Inter Region Economic Network, Nairobi, Kenya  

Home
About IREN
Media & Press
Projects
News & Newsletters
Articles
Events
Resources
Speeches and Publications
Student Outreach
Contact IREN

Chapter 8 - SURA YA NANE



BUSTANI MBILI ZA WANYAMA

Akiendelea na safari yake, Jonathan alifadhaishwa na sheria za kisiwa hiki chenye mashaka. Kwa kweli watu wawezaje kutumikiziwa sheria ambazo haziwapendezi? Haikosi kuna sababu nzuri. Ardhi hii ilionekana yenye kijani sana huku hewa yake nayo ikiwa laini na yenye joto----- hii yafaa kuwa ni paradiso. Jonathan alipunguza mwendo wake wa kasi huku akitembea mjini.

Aliifikia barabara iliyowamba na iliyokuwa na nyua za chuma madhubuti pande zote mbili. Nyuma ya ua kulia kulikuwa na wanyama wa ajabu wenye vimo na sura mbalimbali ------ Simba marara, Punda - milia, tumbili ---- wengi tu. Nyuma ya ile ua nyingine iliyokuwa kushoto kulitembeatembea dazani kadhaa za waume na wake, wote wakiwa wamejivalia mashati na suruali za rangi nyeusi yenye milia mieupe. Makundi haya mawili yaliangaliana mkabala wa barabara na yalionekana ya kuchekesha. Alimwona mume mmoja akiwa kajivalia sare nyeusi huku akizungusha rungu kubwa. Jonathan alimsongea huyu mlinzi aliyekuwa akitembeatembea katikati ya milango ya nyua hizi iliyokuwa imefungwa.

Jonathan aliuliza kwa unyenyekevu, "Hizi nyua ni za nini?"

Huku akifuatanisha mzunguko wa rungu na mwendo wake vema, yule mlinzi alijibu kwa maringo, "Moja yazunguka bustani yetu ya wanyama."

"Oh", alisema Jonathan huku akiwa amekodolea macho kikundi cha wanyama wenye hasira na waliokuwa na mikia mizito iliyokuwa ikirushwarushwa pale penye kuta za kizimba chao.

Mlinzi huyu, kwa kuwa na uzoefu wa kuwaongoza watoto wa pale, aliendelea kumhadhiria Jonathan "Je, umeona sampli nzuri za wanyama pale?" Alidokeza upande wa kulia wa barabara. "Tunawaletewa kutoka kote ulimwenguni. Ua hilo huwaweka wanyama hawa salama ili watu waweze kuwasoma. Unaona, haiwezekani kuwaachilia wanyama wa kigeni kurandaranda huku wakiidhuru jamii."

"Waa!" Jonathan alishangaa. "Haikosi imekugharimu hela nyingi kuwaleta wanyama kutoka ulimwenguni kote na kisha kuwatunza hapa."

Yule mlinzi alimtabasamia Jonathan huku akitikisa kichwa chake taratibu. "Oh, mimi silipii hii bustani ya wanyama. Kila aliye mkazi wa Korampo hulipa kodi ya hifadhi ya wanyama."

"Kila mtu?" Jonathan aliuliza, huku urazini wake ukimwelekeza katika kujitafutatafuta katika mifuko yake iliyokuwa tupu.

"Ndio, kuna baadhi ya watu ambao hukwepa majukumu yao. Wananchi walegevu kama hawa husema hawana moyo katika mambo yahusuyo hifadhi za wanyama. Wengine nao hukataa kwa sababu wana imani kuwa wanyama sharti wasomwe wakiwa katika eneo lao asilia."

Yule mlinzi alipinduka ili kutazama ua uliokuwa upande wa kushoto wa barabara, huku akiwa yuabisha lile lango zito la chuma kwa matumizi ya rungu yake. "Wananchi wanapokataa kulipa ushuru wa bustani ya wanyama, tunawaweka hapa, salama nyuma ya vizuizi hivi. Watu wa ajabu kama hawa waweza kusomwa. Wao pia wanazuiwa kurandaranda na kuidhuru jamii."

Kichwa chake Jonathan kilianza kumsokota kwa kutosadiki yale aliyoyasikia. Huku akilinganisha makundi mawili yaliyokuwa nyuma ya nyua, alistaajabu kama kweli angeweza kugharamia utunzi wa huyu mlinzi pamoja na hizi bustani mbili za wanyama. Alikamata vile vizuizi vya chuma na kuchunguza nyuso zenye kiburi za wafungwa waliojivalia nguo zenye milia. Kisha akauchunguza udhihirisho wenye madharau usoni pa mlinzi aliyeendelea na kizinga mbele na nyuma, huku akizungushazungusha rungu lake.

Yule yule paka wa manjano alikuwa akiingia na kutoka kwenye vizuizi vya hii bustani ya wanyama, akiwa yuazungukazunguka kutafuta mlo. Mlinzi alipiga kizuizi kwa nguvu kwa matumizi ya fimbo yake ambapo yule paka alikimbia kujificha nyuma ya miguu ya Jonathan. Kisha yule paka aliketi chini ili kulamba mguu wake wa mbele na kuwachakura funza nyuma ya sikio lake lililoraruka.

"Natumai unawapenda panya, au siyo, paka? Panya wengi", Jonathan alisema. Huku akimpapasa kichwani, Jonathan alimbatiza rafikiye mpya kwa kusema, "Na 'Mices' vipi? Naam, Mices, umekuwa pande zote mbili za ua. Ni upande upi wa vizuizi walipo wale wanaoweza kudhuru zaidi?"









© Copyright 2005,
Inter Region Economic Network, Nairobi, Kenya, All Rights Reserved.