Inter Region Economic Network, Nairobi, Kenya  

Home
About IREN
Media & Press
Projects
News & Newsletters
Articles
Events
Resources
Speeches and Publications
Student Outreach
Contact IREN

Chapter 1 - SURA YA KWANZA



DHORUBA KALI

Katika mji fulani wenye joto kwenye ukingo wa bahari, kuliishi kijana wa kiume aliyeitwa Jonathan Gullible- muda mwingi kabla mji huu haujawa na wacheza sinema walioyapeleka magari yaliyoweza kugeuzwageuzwa mara saloni mara piki-apu. Yeye hakuwa na umuhimu wowote kwa ye yote isipokuwa kwa wazazi wake, ambao walimuona kuwa mwerevu, mwaminifu, na mwenye maungo ya kimichezo ----- toka utosini pa kichwa chake kilichokuwa na matimutimu ya nywele za hudhurungi ya mchanga hadi chini ya nyayo zake zilizokithiri kwa ukubwa. Wao walifanya kazi kwa bidii kwa duka dogo la kuuza vitu kama vile mishumaa, sabuni, mafuta na kadhalika kwenye barabara kuu ya mji uliokuwa makao ya jamii iliyojishughulisha na uvuvi. Ulikuwa na watu kiasi waliofanya kazi kwa bidii, baadhi wazuri baadhi wabaya, na wengi wao walikuwa ni wa kadiri tu.

Pale ambapo Jonathan angekuwa hafanyi kazi za kawaida nyumbani au kutumwa kuleta bidhaa za ghala la familia yao, angekuwa anaipeleka mashua yake isiyo laini kupitia kwa mlangobahari mwembamba wa bandari ya mashua ndogondogo ili kujistarehesha. Kama vijana wengine wengi walioishi katika eneo hili katika miaka yao ya mwanzo mwanzo, maisha kwa Jonathan yalikuwa chapwa na aliwaona watu katika ujirani wake kuwa si wabunifu. Alitaka sana kuona meli ya ajabu au nyoka mkubwa wa baharini pale alipofanya safari zake fupi fupi kupitia mlangobahari. Alitegemea kuwa labda angeweza kuipata meli ya maharamia ili aweze kuabiri zile bahari saba akiwa ni mmoja katika mabaharia. Au, labda, angekutana na mwinda - nyangumi akizungukazunguka kutafuta mawindo manono na kisha amshirikishe katika shughuli zake. Hata hivyo, nyingi ya safari zake ziliisha pale ambapo tumbo lake liliuma kwa njaa au umio wake ulipowashwa na kiu na kile kilichoishughulisha nafsi yake kikawa ni chakula cha jioni.

Siku moja safi wakati wa msimu wa springi, wakati ambapo hewa ilikuwa kaufu kama shuka iliyokaushwa, bahari ilionekana nzuri sana kiasi cha Jonathan kufikiri kuwa palikuwa hapana haja ya kubeba mankuli ya mchana na vifaa vya kuvulia kwenye meli yake ndogo kabla hajaenda kuivinjari bahari. Alipoiendesha meli yake ndogo kupitia eneo la mawe mawe la jumba la watunza - bandari, alijihisi mwenye uhuru kama vile lile jitai aliloliona likipaa juu ya milima ya mwambao. Huku mgongo wake ukiwa wapigwa na upepo - nyiri wa bahari, Jonathan hakutambua mawingu meusi ya dhoruba yaliyokuwa yakijikusanya kwenye upeo wake wa macho.

Ni muda mfupi tu uliopita ambapo Jonathan alikuwa ameanza kuabiri nje ya lango la bandari, lakini alikuwa akijiwa na imani ya ndani kwa ndani kila uchao. Hewa ilipoanza kuvuma kwa sana, hakuonyesha wasiwasi mpaka akajikuta amechelewa kuikabili. Alijikuta akipigana nayo huku dhoruba kali ikimwangaisha. Mashua yake ilipeperushwa kwenye mawimbi kiasi kwamba ungedhani ni kifuniko ndani ya besini lenye kujaa maji. Kila juhudi alizozifanya kukabili chombo chake hazikufaulu; zilikuwa ni bure ikilinganishwa na hewa nzito. Hatimaye, aliiangukia sakafu ya mashua, akiwa amezishikilia pande zake na kuomba kuwa asizame. Usiku kucha na mchana kutwa Jonathan aliukabili msukosuko uliotisha.

Hatimaye dhoruba ilipoisha, mashua yake ilikuwa imeharibika, boriti yake ikawa imevunjika, tanga zikawa zimeraruka, na ikawa imepinda kulia. Japo bahari ilitulizana, ukungu mzito ulihisika bado, ukazuia utendakazi wake na kumkosesha kuona. Baada ya kutokujua la kufanya kwa muda wa siku nyingi, hazina yake ya maji iliisha na akabidiika kuilowesha midomo yake kwa majimaji yaliyodondoka kutoka nyuzi za chandalua. Kisha ukungu ukaisha na Jonathan akaweza kuona kwa mbali ukingo wa kisiwa. Aliposogea karibu na kisiwa hicho, alikumbana na ardhi ngeni iliyotokana na fuko zenye changarawe pamoja na vilima vilivyokuwa na misitu mizito.

Mawimbi yalimbeba hadi kwenye miamba isiyo na kina. Aliachana na shughuli yake ya kuabiri kwa mashua pale ambapo Jonathan alipiga mbizi harakaharaka hadi kwenye ukingo wa bahari. Hapo, mara akapata na kula kwa pupa mapera ya rangi nyekundu - nyeupe, ndizi zilizoiva pamoja na matunda mengine matamu yaliyojimelea baada ya ufuko huu mwembamba wa changarawe katika nyevunyevu ya tropiki. Mara tu alipopata nguvu tena, Jonathan alijihisi kuwa pweke lakini akashukuru kwa kuwa bado hai. Alifurahishwa hasa na kule kuingia kwake katika mkasa huu pasi na kupenda. Mara akaanza safari kwenye ufuko huo uliokuwa na changarawe nyeupe ili kujionea zaidi yaliyokuwemo kwenye ardhi hii mpya na ya kushangaza.





© Copyright 2005,
Inter Region Economic Network, Nairobi, Kenya, All Rights Reserved.