Chapter 7 - SURA YA SABA
MIPANGO ILIYOPANGWA VEMA ZAIDI
Nyumba chakavu za mbao zilizo za orofa mbili au tatu na zilizokuwa kwenye safu zilijipanga kando kando ya barabara za mji huo. Jonathan aligundua kuwa kulikuwa na nyumba moja kubwa yenye fahari iliyojitenga, na ambayo ilijengwa kwenye bustani kubwa ya kijani. Ilionekana kujengwa madhubuti, ikawa imerembeshwa kwa viunzi vya fito na vibao, na kuta zake nyeupe kupakwa rangi karibuni.
Akiwa amestaajabu, Jonathan aliisogea nyumba ile ambapo alipata kikosi cha watu waliobeba magogo mazito na ambayo kwayo waliupiga upande wa nyuma wa nyumba kwa kujaribu kuiangusha. Hawakuwa na moyo sana na kwa hivyo waliifanya kazi hii pole pole mno. Katika ujirani wao, kulikuwa na mama mwenye heshima zake aliyekuwa na mvi kichwani akiwa kasimama huku mikono yake imekunjwa, akionyesha kuwa hakufurahia yaliyokuwa yakitendeka. Alilia kwa sauti ya juu wakati ambapo kipande cha ukuta kilianguka.
Jonathan alimwendea na kumwuliza, "Ile nyumba yaonekana imejengwa vizuri!" Ni nani mwenyewe?" Hilo ni swali zuri!" yule mama alijibu haraka. "Nilifikiri kwamba niliimiliki nyumba hiyo."
"Ulifikiri uliimiliki? Bila shaka unajua kama kweli unamiliki nyumba", alisema Jonathan.
Ardhi ilitetema wakati ambapo ukuta wa nyuma wote uliangushwa ndani. Mama yule aliyakodoa macho kwa huzuni alipoona wingu la vumbi likivuma kutoka kwa vifusi vya nyumba yake. "Si rahisi vile", mama yule alipaza sauti iliyopiku yale makelele. "Umiliki unakwenda na usimamizi, au siyo? Lakini ni nani anayesimamia nyumba hii? Watawala wanasimamia kila kitu - kwa hivyo ni wao wanaomiliki nyumba hii hasa, japo niliijenga na kulipia kila ubao na msumari."
Huku akiwa yuapandwa na hasira zaidi, alitembea na kupafikia mahali ambapo muda mchache tu uliopita kulikuwa kumesimama ukuta na kisha akaikwanua karatasi kwenye mhimili mmoja uliokuwa umesalia. "Unaangalia notisi hii?" Aliikunjakunja, akaitupa chini na kisha kuikanyaga. "Maafisa wananiambia kile cha kujenga, vile nitajenga, wakati wa kujenga, na malighafi ya kujengea. Kisha sasa wananiambia kuwa wanaibomoa nyumba yenyewe. Je, hali hiyo yaelekea kudokeza kuwa mimi naimiliki mali husika?"
"Naam", alisema Jonathan kizembe, "si uliishi ndani yake?"
"Niliishi tu pale ambapo niliendelea kulipa ushuru wa mali. Lau kama sikulipia, maafisa wangekuwa walinifukuzilia mbali haraka kuliko pigo la ukope!" Yule mama aliendelea kukasirika na akafoka, "Hapana ye yote anayemiliki cho chote. Ni kukodesha tu kutoka kwa Baraza kwa kuwalipa kodi."
"Je, hukulipa kodi?", Jonathan aliuliza.
"Bila shaka nililipa ushuru huu uliolaaniwa!" yule mama alijibu kwa kupiga makelele hasa. "Lakini hawakutosheka. Watawala walisema kuwa mpango wangu wa nyumba haukulandana na wao --- mpango mkuu wa "wamilikaji wenyewe", waliniambia. Walisema kuwa nyumba yangu haikufaa --- kisha wakanipa hela fulani kufidia kile walichofikiri iligharimu. Sasa hivi wanaibomoa ili pawe na bustani. Bustani hii itakuwa na mnara wa ukumbusho katikati ulio mzuri na mkubwa ---- mnara ulio wa mmoja wao."
"Nini basi? Si ulilipwa kwa nyumba yako?" Jonathan alisema. Lakini alifikiri tena na kisha akauliza, "Hukutosheka?"
Alimwangalia kwa jicho la upande. "Lau kama ningekuwa nime tosheka wasingehitaji polisi kuja kuniharakisha, au siyo? Kuhusu hela walizonipa! Zilichukuliwa kutoka kwa jirani zangu. Je, ni nani atakayewalipa? Watawala hawawezi kuwalipa!"
Jonathan alikitikisa kichwa chake kwa masikitiko. "Je, ulisema kuwa mambo haya yote yalikuwa ni sehemu ya mpango mkuu?"
"Ha! Mpango mkuu!" mama yule alisema kwa kinaya! "Huo ni mpango wa mtu aliye na nguvu za kisiasa. Endapo nitaingia siasani basi itakuwa kwamba nitalazimishia watu mipango yangu. Hivyo nitaiba nyumba badala ya kuzijenga. Ni rahisi sana!"
"Lakini mnahitaji ramani ili kujenga mji uliojengwa vema", alisema Jonathan kwa matumaini. Alijaribu kutafuta maelezo yenye mantiki kuhusu mkasa wa yule mama. "Je, si nyingi mmelipa Baraza jukumu la kujitokeza na ramani kama hizi?"
Aliupunga mkono wake kwa kuelekeza kwenye zile nyumba zilizo kwenye safu. "Nenda kajionee. Ramani mbovu zaidi ni zile chache ambazo majengo yake hukamilishwa ---- duni, ghali, na mbovu."
Huku akimgeukia Jonathan, alimwangalia usoni moja kwa moja. "Wazia hili, walijenga uwanja wa michezo ambapo kila watu tisa miongoni mwa kumi hawangeweza kuuona uwanja. Kwa sababu ya kazi yao duni, walibidiika kuukarabati uwanja husika na ukagharimu mara - dufu ya gharama ya mwanzo. Nao ukumbi wao mkuu wa mikutano unaweza kutumiwa tu na wageni na wala si walipa - kodi waliogharamia ujenzi wake. Mipango hii yote ilifanywa na nani? Watawala. Wao huyapamba majina yao kwa rangi nyingi kwenye mawe na ni marafiki zao wapewao kantarasi hizi nzito." Huku mama huyu akimdukuadukua Jonathan kifuani kwa kidole chake, alisema "Ni mipango ya kipumbavu pekee inayowalazimishiwa watu. Mimi sidhamini ulazima!" Kwa ghadhabu, alilitazama jumba lake kwa hasira. Huu si mwisho wangu!"
© Copyright 2005,
Inter Region Economic Network, Nairobi, Kenya, All Rights Reserved.