Inter Region Economic Network, Nairobi, Kenya  

Home
About IREN
Media & Press
Projects
News & Newsletters
Articles
Events
Resources
Speeches and Publications
Student Outreach
Contact IREN

KANUNI SABA ZA SERA YA UMMA ILIYO NZURI

KANUNI SABA ZA SERA YA UMMA ILIYO NZURI
Mhadhara wa kumbukumbu ya James U. Blanchard katika Chumi za Soko Huria -Nairobi, Kenya.

Na Lawrence W. Reed
Rais
Kituo cha Sera ya Umma cha Mackinac Center for Public Policy

Januari 9, 2002

Nawashukuru sana kwa kunipa fursa ya kutoa mhadhara wa kwanza wa umma katika chumi za soko huria nchini Kenya. Ni heshima kubwa kwangu kuwa ni mgeni wa kwanza kuzungumzia Inter Region Economic Network, shirika changa ambalo limejitolea kuchangia ipasavyo katika maendeleo ya kiuchumi nchini Kenya na Afrika Mashariki kwa jumla.

Nafahamu kwamba hakuna muunda sera ambaye hujitokeza na kupendekeza sera mbovu kwa kujua. Sera mbovu yaweza kutokana na kupata habari visivyo, kutokufahamu jinsi ambavyo kanuni za kiuchumi hufanya kazi au katika hali mbaya zaidi kuwa na watu wasiofaa kujitokeza na sera ya umma. Pale Mackinac Center for Public Policy, jukumu letu hasa ni kutafiti na kupendekeza maelezo yajibuyo masuali-leo kuhusu sera, na nilifikiri nilifanya jambo lilo hilo hapa na leo hii. Lakini kwa kuwaza, niliamua kutolizungumzia jambo lolote mahususi bali kukupeni kitu kilicho tofauti kidogo:mkabala mpana na wa juujuu lakini ambao waweza kutumika kwa kila suala. Ningependa sote tufikiri kuhusu tajriba fulani na ujuzi wa kiuchumi. Hizi, kwa maoni yangu, ndizo kanuni za kudumu zifaazo kuunda msingi wa mawazo kuhusu yale tuyafanyayo tukiwa waunda-sera ndani na nje ya serikali.

Ni suala la kiada kwa watu katika taaluma yangu kuziambia hadhira zake kuwa yeye huyakabili masuali yote kwa mtazamo wazi.Bila kujali hiyo ina maana gani kwako, kwangu hiyo haiwezi kuwa sawa na mtazamo mtupu. Tumeweza kujifunza mambo kadhaa katika karne zilizopita. Tunapokubali bila mjadala kuwa jua huchomoza mashariki siyo kuwa tunayo mapendeleo yanaotokana na kutojua.Siyo imani za kinjozi ambazo hutueleza kuwa jamhuri ambayo raia zake wanawakilishwa serikalini ni bora kuliko serikali ya kiimla au ya kifalme.Tunapojifunza kuhusu suala pale Mackinac Center, tunaanza na machukulio ya kimsingi kuwa mali ya kibinafsi na chumi za soko huria ni nzuri kuliko zile zinazopangiwa serikalini.Haya si maoni ya kijuujuu ya mtu mmoja; la, ni moja katika kweli zilizokubalika miongoni mwa watu waliofungua macho pamoja na masikio na ambao kwao busara, mantiki, yaliyokubalika, ithibati, chumi na tajriba humaanisha kitu Fulani.

"Kanuni Saba za Sera ya Umma iliyo Nzuri" ambazo ningependa kujadiliana nanyi leo hii ni mihimili ya uchumi huru. Tunaweza kutokukubaliana kuhusu ni vipi hasa moja au nyingine ya kanuni hizi yaweza kutumikizwa kwa suala fulani sasa, lakini kanuni zenyewe, nadhani ni kweli zilizothibitishwa. Kweli hizi si zangu kiasilia; nimezikusanya tu na kuziweka pamoja . Mbali na ukweli kwamba kanuni hizi ni mihimili ya uchumi huru au kweli za pekee, pia zinajumuisha ujumbe mzuri na mzito. Ninaamini, endepo kila msingi wa kila nchi au jengo la bunge utafunikwa kwa hizi kanuni - na muhimu zaidi, ikiwa kila mbunge atazielewa na kujaribu kuwa mwaminifu kwazo- nchi ya Kenya ingekuwa madhubuti zaidi, huru zaidi, yenye kuendelea zaidi na nchi yenye watu waliotawaliwa vema zaidi.

KANUNI YA KWANZA:Watu huru si sawa, na watu sawa si huru

Kwanza, nitafafanua aina ya 'hali ya usawa' ambao naurejelea katika kauli hii.Sirejelei usawa wa kisheria - kauli kwamba utatolewa hukumu ya kutokuwa na hatia au kuwa na hatia kutegemea kama ulitenda au hukutenda, na kabila, uana, utajiri, imani, jinsia au dini ni vitu ambavyo havina chochote kuhusu usawa. Huu ni msingi muhimu wa utamaduni na ingawa mara kwa mara hatuafikii hali hii, sina shaka kuwa kuna mtu hapa ambaye hatakubaliana na dhana hii.

Hapana, ile 'hali ya usawa' ninayoirejelea ni kuhusu tija na utajiri wa mali- kile tunachochuma na kupata katika maeneo ya sokoni katika biashara, kazi, na ubadilishanaji bidhaa.Ninaongelea usawa wa KIUCHUMI. Hebu na tuigawe kanuni hii ya kwanza katika vipande viwili sawia.

Watu huru si sawa. Pale ambapo watu wako huru kuwa wao, wakiweza kujiamulia hatima zao, wakiweza kujitunza ili kuweza kustawisha maisha yao na yale ya familia zao, matokeo katika maeneo ya sokoni yatakuwa si usawa wa matokea.Kwingi, watu watapata viwango tofauti tofauti vya chumo, kwingi watapata kujikusanyia viwango tofauti tofauti vya utajiri. Huku wengine wakilalamikia ukweli huu na kuzungumzia kwa masikitiko 'mtafaruku baina ya matajiri na masikini' nafikiri pale ambapo watu watakuwa ni wao wenyewe na katika jamii huru ni jambo zuri. Kila mmoja wetu ni kiumbe wa kipekee, ni tofauti katika njia zisizohesabika kutoka kwa kiumbe yeyote yule awe aliye hai au aliye kufa. Mbona sisi tutarajie maingiliano yetu katika maeneo ya sokoni kuzalisha matokeo yayo hayo duniani?

Sisi tu tofauti katika talanta zetu. Kunao wale walio na talanta nyingi zaidi,au wale walio na talanta muhimu zaidi. Baadhi hawatambui talanta zao zenye upeo wa juu mpaka hatimaye maishani mwao, au hata hawatambui kabisa. Magic Johnson ni mchezaji mpira wa vikapu aliye na talanta. Je, itashangaza yeyote kuwa yeye hupata pesa nyingi zaidi kwa kucheza mpira huu wa vikapu kuliko zile ninazoweza kupata mimi? Nchini Kenya, Kipchoge Keino alipata fedha nyingi kutokana na ukimbiaji mbio; ni vipi ambavyo utamshangaza yeyote kuwa alipata pesa nyingi kutokana na ukimbiaji mbio kuliko labda yeyote yule hapa ukumbini alivyowahi kupata?

Isitoshe, tu tofauti kwa jinsi tunavyofanya kazi na tunavyopendelea kufanya kazi. Kuna baadhi wafanyao kazi kwa bidii, kwa muda mrefu, na kwa uzuri zaidi kuliko wengine. Hii ndio iletayo tofauti kubwa katika jinsi watu wenyewe wanavyothamini kile wafanyacho na kiasi cha pesa ambacho wangehiari kukilipia.

Tunatofautiana pia katika akiba zetu. Ningezua mjadala kuwa endepo rais angeamua kutusawazisha katika uchumi na utajiri usiku wa leo, tungekuwa tofauti tofauti tena wakati kama huu hapo kesho kwa kuwa kunao katika sisi ambao wangeweka akiba ilhali kunao ambao wangeutumia.Hizi ndizo sababu tatu, lakini si tatu pekee, zitakazowapelekea watu huru wasiweze kuwa sawa kiuchumi.

Watu sawa si huru, nusu ya pili ya kanuni yangu ya kwanza, inajitokeza kihali halisi.Nionyeshe watu popote pale ulimwenguni ambao ni sawa kiuchumi, na nitakuonyesha watu wasio huru sana. Mbona?

Njia ya pekee ambayo kwayo unaweza kuwa na chembe za nafasi ya kusawazisha mapato na mali kote kwenye jamii ni kutumia bunduki. Yaani utalazimika kutumia maguvu ili kuwafanya watu wawe sawa. Utabidiika kutoa amri, kuua, kunyonga, kutumia mtutu wa bunduki, au kuua kwa kutumia stima, ambapo hali itakuwa vifuatavyo:- "Usifanye vizuri kuliko ulivyofanya hapo awali. Usifanye kazi kwa bidii au kwa uzuri kuliko jirani yako. Usiwe makini zaidi katika kuweka akiba kuliko mwenzako. Usiwe wa kwanza kujitokeza na bidhaa mpya. Usijitokeze na bidhaa au huduma ambayo watu waweza kuitaka zaidi ya jinsi wanavyoweza kutaka ya mkinzani wako".

Amini usiamini usingetaka jamii yenye sheria kama hizi. Khmer Rouge Cambodia mnamo mwisho mwisho mwa miaka ya 1970 iliikaribia hali hii, na matokeo yalikuwa kwamba zaidi ya watu milioni mbili katika jumla ya watu milioni nane walikufa katika muda usiozidi miaka minne. Isipokuwa kwa maulama waliokuwa kwenye ngazi za juu na ambao walikuwa na uwezo mkubwa, watu wa nchi hiyo maskini ambao walifanikiwa kuepuka kifo wakati huo waliishi katika hali inayoweza kufananishwa na ile ya zama za mawe.

Je, kanuni hii ya kwanza ina ujumbe gani? Usibabaishwe na tofauti za mapato baina ya watu pale ambapo watu husika wamefanya bidii kuyapata hayo mapato. Endapo mapato hayo yatokana na vizuizi vya kisiasa vilivyo bandia, viondolewe mbali vizuizi hivyo. Lakini usijaribu kamwe kuwachukua watu wasio sawa na kuwaweka katika lindi moja.Hutafaulu na utajisumbua sana kwa kujaribu kufanya hili.

Kwa mfano, viwango vya ushuru vilivyo vya kupokonya watu haviwafanyi watu kuwa sawa, hata vinawafanya watu wafanyao kazi kwa bidii au wawekezaji kwenda kwingine au kufanya shughuli nyingine huku wale ambao wangefaidika kutokana na shughuli zao wakimaskinishwa.Abraham Lincoln ameambilika kuwa alisema, "Huwezi kumkweza mtu kwa kumlazimisha mwingine kuwa chini".


KANUNI YA PILI:Kile kilicho chako, utakitunza; kile ambacho si cha yeyote au cha kila mtu hakitunzwi.

Kanuni hii yamulika hasa maajabu ya mali ya kibinafsi.Inaelezea kwa kina kuhusu chumi za kijamii ulimwengni kote.

Katika Miliki ya Usovieti, serikali zililipa kipaumbele suala la kupangia pamoja na la serikali kumiliki kila kitu. Serikali hizi zilitaka kupiga marufuku au kupunguza kabisa mali ya kibinafsi kwa sababu zilifikiria kuwa umilikaji mali wa kibinafsi ni wa kujitakia ambapo matokeo yake huwa kinyume. Walisema kuwa pale serikali inaposimamia mambo, raslimali za nchi zingetumika ili kufaidi kila mtu.

Kile ambacho hapo awali kilikuwa ni chakula cha mkulima kikawa ni chakula cha watu ambapo watu waliishia kuwa na njaa. Kile ambacho hapo awali kilikuwa ni kiwanda cha mwekezaji kikawa ni 'kiwanda cha watu"ambapo bidhaa zilizozalishwa zilikuwa duni sana kiasi kwamba hazingeweza kupata masoko ng'ambo. Tunafahamu sasa kuwa ile Miliki ya Usovieti ya kale ilizalisha uchumi ule ule , na mazingira yale yale yaliyotisha.Hilo ndilo funzo linalotokana na majaribio yoyote yale kuhusu ujamaa:huku wafuasi wa ujamaa wakiwa wachangamkia msemo kuwa wahitaji kuvunja mayai ili kuyakaanga,hawayakaangi. Lao linaishia kuwa ni kuvunja mayai tu.[Tazama mtandao www.mackinac.org/articles.asp?ID=2668 ]

Endapo wafikiri kuwa wewe ni hodari katika utunzaji wa mali, nenda kaishi katika nyumba ya mtu mwingine, au peleka gari ya mwingine kwa muda wa mwezi mmoja. Nakuhakikishia kuwa nyumba yao na gari yao ni tofauti na yako. Nchini Kenya, kunao msemo maarufu usemao "mali ya Umma" ulio na maana kuwa "Mali ya kila mtu, kwa hivyo anayefaa kuijali ni nani ?" Madereva wafanyao kazi serikalini si makini kwenye barabara zilizojaa mashimo; matokeo yake ni kwamba magari ya serikali yanaharibika na kuegeshwa kwa wingi wake karibu na kila afisi ya serikali.Majengo na asasi za umma vyote vimo katika hali mbovu- vyote ni mali ya kila mtu, kwa hivyo si mali ya yeyote.

Ikiwa utataka kuchukua raslimali haba zilizopo katika jamii na kuzivuruga, kile ifaacho kufanya ni kuichukua hiyo raslimali kutoka kwa watu walioizalisha au wale walioitafuta na kuipa halmashauri fulani jukumu la kuisimamia. Kwa pigo moja, utaweza kuharibu kila kitu.


KANUNI YA TATU: Sera nzuri yatuhitajia kutia maanani athari za baadaye na kwa watu wote, na wala si athari za sasa na kwa watu wachache.

Labda ni kweli, kama mwanauchumi wa Uingereza John Maynard Keynes alivyosema, "hatimaye sote tu wafu".

Lakini hali hii isiwe ni kibali kwetu kuanzisha sera zinazowafanya watu wachache kufaidi sasa huku watu wengi wakija kuhasirika kesho.

Naweza kufikiria sera nyingi za aina hizi.Lyndon Johnson alipoivunja jamii ya Great Society, fikira ilikuwa kwamba kunao watu ambao wangefaidi leo kutokana na hundi ya utunzi wa wahitaji.Tunafahamu sasa kuwa kwa muda mrefu, muungano uliopigania utunzi wa wahitaji ulizalisha hali ya kulaza damu, kuvunjika kwa familia, vizazi kutegemea vingine na hali ya kutojiweza,walipa ushuru kutozwa zaidi, na kuzalisha hali mbovu na zisizo razini za kitamaduni ambazo zitakuja kuondoshwa baada ya vizazi vingi. Vivyo hivyo, sera za kutumia zaidi ya mapato na ukuzaji wa serikali- huku zikiwatajirisha watu wachache- ni hali ambazo zimeharibu uchumi wa nchi na kuondoa hali ya kuwa na mbeko kwa miongo.

Mnamo mwaka wa 1992 serikali ya Kenya ilifyatua manoti ya pesa ili kugharamia uchaguzi.Athari za hali hii ni kuvurugwa kwa hali yake ya kiuchumi na kimaendeleo ambayo yahisika hata sasa. Makampuni mengi yamefungwa, wafanyikazi wakapunguzwa na inavyoonekana ni kuwa hapana yeyote atakayekujua kiini asilia hasa cha matatizo yote haya. Katika kiwango cha kibinafsi, wale katika nyinyi mnaokunywa pombe nyingi mwaweza kusema kuwa kadiri mnapokunywa tena na tena ndipo mnapojihisi vema zaidi. Mnachangamka na kufurahi, lakini athari za huu unywaji uliokithiri zinahisika keshoye- hang'ova, ambapo mtu hujikuta anasikitika kwa kunywa zaidi.

Kanuni hii ni mwito hasa kwetu tuwe makini katika fikira zetu. Inasema kuwa hatupaswi kuwa twafanya maamuzi kijuujuu.Ikiwa mwizi ataiba pesa zozote kutoka benki hadi nyingine na kisha kuzitumia pesa hizo madukani kijijini pake, hutakuwa unafikiria vema ikiwa kitu cha pekee ambacho utafanya ni kuwachunguza wenye maduka na kuhitimisha kuwa mwizi huyo ameuinua uchumi.

Twafaa kukumbuka kwamba leo ni kesho ambayo watunga sera waovu wa jana walituambia kuwa tungepuuza. Endapo tutataka kuwa watu wazima wanaoweza kutegemewa, hatupaswi kujitunza kama vitoto vilivyozaliwa juzi na ambavyo nia yake hasa imeelekezwa kwavyo na kwa sasa na hapa.


KANUNI YA NNE: Unapohimiza kitu, unakipata kwa wingi wake; unapokichukia kitu, unakipata kwa uchache wake.

Wewe pamoja nami tukiwa binadamu ni viumbe wanaokwenda na vivutio na vikataza kuvutiwa Tunakwenda na vivutio na vikataza kuvutiwa. Tabia yetu inaathiriwa na hivi vitu viwili, wakati mwingine kwa nguvu kubwa sana. Watunga sera wanaosahau hili hujikuta wamefanya mambo ya kipumbavu kama vike kuongeza ushuru kwa shughuli fulani na kutegemea kuwa watu wakubali hali hiyo jinsi walivyozoea, kana kwamba wao ni kondoo waliopiga foleni kunyolewa.

Kule Marekani, George Bush (wa kwanza) alipolazimishwa kuondoa ahadi yake ya mwaka 1988 ya "No New Taxes" yaani "Hapana ushuru mpya", kulitokea nyongeza kubwa ya ushuru msimu wa sama wa mwakani 1990. Bunge la Marekani (congress) liliongeza ushuru kwa mashua, ndege na vito vyenye thamani miongoni mwa vitu vingine. Walifikiria kuwa kwa kuwa ni matajiri wanaonunua vitu kama hivi, lazima wavinunue kwa ushuru wa juu. Walitegemea kupata dola milioni thelathini na moja kama pato kutokana na ushuru mpya kwa vitu hivi vitatu tulivyoviorodhesha. Tunajua sasa kuwa makusanyo haya ya juu yalizalisha dola milioni kumi na sita pekee ambapo jumla ya dola milioni ishirini na nne zilitumika katika kuwalipa watu waliopoteza kazi kutokana na kufurishwa kwa viwanda kufuatia ongezeko la ushuru.Ni katika serikali pekee ambapo watunga sheria mara kwa mara husahau umuhimu wa vivutio, wakaweza kuwa na azimio la thelathini na moja, wakapata kumi na sita pekee, na kisha wakatumia ishirini na nne ili kuipata na halafu kufikiria kuwa wamefanya vema.

Je, wataka kuvunja familia? Mtuze baba vema pale anapoivunja familia yake, Je, wataka kupunguza akiba na uwekezaji? Toza ushuru mara mbili kwa shughuli hizi, na kisha ongeza ushuru wa kuwa na pesa nyingi. Je, wataka kupunguza kazi? Iwekee adhabu kali ya ushuru kiasi cha watu kuamua kuwa haifai tena kufanya kazi.


KANUNI YA TANO: Hapana mtu atumiaye pesa za mtu mwingine kwa uangalifu jinsi anavyozitumia zake mwenyewe.

Je, ni vipi ambavyo wewe huzitumia pesa zako za marupurupu unapokuwa kwenye shughuli za kiserikali au kikampuni? Je, umewahi kufikiria ni kwa nini wafanyakazi serikalini watahiari kuishi kwenye hoteli za viwango vya chini na kisha kutafuta risiti ambazo hazikuandikwa ili waweze kuhalalisha matumizi mengine? Ukiona jinsi serikali yako inavyotumia pesa kwa miradi, utatarajia nini?

Marekani kunatambwa hadithi za jinsi serikali inavyonunua nyundo na vyoo vinavyogharimu dola 600 na 800 mtawalia. Hapana popote ulimwenguni ambapo utapata mtu akitumia kwa kupenda, hela kama hizi kwa kununua nyundo au choo. Lakini hutendeka serikalini na wakati mwingine kokote kule ulimwenguni pia. Mbona? Kwa sababu, kimazoea anayezitumia fedha hizi anatumia fedha za mtu mwingine.

Mwana uchumi Milton Friedman alifafanua hali hii wakati fulani uliopita aliposema kuwa kunazo njia nne pekee za kutumia pesa. Unapozitumia pesa zako mwenyewe kwa manufaa yako, unafanya makosa ya hapa na pale lakini ni machache na yanaweza kupuuzwa. Kiungo kati ya yule aliyezichumia, yule anayezitumia, na yule anayepata manufaa ya hatimaye, ni cha nguvu mno.Unapozitumia pesa zako kumnunulia mtu mwingine zawadi, unacho kivutio cha kuweza kupata thamani ya pesa zako lakini huenda usipate kitu ambacho mpokezi aliyelengwa anataka hasa au anathamini. Unapotumia pesa za mtu mwingine ili kujinunulia kitu, kama vile mankuli ya mchana bila kupewa viwango vya hela za kutumia, unakuwa na kivutio fulani cha kupata kitu kifaacho lakini hutakuwa na sababu kubwa ya kutokuwa mbadhirifu. Hatimaye, unapotumia pesa za watu wengine ili kununua kitu kwa manufaa ya mtu mwingine, uhusiano baina ya mtu aliyechuma, anayetumia kununulia vitu na anayepokea kulichonunuliwa ni wa mbali- kunao uwezekano mkubwa sana wa ujanja na kufuja. Fikiria hali hii - mtu kutumia pesa za mtu mwingine kumfaidi mtu mwingine tofauti. Hivyo ndivyo serikali ifanyavyo kila mara, kwa kuwa ni serikali.

Lakini kanuni hii si tu kwamba ni maelezo kuhusu serikali. Nakumbuka wakati mmoja, zama za 1993-94 wakati ambapo kituo cha Mackinac Center kilitazama shughuli za shirika la elimu la Michigan Education Association kuhusu hoja ya kujitegemea kwamba lingepinga ushindani wowote ule ambao ungeandikisha huduma zozote zile zilizonuiwa kuunga mkono huduma za shule (kama vile ununuzi wa basi, chakula au ulinzi) na wilaya ya shule yoyote wakati wowote na mahali popote. Tuligundua kwamba pale East Lansing ambayo ni makao makuu ya kifahari ya MEA, muungano haukuwa na watunza na wafanyikazi wa chakula wa kudumu na ambao walikuwa wanachama wa chama cha wafanyikazi. Muungano huu ulikuwa ukipeana mikahawa, utunzi, ulinzi na upelekaji barua kwa makampuni ya kibinafsi, na ambapo asilimia 75 ya makampini haya yalikuwa na watu wasio wanachama wa vyama vya wafanyikazi.

Kwa hivyo MEA- muungano mkubwa zaidi wa wapishi, watunza, madereva wa mabasi na walimu nchini- ulikuwa ukifanya kitu kimoja kwa matumizi ya pesa zake huku ukitaka kuwe na kitu tofauti kabisa kuhusiana na pesa za walipa ushuru wa umma. Hapana mtu - na rudia, hapa mtu- ambaye hutumia pesa za mtu mwingine kwa uangalifu namna anavyozitumia zake.


KANUNI YA SITA: Serikali haina chochote cha kumpa yeyote isipokuwa kile ambacho inachukua kwanza kutoka kwa mtu fulani, na ile serikali ambayo ni kubwa kiasi cha kukupa kila kitu unachokitaka ni kubwa kiasi cha kuchukua kila kitu ulichonacho.

Huu si msimamo mkali, wala wa kiitikadi, na unaopinga serikali. Hii ndivyo hali ya mambo ilivyo. Inazingumzia pakubwa kuhusu hali halisi ya serikali. Kunao mtafaruku mkubwa nchini Kenya kuhusu pendekezo la serikali la kutoa bure elimu ya msingi. Walimu wakuu wa shule pamoja na viongozi wengine wamekuwa wakiuliza kama pesa za kuendesha elimu hii zitatoka wapi. Kanuni hii ya sita yaweka wazi ukweli kuwa hata pale ambapo serikali ingeweza kutoa elimu ya "bure", umma utalipia kupitia kwa njia nyingine. Endapo watakuwa waangalifu, watashangaa kuona jinsi ilivyo ghali kwa serikali kutoa huduma kama hizi.

Kunao wakati ambapo George Washington aliwahi kusema, "serikali haihusu mantiki. Inakwenda na ufasaha. Inatumia maguvu. Ni kama moto, unaoweza kuwa ni hudama hatari au mwajiri sugu". Fikiria hilo kwa muda. Washington alikuwa akisema kuwa hata kama serikali si kubwa kama alivyoitegemea kuwa na hata kama inafanya kazi yake vema zaidi kiasi cha kuwa kweli ni mhudumu kwa watu, bado ni hatari! Kama mchekeshaji Groucho Marx alivyowahi kusema kuhusu nduguye wa kiume Harpo, "Yeye ni mwaminifu,lakini unahitaji kuhusiana naye kwa tahadhari".Wafaa kuwa mwangalifu kwa serikali bila kujali kama ni nzuri zaidi au ndogo kwa sababu, kama alivyoonya Jefferson,ni tabia ya serikali kukua na ina uhuru wa kurudi nyuma. Endapo nitaruhusiwa kuongeza nukuu jingine kwa fikira hii, alikuwa ni Alexander Hamilton ambaye alitwambia kwa busara kuwa, " kumteka binadamu bakunja kunahusu kuteka matamanio yake".

Kile kinachoitwa "Nchi ya ustawi wa jamii" si chochote ila kumpokonya Peter na kumlipa Paul, baada ya kuvuruga na kutumia vibaya utajiri wa Peter kupitia kwa urasimu mbaya na mbadhirifu.Mwanauchumi WalterWilliams aliwahi kusema kuwa 'nchi ya ustawi wa jamii' ni kama kulisha korobindo kupitia kwa farasi. Ama njia nyingine ni kama sisi sote kusimama kwenye mviringo mkubwa na kila mmoja wetu akiwa ameutia mkono wake mfukoni mwa mwenzake. Kunaye mtu aliyewahi kusema kuwa nchi ya ustawi wa jamii inaitwa hivyo kwa sababu ndani yake wanasiasa hupata kile wakitakacho huku sisi wengine tukilipia huduma hizo.

Watu walio huru na wenye kujitegemea hawaitegemei serikali. Wanaiona serikali siyo kama chemichemi ya vitu vya 'bure' bali kama mlinzi wa uhuru wao, na ambao unafungamanishwa na majukumu fulani madogo ambayo huzunguka katika uwekaji usalama, kumpa kila mtu haki yake, huku ikimwacha kila mmoja wetu huru. Kunayo hatari ya kutegemea serikali kama ambavyo staarabu kama zile za Roma ya kale zilivyodhihirisha kwa uchungu.

Mbunge wako ajapo nyumbani na kusema, "Tazama kile nilichokuleteeni!" sharti muombe kujua kutoka kwake kama ni nani anayekigharamia. Kama kweli anasema haki atakwambia kuwa sababu ya pekee iliyompa kupata hicho kitu fulani ni kule kukipigia kura dhidi ya wabunge wenginewaliokitaka pia- na kwamba wewe wakilipia hicho kitu pia.

KANUNI YA SABA: Uhuru ndio msingi wa mahusiano yote ulimwenguni.

Endapo kanuni sita za mwanzo hazikutoa mwanga tosha, nimeongeza hii kama kanuni yangu ya saba na ya mwisho.

Uhuru si tu ufahari au wazo zuri. Ni zaidi ya tukio la furaha au dhana inayotetewa. Ni kile kiwezeshacho vitu vingine vyote kutendeka.Bila uhuru, maisha yachukiza. Ikizidi, hapana maisha bila uhuru.

Sera ya umma ambayo haitilii maanani uhuru au ambayo haitunzi au kutilia nguvu uhuru yafaa kushukiwa mara moja na mtu aliye makini.Watu wafaa kuwa wauliza, "Ni nini tunachokipata pale tunapoulizwa kudondosha baadhi ya uhuru wetu?" Bila shaka si tu vivutio vya sasa au "mkorogo wa mambo". Ben Franklin alipiga hatua katika kutushauri kuwa "Yule anayeacha uhuru muhimu ili kupata usalama mdogo wa sasa hastahili uhuru wala usalama".

Mara kwa mara siku hizi, watunga sera hawafikirii hata kuhusu hali jumuishi ya uhuru wanapotunga sera mpya. Kama inafurahisha au inahisika vema au inawapelekea kuchaguliwa wanafanya hivyo.Endapo kutakuwa mtu ambaye atapinga mambo kuhusu uhuru atachekwa au kupuuzwa. Leo hii, serikali ya Amerika katika viwango vyake vyote hutumia zaidi ya aslimia 42 ya kile kinachozalishwa na wananchi wa Amerika- hii ni kulinganisha na tuseme asilimia 6 au 7 pale mwakani 1900. Mbali na hali hii, utapata kuwa kunao watu wachache sana wanaoelekea kutaka kuuliza wale wanaopigania mamlaka makubwa kwa serikali swali muhimu kama vile, "Mbona asilimia 42 haitoshi?", "Je, ni asilimia ngapi zaidi unayoitaka?", au "Je, katika fikira zako unafikiri ni kiwango gani cha chumo ya mtu ambacho mtu huyo anastahili kupata?"

Ninafuraha kuwa IREN imejitolea katika kuendeleza kanuni hizi katika eneo la Afrika Mashariki. Nina imani kuwa kanuni hizi zinao umuhimu mkubwa.Kwa muda mwingi katika historia ya Amerika, Wamarekani wamezipa kipaumbele na hiyo ndiyo sababu wao ndio watu wenye lishe bora zaidi, mavazi bora zaidi, na makazi bora zaidi kuliko watu wote ulimwenguni kote. Nakuombeni msaidie IREN katika kusambaza mawazo haya nchini Kenya, na mtashangazwa na jinsi ambavyo yatapokelewa vema na kutumikizwa. Nashukuru kwamba nimepata fursa ya kujadili mawazo haya pamoja nanyi leo, na nawashukuru kwa yote mtakayofanya kuanzia leo ili kuweza kuyatumikiza kwa wote.

Kwa habari zaidi tazama www.irenkenya.org kwenye mtandao au andika kwa IREN, S.L.P. 135, GPO 00100, Nairobi.




© Copyright 2004,
Inter Region Economic Network, Nairobi, Kenya, All Rights Reserved.