yoyote ," alisema mtu huyo huku akitabasamu. "Halijawahi kuwa zuri hivi." Kengele iligonga na yule jamaa akautangaza umati."Mwisho wa Masikio!" Wanaume wote wawili waliruka wakasonga mbele huku wakitupa ngumi na kila mmoja akijitahidi kukwepa masumbwi ya mwenziwe.
"Sikiza , kijana, hapana lolote la kukutia shaka," akamtuliza yule karani. "Mshindi na mshindwa wote huondoka na kibunda cha pesa.
Mmoja wa wapiganaji wale alianguka sakafuni ghafla, baada ya kulimwa ngumi nzito mgongoni. Umati ulinguruma kwa shauku, wakati karani naye akihesabu pesa na kuzitia kwenye kasha.
"Wote wawili wanajishindia zawadi?" aliuliza Jonathan.
"…mia tano, mia sita…..kweli," akasema yule jamaa ,akisita kidogo kuhesabu. "Hili ndilo pigano maarufu kabisa kisiwani. Wakati mwingine mshindwa hujipa zaidi ya mshindi…. Mia saba, mia nane….."
Macho ya Jonatan yalitanuka .
"Mtu yeyote aweza kutajirika kwa kushindwa?
"Sio mtu yeyote .Wapasa kuwa na kazi nzuri ili kushindwa kabla ya kukabiliana na bingwa."
Sielewi," akasema Jonathan. "Mfanyakazi anawezaje kuhatarisha kazi yake ili kuvunjwavunjwa na bingwa?" Kengele ilitimiza duru nyingine na umati ukatulia.
"……mia tisa, elfu. Ndivyo ilivyo hasa. Kwani hujawahi kuisikia sheria ya ushindwa?" aliuliza jamaa huyo huku akigongagonga zile noti kutengeza vitopa vya kuvutia. "Sheria ya ushindwa inaondoa hatari. Mshindwa hajali chochote . Si hundi ya malipo, si gharama ya matibabu ,si nini."
"Mbona asijali?" alisaili Jonathan.
"Baada ya pigano , mshindwa huwa hafanyi kazi tena na mwajiri wake hulipa kila kitu."
Jonathan alinyosha shingo yake juu ya ule umati na kumwona mtu mmoja kajilaza pambazoni akipanguswa uso na mhudumu- jukwaa.
"Mwajiri anahusika vipi na pigano hili?"
"Si kwa vyovyote," akasema jamaa.
"Mfanya kazi hudai kuwa alijeruhiwa akiwa kazini na kuwa hawezi kuendelea kufanya kazi ,waelewa?"
"Mh mh," akajibu Jonathan akijitahidi kabisa kuelewa . "Hivyo ni kusema mshindwa aweza kuongopa ili apate pesa hizo?"
"Imewahi kutokea hivyo," alisema mtu yule huku akikoneza jicho kijanja. "Chunga usinielewe nisivyo, sio wafanya kazi wote wanaoweza kuongopa ili kufaidi mpango huu wa kuvutia kwa miaka kadhaa. Lakini sheria ya ushindwa huwazawadi wanaofanya hivyo.Hivyo basi kila siku twapata wachezaji wapya.Ni mpango murua kabisa . Kwa muda wa miaka arobaine iliyopita hapana yeyote aliyewahi kukataliwa dai."
Jonathan sasa alielewa mbona kila mtu alivalia ile Mishipi na Kanda. Baraza nalo linalohusikaje?"
Yule mtu aliangua kicheko, "Watatupa msaada wa aina yoyote ile -nasi tunatii Siku ya Uchaguzi."
"Polisi !" alipiga kelele mmoja wa watu katika umati . Wengi walishuka wakapiga magoti mara moja. Yule karani alifunga kasha lake la pesa haraka haraka,akakunja meza na kuanza kupiga uluzi bila wasiwasi wowote.
Jonathan alichunguza barabara kuona kama palikuwepo dalili za polisi. Alipowaona Afisa Stuart na polisi wengine wakilikaribia jukwaa, Jonathan aliuliza, "Taabu gani ? Au hilo pigano si halali?"
"La hasha " alijibu yule jamaa kwa utulivu. "Polisi hufurahia kinyang'anyiro kizuri kama tu jamaa mwingine yeyote. Ni uchezaji kamari wa kibinafsi ndio haramu.Baraza la Mabasiri linasema kuwa michezo ya kubahatisha ni ukiukaji adili-isipokuwa kwenye Tamasha ya Nia Maalumu ambako wanapata sehemu ya zawadi zinazoshindwa. Tweed naye, kwa upande wake ,anaonelea ingekuwa bora tukiyahifadhi masikio yetu hadi kwenye uchaguzi."
Hapo hapo kengele ililia na umati ukashangilia. Jonathan alihisi mtu akimgusa begani na akageuka. Alikuwa Alisa ,"Alitabasamu na kusema, "Paka wako yu wapi?"
© Copyright 2005,
Inter Region Economic Network, Nairobi, Kenya, All Rights Reserved.