Chapter 5 - SURA YA TANO
MISHUMAA NA MAKOTI
Jonathan aliandamana na mama huyu, aliyekuwa akikata tamaa, pamoja na mwanaye kwa mwendo wa maili kadhaa kutelemka barabarani kuelekea nyumbani kwa jamaa zake. Walimshukuru kwa wema wake mwingi na kumwomba akae nao. Kwa kutazama nyumba ile mara moja tu alitambua kuwa haingeweza kuwatosheleza wanafamilia wote, na kwa hivyo aliomba kuondoka ambapo aliendelea na safari yake.
Barabara hiyo ilimpeleka mtoni ambapo alipata daraja iliyounganisha sehemu hiyo na mji uliokuwa kwenye kuta upande ule mwingine. Ile daraja nyembamba ilikuwa ni mgao wa lazima. Kwenye upande wa kulia wa daraja, kulikuwa na dokezo lililoonyesha mjini na lilisoma, "INGIA JIJI LA STULTA, KISIWA CHA KORUMPO." Ule upande mwingine wa mgao, kulikuwa na dokezo jingine lililosoma, "KUTOKA TU, USIPAINGILIE." Na wala hiyo siyo sura ya pekee ya mji huo iliyokuwa ya ajabu. Ili kuvuka na kuingia mjini pale, ilibidi mtu apande juu ya vizuizi vilivyokuwa na ncha kali. Mikusanyo ya miamba kali pamoja na mawe makubwa vilizuia lango lote la daraja. Wasafiri kadhaa walikuwa wameangusha vifurushi vyao ama njiani au ndani ya mto badala ya kuvitupa juu ya kile kizuizi chenye mawemawe. Wengine, hususan wazee, waliamua tu kurudi walikokuwa wakitoka.
Nyuma ya msafiri mmoja mnyonge, Jonathan aligundua yule paka aliyezoeleka mwenye rangi ya milia ya manjano aliye na sikio lililoraruka kulia akiwa yuanusia na kukwakura furushi lililokuwa limetupwa. Huku akiwa bado anamwangalia, yule paka alichopoa kipande cha nyama kilichokauka kutoka kwa lile bunda liloraruka.
Kinyume na mahali pa kuingilia, mahali pa kutokea upande mwingine wa daraja palikuwa laini na shwari. Wafanyabiashara waliobeba bidhaa kutoka mjini walitoka kwa urahisi. Jonathan alistaajabu, "Kwa nini kuingia mahali hapa ni matanga hali kupatoka ni harusi?"
Jonathan aliparamia ule upande wa daraja ulio wa kuingilia mjini, akiteleza kwenye msingi usio laini huku akijiburuta kukwea ile miamba. Hatimaye alipafikia mahali palipokuwa na malango mawili mazito yaliyokuwa yametengenezwa kwa mbao na ambayo yalikuwa yamefunguliwa wazi kumruhusu kuingia kupitia ukuta muhimu wa mji. Watu walioendesha farasi, watu waliobeba masanduku na vifurushi, na watu walioendesha aina mbalimbali za makochi na rukwama walipitapita mabarabara ya mle. Jonathan aliyanyosha mabega yake, akalitoa vumbi kwenye shati na suruali zake raruraru halafu akatembea taratibu kupitia langoni. Yule paka alijipenyeza ndani nyuma yake.
Mara tu alipoingia ndani, alimkuta mwanamke aliyekuwa ameshika karatasi iliyokunjwa akiwa ameketi nyuma ya meza iliyokuwa imefunikwa vinishani vilivyong'ara. "Tafadhali", aliomba yule mwanamke, akiwa yuatabasamu sana na huku akitaka kumdundika Jonathan moja ya vinishani hivyo mfuko wa shati lake, "je, utanitilia kidole lalama yangu?"
"Naam, sijui", aligugumiza Jonathan. "Sijui kama unaweza kuniongoza kufika katikati mwa mji?" Yule mke alimchunguza kwa jicho la tuhuma. "We hujui mji?"
Jonathan alisita, kwa kutambua ile toni kali iliyotoka kwenye sauti yake. Kisha ghafula akasema, "Na kwenye hii lalama yako, ni wapi nitakapotia sahihi?"
Yule mwanamke alitabasamu tena. "Tia sahihi chini ya jina la mwisho, hapa hivi. Unawasaidia watu wengi sana kwa hii."
Jonathan alipandisha pandisha mabega yake na kisha akiichukua kalamu yake. Alimsikitikia kwa jinsi ambavyo alikaa akitokwa na majasho kote kote huku akiwa kavalia magwanda mazito kwenye mchana mwema uliochomoza jua. "Je, hii lalama inahusu nini?" Jonathan aliomba kujua.
Alifumbata mikono yake mbele yake kana kwamba alijitayarisha kuimba wimbo wa mtu mmoja peke yake. "Hii ni lalala ya kulinda kazi ya viwanda. Wewe ungependa pawepo kazi na viwanda, au siyo?" alimrai.
"Hasa", alijibu Jonathan, huku akimkumbuka yule mama mbunifu aliyeshikwa kwa kuhatarisha kazi za wakata miti. Jambo la mwisho ambalo angeweza kufanya ni kuonyesha kuwa hazijali kazi za watu wengine.
"Je, hii lalama atasaidiaje?" aliuliza Jonathan huku akiliandika jina lake vibaya sana kiasi cha labda kutokuweza kusomeka na ye yote.
"Baraza letu la Watawala huvilinda viwanda vyetu dhidi ya mazao yatokayo nje ya mji wetu. Kama unavyoweza kuona, tumepiga hatua kwa upande wa daraja lakini kunayo mengi yafaayo kutendwa. Endapo watu wa kutosha wataitia sahihi lalama hii yangu, Watawala wameahidi kupiga marufuku bidhaa za kigeni zinazohasiri kiwanda changu." "Kiwanda chako ni kipi?" Jonathan aliuliza.
Yule mama alitangaza kwa majivuno, "Mimi nawakilisha watengenezaji wa mishumaa na makoti. Lalama hii yataka jua lipigwe marufuku."
"Jua?", Jonathan alisema kwa mshangao. "Vipi, ah, mbona jua lipigwe marufuku?"
Alimtazama Jonathan kwa njia ya kujitetea. "Najua kuwa yaonekana kinyume kiasi, lakini tazama - jua huhasiri watengeza mishumaa na makoti. Watu hawanunui mishumaa na makoti wakiwa na joto na pia mwanga. Kusema kweli jua ni chanzo rahisi sana cha mwanga wa kigeni pamoja na joto. Naam, hali hii haiwezi kamwe kuvumiliwa!"
"Lakini mwanga na joto kutoka kwa jua ni bure", Jonathan alipinga.
Yule mama alionekana aliyeudhika na akalalamika kwa kusema, "Hilo ndilo tatizo, si waliona?" Huku akitoa karatasi ndogo na penseli, alijaribu kumchorea ishara chache. "Kwa mujibu wa hesabu zangu, gharama ya chini ya bidhaa hizi za kigeni hupunguza uwezekano wa uajiri pamoja na ijara kwa asilimia isiyopungua 50 --- yaani, katika viwanda ninavyowakilisha. Ushuru mkubwa kwa madirisha, au labda makatazo ya moja kwa moja, waweza kuiboresha hali hii vema."
Jonathan aliitia chini lalama ya yule mama. "Lakini endapo watu watalipia mwanga na joto, watakuwa na hela chache za kugharamia huduma nyingine - vifaa kama nyama au vinywaji au mkate."
"Mimi siwakilishi wenye maduka ya nyama, au wanaogema, au waoka mikate", yule mwanamke alisema ghafula. Kwa kutambua kuwa Jonathan alikuwa kabadilisha nia, alimnyang'anya ile lalama. "Yamkinika wazi kuwa nia yako imo hasa katika kutetea bidhaa za ulaji kuliko ilivyo katika uhifadhi wa kazi na uwekezaji wa kibiashara ulio mathubuti. Nakutakia siku njema", alisema, huku akiyahitimisha mawasiliano ghafula.
Jonathan aliondoka pale mezani. "Kulipiga marufuku jua?" aliwaza. "Fikira zilizoje hizi! Mwanzo vishoka na chakula, halafu jua. Je, ni kipi watakacho kifikiria halafu?"
© Copyright 2005,
Inter Region Economic Network, Nairobi, Kenya, All Rights Reserved.